Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-05-10 16:48:12    
Moja ya sanaa za jadi za Kichina, uchapaji urembo kwenye kitambaa kwa nta

cri

Uchapaji urembo kwenye kitambaa kwa nta ni moja ya sanaa za kale na za jadi nchini China. Sanaa hiyo ilirithishwa kizazi hadi kizazi na imeenea sana katika mkoa wa Guizhou, kusini magharibi mwa China miongoni mwa watu wa makabila madogo madogo.

Zaidi ya miaka 2000 iliyopita, nchini China kulikuwa na ufundi wa "kuchora maua kwenye vitambaa kwa nta, kisha kutia rangi, na baada ya kuondoa nta maua yakaonekana." Kwenye kitambaa maua yaliyochorwa kwa nta hayashiki rangi, baada ya kuondoa nta maua meupe yanaonekana. Mapema katika Enzi ya Tang (618-907) vitambaa vyenye urembo wa nta vilikuwa vinajulikana sana na viliuzwa barani Asia na hata Ulaya. Kutokana na maendeleo ya uchumi katika sehemu ya kati ya China, viwanda vya kuchapa urembo kwa nta vilitokea na kufanya kazi badala ya mikono, ufundi wa kuchapa urembo kwa mikono katika sehemu nyingi nchini China ukapotea. Kutokana na kuwa mkoa wa Guizhou uko katika sehemu za milimani ambazo zimejitenga na sehemu nyingine, hadi leo ufundi huo unaendelea kizazi hadi kizazi. Ufundi uliotumiwa na urembo uliochorwa mkoani humo wote umerithi uzuri wa siku za kale. Katika vijiji vya Paidao na Paimo wilayani Danzhai karibu wanavijiji wote wanawake tokea wenye umri wa miaka zaidi ya kumi hadi sabini wote wana uzoefu wa ufundi huo, kila wakiwa na nafasi hawaachi kuchora picha mbalimbali kwa nta, na sanaa hiyo ni hadhi ya wasichana kuwavutia wachumba wao.

Vitambaa wanavyotumia wanavijiji hao kutiwa urembo kwa nta ni bafta, na nta wanaipata kutoka masega ya nyuki, rangi ni buluu inayopatikana kutoka kwenye majani ya aina moja ya mmea. Chombo wanachotumia kuchora ni kijiti chenye mdomo wazi kama wa bata kwenye ncha, ili nta iliyoyeyushwa iweze kukaa mdomoni baada ya kuchovya.

Kabla ya kuchora picha za urembo, kitambaa cheupe hutandikwa mezani na sufuria ndogo inayoyeyusha nta inakuwa pembeni, na picha huchorwa kwa kijiti hicho kilichochovya maji ya nta. Aghlabu wenyeji hawana ramani iliyochorwa tayari bali wanachora kwa mujibu jinsi wanavyofikiri, hawatumii lula wala bikari, lakini mistari na duara wanazochora hunyooka na kuwa mviringo sana, na ndege, maua, samaki na vitu vingine vinafanana sana na vitu halisi. Baada ya kuchora, vitambaa vinatiwa ndani ya maji ya rangi kuroweka kwa siku tano au sita hivi, kisha vinatolewa na kuchemshwa, nta ikayeyuka ndani ya maji ya moto na asili ya bafta itaonekana. Kitambaa kilichorowekwa ndani ya maji ya rangi kinakorogwa korogwa, nta inapasuka pasuka na kuacha mipasuko ambayo maji ya rangi yanapenya kwenye bafta. Mipasuko hiyo ni kama roho ya sanaa ya kitamba hicho, kwani hata picha moja ilichapwa kwenye vitambaa tofauti, alama za mipasuko hazitakuwa sawa. Kwa hiyo vitambaa vya bandia vinatambulika mara moja. Watu wanasema, kuchapa urembo kwenye kitambaa kwa nta ni kama mtoto wa tumboni, kwamba unaweza kuwazia sura ya mtoto atakaaje lakini huna uhakika mpaka mtoto azaliwe."

Urembo uliochorwa kwenye kitambaa baadhi ni watu, baadhi ni maua au ndege.

Vitambaa vilivyotiwa urembo wa nta vinatumika sana maishani, kama vile shela, aproni, nguo, sketi, mwamvuli, kitambaa cha foronya, mfuko wa vitabu au mbeleko. Hivi sasa vitambaa vilivyotiwa urembo kwa nta vinapatikana kutoka aina tatu za kazi, moja ni kazi ya wenyeji kwa mikono, nyingine ni kazi ya viwandani kwa ajili ya kuuzwa sokoni, nyingine ni kazi ya wasanii kwa ajili ya burudani.

Hivi sasa "joto la vitambaa vilivyochapwa urembo kwa nta" limekuwa kali zaidi, vitambaa hivyo vinahitajika sana duniani. Lakini kutokana na kuwa kazi nyingi za kuchapa vitambaa hivyo vinafanywa kwa mikono, na haziwezi kufanywa kwa mashine, vitambaa hivyo havitoshelezi mahitaji.

Idhaa ya kiswahili 2005-05-10