Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-05-10 11:26:05    
Barua 0510

cri
Kabla ya kuwaletea barua tulizozipokea, tunapenda kuwaarifu wasikilizaji wetu kuwa, toleo la kwanza la jarida dogo la Daraja la Urafiki mlilokuwa mkilisubiri kwa hamu limeshapishwa na litaanza kutolewa wiki ijayo. Baada ya siku chache zijazo, tutawatumia wasikilizaji wetu wengi jarida hilo. Kwenye toleo la kwanza la jarida hilo tumechapisha risala ya mwaka mpya aliyoitoa mkuu mpya wa Radio China kimataifa Bwana Wang Gennian, barua, makala na mashairi tuliyopokea kutoka kwa wasikilizaji wetu na makala chache zilizojulisha utamaduni na vivutio nchini China.

Kutokana na uzoefu wetu mdogo, kutakuwepo na dosari kidogo kwenye toleo la kwanza la jarida hilo, na huenda lisiwavutie wasikilizaji wetu kama tunavyotaka. Tunawaomba wasikilizaji wetu watakaotumiwa jarida hilo, watuvumilie kwa hilo na wawe tayari kutoa maoni na mapendekezo yao. Polepole ndio mwendo, tuna imani kuwa, kutokana na juhudi za pamoja za wasikilizaji wetu, tutaweza kuboresha siku hadi siku jarida hilo ili liwavutie na kuwafurahisha wasikilizaji wetu na kuwa daraja halisi la urafiki kati ya Radio China kimataifa na wasikilizaji wake.

Sasa tunawaletea barua tulizopokea kutoka kwa wasikilizaji wetu. Tunaanza na barua ya msikilizaji wetu Marianus Mhagama wa Tanzania ambaye ametuletea barua pepe ikisema kuwa, anafurahi sana kutembeela tovuti yetu kwenye mtandao wa internet, ambapo aliona jinsi ambavyo tunafanya kazi kubwa ya kutafsiri na kurusha matangazo kwa lugha ya Kiswahili.

Anapenda kutoa mapendekezo mawili, kwanza anashauri matangazo yetu yaliyoko kwenye tovuti (akiwa na maana taarifa ya habari) iwe ni matangazo ya moja kwa moja, badala ya ilivyo sasa ambapo habari hurekodiwa. Kama inawezekana, basi yawe ni matangazo yanayohusu mambo mengi kama vile michezo, utamaduni, uchumi, siasa na kadhalika badala ya habari peke yake. Pili, anashauri kuweko na matangazo yetu katika jiji la Dar es Salaam. Anasema ni bahati mbaya sana kuwa Dar es Salaam hawapati matangazo yetu kwa njia ya FM, ingekuwa ni vizuri sana kama yangepatikana kwa njia ya FM.

Kuhusu ushauri wake wa kuyafanya matangazo yawe moja kwa moja, labda kwa hivi sasa bado haiwezekani kwani muda wa matangazo yetu ni ya muda wenye kikomo, tena masafa ya matangazo ni ya mafupi, tunapaswa kutumia kila dakika hata kila nukta za matangazo yetu bila kupoteza muda kutokana na makosa ya kutangaza na marudio yake.

Hali ya radio nyingine duniani ni tofauti na hali yetu, kwani baadhi yao zimepata nafasi za ushirikiano na radio mbalimbali huko Dar es Salaam au huko Zanzibar, zimekuwa na muda wa kutosha kutangaza moja kwa moja kwa wasikilizaji wao. Idhaa ya Kiswahili ya Radio China kimataifa iliwahi kufanya juhudi za kutafuta ushirikiano huko Dar es Salaam lakini kutokana na sababu mbalimbali hatukufanikiwa. Lakini tumeambiwa kuwa, Radio China kimataifa inafanya juhudi kutafuta ushirikiano na nchi mbalimbali ama kuanzisha kituo cha kurusha matangazo yetu barani Afrika, bila shaka vipindi vya idhaa ya Kiswahili vitaongezewa muda na matangazo yetu yataboreshwa na kuwafurahisha zaidi wasikilizaji wetu siku za mbele.

Msikilizaji wetu Abdullahi W. Shabaan wa sanduku la posta 1304 Kakamega Kenya anasema katika barua yake kuwa anatushukuru kwa kumtumia kadi maalum kuhusu utambulisho wa tovuti ya kiswahili pamoja na ratiba ya vipindi. Pia anasema anafahamu kuwa michezo ya Olimpiki ya mwaka 2008 itaandaliwa mjini Beijing, kwa hiyo angeomba tumtumie gazeti linaloonesha maandalizi ya michezo hiyo ya kimataifa.

Tunapenda kumwambia kuwa, kila mara katika taarifa ya habari inayosomwa kila siku kwenye idhaa ya Kiswahili ya Radio China kimataifa na vipindi vya michezo, tunasoma mara kwa mara taarifa kuhusu maandalizi hayo ya michezo ya Olimpiki ya mwaka 2008 itakayofanyika hapa Beijing. Hivi sasa maandalizi yanaendelea kufanyika, na tokea mwaka huu uanze, ujenzi wa viwanja na majumba ya michezo umeanzishwa kwa pande zote mjini Beijing, tutaendelea kuwaletea wasikilizaji wetu habari kuhusu maandalizi hayo, tunaomba radhi kwani kwa sasa hatuwezi kupata gazeti linaloonesha maandalizi hayo peke yake.

