Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-05-09 17:40:19    
China yaadhimisha Siku ya Kusoma Vitabu Duniani

cri

Tarehe 23 Aprili ni Siku ya Kusoma Vitabu Duniani. Ili kuadhimisha siku hiyo Shirikisho la Maktaba, Shirikisho la Hakimiliki za Kunakili, Shirikisho la Waandishi wa Vitabu na Shirikisho la Wachapichaji yalifanya shughuli nyingi.

Wasikilizaji wapendwa, mliyosikia ni sauti ya kusoma vitabu katika Tamasha la Kusoma Makala Maarufu lililofanyika uwanjani mbele ya maktaba ya taifa ya China mjini Beijing. Waandishi wakubwa wa vitabu Bw. Zhang Kangkang, Liang Xiaosheng na wengine wakiwa pamoja na wanafunzi wa vyuo vikuu na shule za msingi walihudhuria tamasha hilo.

Tarehe 23 Aprili, mwaka 2005 ni siku ya maadhimisho ya miaka 10 ya Siku ya Kusoma Vitabu Duniani iliyowekwa na UNESCO, na siku hiyo pia ni maadhimisho ya siku ya kuzaliwa kwa mshairi mkubwa wa Uingereza Bw. Shakespeare na maadhimisho ya siku ya kufariki dunia kwa mwandishi mkubwa wa vitabu wa Hispania Cervantes Saavedra.

Katika miaka ya karibuni, kutokana na uchumi wa China kuendelea kwa haraka, tabia ya jadi ya kusoma vitabu imeathiriwa vibaya kutokana na maisha bora, mabadiliko ya mwelekeo wa matumizi pesa, michezo mingi ya televisheni, mtandao wa internet na michezo ya elektroniki. Kutokana na hali hiyo, mwaka 1997 China ilianzisha "mradi wa kuongeza elimu" kwa kuwataka "wananchi wasome vitabu na wajenge jamii yenye tabia ya kusoma vitabu", na iliutangaza mwezi Desemba kuwa ni "mwezi wa kusoma vitabu" nchini China, kwa kuchangiwa na shughuli za Siku ya Kusoma Vitabu Duniani ikitarajia kupata mazingira ya "kupenda kusoma, kusoma vitabu vingi na kusoma vitabu bora" katika jamii nzima nchini China. Katibu mkuu wa Shirikisho la Maktaba la China Bi. Tang Gengshen alisema,

"Tokea siku ya kusoma vitabu duniani itangazwe hadi sasa, nchi 100 zimeshiriki kwenye maadhimisho hayo. Shirikisho la Maktaba lilifanya shughuli nyingi za kuwahamasisha wananchi kusoma ili kuifanya jamii ya China iwe na tabia ya kusoma."

Tofauti na miaka iliyopita, shughuli za maadhimisho ya siku ya kusoma vitabu duniani zimechanganywa na shughuli za kuhifadhi hakimiliki. Bw. Shen Rengan ni mkurugenzi mkuu wa bodi ya wakurugenzi ya Shirikisho la Wachapishaji la China, alipohojiwa na waandishi wa habari alisema, China imefanya kazi nyingi katika hifadhi ya hakimiliki ya kunakili. Mwaka 1991 China ilitunga sheria, mwaka 2001 ilirekebisha sheria hiyo na tarehe mosi Machi mwaka huu sheria nyingine ya "usimamizi wa hakimiliki ya kunakili" imeanza kutekelezwa, hii inamaanisha kuwa kazi ya hifadhi ya hakimiliki nchini China imepanda ngazi mpya. Bw. Shen Rengan alisema,

"Tokea UNESCO ianzishe harakati za kuhifadhi hakimiliki ya kunakili na kusoma vitabu miaka 10 iliyopita, China imetoa mchango mkubwa katika harakati hizo. Katika miaka hiyo sheria za kuhifadhi hakimiliki zimekamilika hatua kwa hatua, watu wanaosoma vitabu wameongezeka, na waandishi wa vitabu pia wameongezeka. Sina wasiwasi kuwa kwa kufanya shughuli hizo za kusoma vitabu, watu wanaoheshimu elimu, maslahi ya waandishi na hakimiliki yao watakuwa wengi zaidi."

   

Tofauti na miaka iliyopita, maadhimisho ya mwaka huu yaliongeza harakati nyingine ya kusaidia sehemu maskini kwa vitabu. Katika miaka ya karibuni hali ya kukosa vitabu katika sehemu ya magharibi ya China na sehemu nyingine maskini imetiliwa maanani katika jamii. Idara nyingi na waendeshaji wengi wa mashirika wametoa misaada ya kujenga maktaba na kutoa vitabu kwa ajili ya sehemu hizo. Mkuu wa Shirikisho la Maktaba alitoa tuzo ya sifa kwa watu mashuhuri wa Hong Kong Bw. Shao Yifu, Shi Jingyi na wengine kama ni mfano kwa wengine.

Katika siku hiyo, maduka mengi makubwa ya vitabu mjini Beijing yalifanya mihadhara na kusoma mashairi. Mwanafunzi mmoja wa chuo kikuu Bi. Li Wei alisema kuwa ingawa jamii ya kisasa inawapatia watu huduma mbalimbali za burudani, lakini vitabu pia ni ngazi ya maendeleo, vinasaidia watu kuongeza elimu na kupata hekima. Alisema,

"Vitabu ni chimbuko la elimu, vitabu vinatupatia elimu nyingi ambayo haipatikani katika maisha ya kawaida. Nitachukulia vitabu kama ni rafiki yangu mwema na nitaishi navyo mpaka itakapozeeka."