Kabla ya kuwaletea barua tulizozipokea, tunapenda kuwaarifu wasikilizaji wetu kuwa, toleo la kwanza la jarida dogo la Daraja la Urafiki mlilokuwa mkilisubiri kwa hamu limeshapishwa na litaanza kutolewa wiki ijayo. Baada ya siku chache zijazo, tutawatumia wasikilizaji wetu wengi jarida hilo. Kwenye toleo la kwanza la jarida hilo tumechapisha risala ya mwaka mpya aliyoitoa mkuu mpya wa Radio China kimataifa Bwana Wang Gennian, barua, makala na mashairi tuliyopokea kutoka kwa wasikilizaji wetu na makala chache zinazojulisha utamaduni na vivutio nchini China.
Kutokana na uzoefu wetu mdogo, kutakuwepo na dosari kidogo kwenye toleo la kwanza la jarida hilo, na huenda lisiwavutie wasikilizaji wetu kama tunavyotaka. Tunawaomba wasikilizaji wetu watakaotumiwa jarida hilo, watuvumilie kwa hilo na wawe tayari kutoa maoni na mapendekezo yao. Polepole ndio mwendo, tuna imani kuwa, kutokana na juhudi za pamoja za wasikilizaji wetu, tutaweza kuboresha siku hadi siku jarida hilo ili liwavutie na kuwafurahisha wasikilizaji wetu na kuwa daraja halisi la urafiki kati ya Radio China kimataifa na wasikilizaji wake.
Msikilizaji Yohana Lulyalya Sayii wa sanduku la posta 116 Ng'wang'wali Bariadi Tanzania ametuletea barua akisema kuwa, anashukuru sana kwa radio China Kimataifa kuwapatia wasikilizaji fursa ya kutoa maoni na mapendekezo kuhusu kuboresha vipindi mbalimbali vya idhaa ya kiswahili ya Radio China kimataifa, hasa kuhusu jarida la Daraja la Urafiki.
Yeye anaunga mkono kwa kufanikisha mambo mengi ambayo watazidi kupendekeza katika jarida letu. Na ametuletea shairi lenye sehemu mbili, sehemu ya kwanza inahusu lugha na ya pili inahusu urafiki. Pia anaomba kuwe na jopo ambalo litashughulikia na kuboresha maswala mbalimbali katika jarida la Daraja la Urafiki.
Yeye Yohana Lulyalya Sayii anajipendekeza awemo katika jopo hilo ili kuboresha jarida hilo, kwa kuchangia mambo mbalimbali ambayo yatakuwa na mvuto kwa wasomaji wa jarida hilo duniani, kwani idhaa hii haina ubaguzi. Na anaitakia Radio China kimataifa izidi kupasua mawimbi ulimwenguni kote hadi sayari ya mwisho.
Shairi lake linasema hivi:
Lugha hii ni ya mbele, idhaa nyingi hutangaza
Walakini pole pole, wasomi nao huhimiza
Kitu ubora milele, lugha hii kuhimiza
Nakufikia kileleni, ni CRI yatangaza
Tudumishe urafiki, kwa lugha yetu kiungo
Kiswahili kina sifa, kwa nahau na maana
Huyafanya mataifa, mengi kusikilizana
Kikitoa taarifa, kwa wengi huwa bayana
Tena kinaleta sifa, kwa kuitangaza China
Tudumishe urafiki, kwa lugha yetu kiungo
Urafiki jambo zuri, vitu vyote huungika
Chemchem husafiri, kutafuta ushirika
Mto mwenziwe bahari, kiangazi kwa masika
Mchina mie fahari, urafiki kuuweka
Akutakaye mtake, vibaya kumuacha
Nami sina makeke, kwa jambo ninalotaka
Natamani nifike, kukomaza ushirika
Mkono wako nishike kama ulivyo tunuka
Nimesoma na shairi, katika wako waraka
Sikuona dosari, hata mwisho nikafika
tungo yako ni nzuri, inapaswa kusifika
Urafiki ni mzuri, mambo mengi kusifika
Msikilizaji wetu Wallace Masanja wa sanduku la posta 85 Sikonge Tabora Tanzania anasema katika barua yake kuwa, yeye ni miongoni mwa wasikilizaji wa Radio China kimataifa inayowarushia matangazo kutoka Beijing kwa kupitia masafa mafupi. Anapenda kutoa mapendekezo yake juu ya uandaaji wa jarida dogo la Daraja la Urafiki. Mapendekezo yake ni kama yafuatayo:
Kwanza anaomba jarida la daraja la urafiki liwe tayari kupokea maswali mbalimbali kutoka kwa wasikilizaji wetu, na baadaye kujibiwa nasi katika toleo linalofuata. Kwani kwa kufanya hivyo itawasaidia wasikilizaji wote wanaoishi katika dunia ya tatu kuweza kufahamu mambo mbalimbali, kwani yeye ni mmoja wapo anayependa kutambua ni jinsi gani ulimwengu unavyokwenda.
Pili anaomba katika uandaaji wa gazeti dogo la daraja la urafiki liwe na sehemu maalum itakayowapa wasikilizaji nafasi ya kuweza kutuma salamu kupitia gazeti hilo. Kwani kwa kufanya hivyo ndugu watangazaji wataweza kuongeza wasikilizaji wa CRI. Hayo ndio mapendekezo yake katika uandaaji wa gazeti dogo la daraja la urafiki.
Tunaona mapendekezo yake yote ni mazuri ambayo yatasaidia kazi yetu ya kuhariri na kuchapisha gazeti letu dogo la daraja la urafiki, tunamshukuru sana. Ni matumaini yetu kuwa wasikilizaji wetu watatuletea maoni na mapendekezo baada ya kusikiliza matangazo, kutembelea kwenye tovuti na mengineyo.
Na msikilizaji wetu Hilal Nasor Zahor Al Kindy wa sanduku la posta 119 Al Amrat Oman, ametuletea barua akisema kuwa, anashukuru iwapo tutachapisha shairi lake hilo kwenye jarida dogo la daraja la urafiki, shairi lake hilo lina kichwa kinachohusu Maji
Hakika maji yakiadimika binadamu ana taabu
Mungu katupa riziki yake kwetu
Kila kitu kinahitaji maji sana
Bila ya maji maisha yana taabu
Mwili wa binadamu ni kiasi cha 75 % ya maji
Maji lazima tuyahifadhi sana
Maji pia yahitajiwa na ndege na miti
Nyumba huwezi kujenga bila ya maji
Tena maji yahitajiwa kwa mwili
wa binadamu na wanyama
Kwa hiyo nawaomba wote tuyatunze
na tuyatumie kwa manufaa
Tunamshukuru sana kwa shairi lake hilo linalowaonya watu wa dunia nzima wathamini maji ambayo ni kitu kisichoweza kukosekana katika maisha ya watu na uzalishaji mali.
Idhaa ya kiswahili 2005-05-10
|