Msikilizaji wetu huyo amesema kuwa, mwisho anataka kutujulisha watangazaji na wafanyakazi wote wa idhaa ya kiswahili kuwa sasa yeye na wanachama wenzie wamefanikiwa kutuma barua bila kutumia stempu za nchi yao. Pia anapendekeza kama ikiwezakana wasikilizaji wangepewa kadi maalum ili waitumie kuwasiliana na Radio China kimataifa kama wanavyotuma barua, na kwa upande wa matangazo anaomba tuongeze muda kidogo wa matangazo walau uwe saa nzima, moja ya sababu za ombi hilo ni kusomwa kwa kadi chache za salamu.

Tunashukuru sana kwa mapendekezo yake, tumepokea maombi na mapendekezo mengi kuhusu muda wa vipindi na hata malalamiko kuhusu kipindi cha salamu zenu, hilo kwa sasa linafanyiwa kazi kwa hiyo tunaomba muwe wavumilivu, tunatumai katika siku za baadaye maombi hayo na mapendekezo hayo yatatekelezwa. Na kuhusu suala la simu kwa sasa bajeti yetu ina ukomo kwa hiyo si rahisi kwetu kuwawezesha wasikilizaji watupigie simu bila malipo, kwa sasa tunaomba muendelee na barua.

Vilevile msikilizaji wetu huyo Abdullahi Shaban ametuletea shairi lenye kichwa "Mama wa Kambo", tunapenda kuwasomea wasikilizaji wetu shairi lake ili tujihisi kwa pamoja hisia za msikilizaji wetu huyu.

Hodi hodi mlagoni, mama kambo kaingia

amenituma dukani, huku na matusi tele,

kaniambia jifiche, kwa sababu ya matambara,

kifa baba au mama, ni kipi kilicho bora?

Vitanda tele nyumbani, kaniambia lala chini,

Vyakula tele nyumbani, kanipikia kibaya

Kama mama angekuwa, singeyaona haya.

kifa baba au mama, kipi kilicho bora?

Bwana Abdullah Shaban pia ameandika shairi lingine lenye kichwa cha Kilio, shairi hilo linasema hivi:

Mwanzoni hakuja, kuwaletea kilio,

kilio ni cha mashaka, wenzangu nisikilizeni.

Tisini na tatu baba yangu alinilea

baada ya miaka miwili baba kaaga dunia,

nililia kumfuata, lakini nikatugama taabu nazo nikapata,

na zikanitia huzuni.

Mama yangu alinizaa mtoto, baada ya miaka miwili,

akaaga dunia, nililia kumfuata, lakini nikatugama,

taabu nazozipata, zinanitia huzuni.

Kwa mjomba nilienda mfanyakazi nikawa

hata kwa ndugu nikaenda mchunga ng'ombe nikawa

nilitamani kusoma lakini sikuweza.

Taabu nazo zipata, zinanitia huzuni.

Matambara nguo zangu, vidonda ni mwili wangu

naenda kanisani ili nimuombe mungu,

ili nimuombe Mungu anitoee mashakani,.

Taabu nazozipata zinanitia huzuni.

Msikilizaji wetu huyo ameandika pia hadithi yenye kichwa "Mwizi wa mbuzi" Hadithi inasema

Hapo zamani za kale kulikuwa na mkulima mmoja ambaye alikuwa amefuga mbuzi wengi, kwa bahati mbaya hakuwa na mbwa. Siku moja mwizi alikuja kwa huyo mfugaji, akanyemelea hadi akafika kwenye boma la mbuzi. Alipofika kwenye hilo boma, alimnyatia mbuzi mmoja na kamkamata kiustadi na akakimbia naye.

Na wakati huo wa vurumai, mkulima alisikia na akaamka upesi alipofika kwenye boma la mbuzi, alikuta boma la mbuzi limevunjwa na mbuzi mmoja hayupo, mkulima alikasirika na asiwe la kufanya, akaishia kusema siku za mwizi ni arobaini.

Turudi kwa mwizi tuone kama alifika salama ama vipi, mwizi alipofaulu kazi yake akaona leo siku imekuwa nzuri kwake. Akiwa njiani alikutana na mzee fisi, mzee fisi kuona hivyo akasema leo mawindo yangu hayatafika mbali, alimrukia yule mwizi na akamrarua na kumwua, halafu akamchukua yule mbuzi. Fisi naye akaenda huko akiwa amefurahi kupita kiasi na akamfanya mbuzi huyo kitoweo.

Tunamshukuru sana msikilizaji wetu Abdullahi Shaban kwa mashairi na hadithi alizotuletea. Ni matumaini yetu kuwa Bwana Shaban na wasikilizaji wetu wengine wataendelea kutuletea barua, makala na mashairi ili kutusaidia kuboresha vipindi vyetu kwenye radio na tovuti.

Idhaa ya kiswahili 2005-05-10