Shirika la Kazi la Kimataifa, ILO, tarehe 11 lilitoa ripoti ikisema kuwa hali mbaya ya kulazimishwa kufanya kazi inaendelea kuwepo duniani, kwa hiyo kukomesha kulazimisha kufanya kazi ni changamoto kubwa inayoikabili jumuyia ya kimataifa.
Ripoti hiyo yenye kichwa cha habari "Uundwe Muungano wa Kupinga Ulazima wa Kazi Duniani" imegawa kazi za kulazimishwa katika aina tatu. Aina ya kwanza ni kazi zilizolazimishwa na serikali, jeshi na vikundi vya kijeshi ikiwemo miradi inayowashirikisha umma kwa lazima, aina hiyo inachukua 20% ya ulazima wa kazi duniani. Aina ya pili ni ulazima wa kazi ya ukahaba inayolazimishwa na wafanyabiashara kwa ajili ya unyonyaji, ikiwemo biashara ya ukahaba kwa lazima au kufanya biashara hiyo kwa hiari mwanzoni na baadaye kutoweza kujinasua, watu hao wakiwa ni pamoja na watoto wote wanaofanya biashara hiyo. Aina ya tatu ni kazi zinazolazimishwa na wafanyabiashara binafsi zikiwemo kazi za kulipa deni na kazi za utumishi wa nyumbani. Aina ya kwanza na ya pili zinachukua ulazima wa kazi duniani 11% na 64%.
Ripoti inasema kuwa watu wanaofanya kazi hizo hivi sasa hawapungui milioni 12.3, yaani kila kati la watu 1000 watu wanne wanafanya kazi hizo na kati ya hao wanne watu wasiozidi umri wa miaka 18 wanachukua nusu. Kuna watu milioni mbili na nusu wanaofanya kazi kwa kulazimishwa na serikali na vikundi vya uasi wa kijeshi. Tatizo hilo likichunguzwa kwa jinsia, miongoni mwa watu hao wanawake na watoto wa kike wanachukua 56%, wanaume na watoto wa kiume wanachukua 44%. Miongoni mwa wanaofanya biashara ya ukahaba kwa lazima, 98% ni wanawake na watoto wa kike.
Ripoti inasema kuwa ulazima wa kazi ni tatizo la dunia nzima ambalo lipo katika nchi zote zikiwemo nchi zinazoendelea na zilizoendelea. Watu hao wengi zaidi wako katika Asia na Pasifiki, ifuatayo ni Latin Amerika, sehemu ya Caribean na kusini mwa Sahara barani Afrika. Katika nchi zinazoendelea, kutokana na umaskini kazi za kulazimishwa zinaendeshwa zaidi na watu binafsi kwa ajili ya unyonyaji. Na katika nchi zinazofanya mageuzi ya kiuchumi kazi hizo zinaonekana kwa aina mbili. Ya kwanza ni unyonyaji wa kibiashara ambao unachukua karibu nusu ya kazi zinazolazimishwa; Pili ni biashara ya watu, hii ni njia muhimu ya kusababisha watu wengi kufanya kazi kwa kulazimishwa ambao 75% ya watu wanaolazimishwa kazi wanahusika na biashara ya mauzo ya watu. Hapa duniani kila mwaka fedha zinazopatikana kutokana na biashara ya watu zinafikia dola za Kimarekani bilioni 32 na kati ya fedha hizo bilioni 15.5 zinachukuliwa na nchi zilizoendelea.
Kutokana na kuwa tatizo hilo ni nyeti, nchi nyingi zinakataa kukubali kuwepo kwa tatizo hilo, kwa hiyo kufichua na kutatua tatizo hilo si jambo rahisi, zaidi ya hayo watu husika wengi hawataki kujitokeza kutoa ushahidi kwa sababu wanahofia kulipizwa kisasi au kuachishwa kazi.
Mkuu wa Shirika la Kazi la Kimataifa Bw. Juan Somavia kwenye ripoti hiyo alisema kuwa ulazima wa kazi ni janga, ni tunda baya linalopatikana katika mchakato wa utandawazi, lakini kamwe lisikubalike katika dunia hii ya leo. Alisisitiza kuwa kuwaadhibu wanaowalazimisha watu hao ni mawazo ya pamoja duniani, lakini kutokana na kutokuwepo kwa mpaka ulio wazi kati ya kazi zinazolazimishwa na kazi za kawaida, kwa hiyo ni vigumu kuwashitaki.
Mwishoni mwa ripoti hiyo inasema kuwa ili utandawazi uwe wa uadilifu na kuwaletea watu wote "kazi ya heshima" ni lazima kukomesha kazi za kulazimishwa.
Idhaa ya kiswahili 2005-05-12
|