Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-05-12 16:58:23    
Jinsi wakazi wa Mji wa Lanzhou wanavyopenda Tambi

cri

Lanzhou ni mji mkuu wa mkoa wa Gansu, kaskazini magharibi mwa China. Tukiutaja mji wa Lanzhou, watu wengi watakumbuka chakula maarufu cha mji huo, yaani tambi zenye nyama za ng'ombe. Tambi zenye nyama ya ng'ombe si kama tu zinapendwa na wakazi wa Lanzhou, bali pia zinakaribishwa sana na wachina kote nchini na hata wanaoishi ng'ambo, hii ni fahari ya wakazi wa Lanzhou.

Mjini Lanzhou, mikahawa ya tambi zenye nyama za ng'ambo inaonekana hapa na pale, wateja wanaosongamana na tambi zinazonukia ni jambo la kawaida wakati wa asubuhi kwenye mikahawa ya Lanzhou. Wafanyakazi, wazee na wanafunzi wote wanapenda kula tambi kabla ya kwenda kazini au shuleni.

Bwana Shi Feng anafanya kazi katika kituo cha utamaduni cha Lanzhou, mke wake ni mhasibu, binti yake anasoma katika chuo kikuu cha Lanzhou. Hivi sasa hali ya maisha ya familia ya Bw. Shi Feng imeinuka, kula chakula katika mkahawa ni jambo la kawaida, lakini wanafamilia wake wote wanapendelea tambi zenye nyama za ng'ombe kuliko vyakula vingine.

"Nimeishi mjini Lanzhou kwa miaka zaidi ya 30, karibu kila asubuhi nakula tambi zenye nyama za ng'ombe. Tambi hizo si kama tu ni za bei rahisi, bali pia zinasaidia kujenga afya."

Tambi za Lanzhou huchemshwa kwenye supu ya nyama za ng'ombe, na kukolea kwa vipande vya figili nyeupe, pilipili nyekundu na kisibiti, na kuifanya tambi ionekane ina rangi ya kupendeza.

Upikaji wa tambi za Lanzhou unazingatia sana supu yake. Supu ya nyama za ng'ombe hutengenezwa kwa kuweka viungo kumi kadhaa, sifa ya supu yenyewe ndiyo sifa ya mikahawa ya tambi, mikahawa mbalimbali hutofautiana kutokana na ladha mbalimbali za supu. Hivyo namna ya kupika supu ndiyo siri ya biashara ya mikahawa mbalimbali. Bwana Hao Yanshi ni mpishi maarufu wa tambi za nyama ya ng'ombe, ustadi wake wa kupika supu hiyo umerithishwa kutoka kwa babu yake na baba yake. Licha ya supu, ustadi wa kutengeneza tambi pia ni muhimu sana. Bwana Hao Yanshi anasema:

"Hatua ya kwanza ya kutengeneza tambi ya kukoroga na kukanda unga wa ngano, namna ya kuvuta tambi ni ustadi mwingine muhimu. Mpishi hawezi kutengeneza tambi vizuri kabla ya kujifunza kwa zaidi ya mwaka mmoja."

Tambi zenye nyama za ng'ombe si kama tu ni chakula cha jadi cha wakazi wa Lanzhou, wageni wakifika Lanzhou kwa muda pia wanavutiwa na tambi hizo. Msichana Dong Yu anatoka mkoa wa Zhejiang, mashariki mwa China, ameishi mjini Lanzhou kwa miaka 6, sasa anapenda sana kula tambi zenye nyama za ng'ombe kama wenyeji wa huko. Anasema:

"Nilipokuja mjini Lanzhou, niliona kuwa bakuli la kuwekea tambi ni kubwa mno, sikuweza kumaliza. lakini sasa bakuli moja la tambi halinitoshi. Kila mara nikifika tu mjini Lanzhou kutoka nyumbani kwangu huingia mkahawani kula tambi zenye nyama za ng'ombe."

Hivi sasa, mji wa Lanzhou una mikahawa zaidi ya 1200 ya tambi zenye nyama za ng'ombe. Baadhi ya mikahawa mikubwa inaweza kupata mapato zaidi ya yuan milioni 40 kwa mwaka.

Aidha, matumizi makubwa ya tambi yenye nyama za ng'ombe yamestawisha ufugaji wa ng'ombe, kilimo cha ngano na utengenezaji wa unga wa ngano katika sehemu zilizo karibu na mji wa Lanzhou, ambayo yametoa mchango mkubwa katika kustawisha uchumi wa huko na kuongeza nafasi za ajira. Katika miaka ya hivi karibuni, serikali ya huko imeweka kigezo cha kushughulikia mikahawa ya tambi yenye nyama za ng'ombe, na tayari imesajili chapa ya "tambi zenye nyama za ng'ombe za Lanzhou".

Hivi sasa watu wanaweza kula tambi zenye nyama za ng'ombe ya Lanzhou nchini kote. Kampuni maarufu ya tambi ya Malan imeanzisha mikahawa zaidi ya 400 nchini kote, pia imefungua matawi yake katika nchi za nje kama vile Marekani, Ufaransa na Singapore. Kama ukikuta mkahawa wa tambi ya Lanzhou usichelewe kuingia ndani na kuonja tambi za nyama ya ng'ombe za Lanzhou, bila shaka utazifurahia.

Idhaa ya kiswahili 2005-05-12