Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-05-13 16:25:37    
serikali yawatuma watumishi kuwasaidia wazee majumbani mwao

cri

Takwimu zinasema kuwa, hivi sasa asilimia 10 ya wachina ni wazee wanaozidi umri wa miaka 60. kutokana na China kuingia katika jamii yenye idadi kubwa ya wazee, jinsi ya kuwahudumia wazee imekuwa jambo lisilopuuzika. Katika miaka ya hivi karibuni, idara husika za serikali ya China zimetafuta njia mwafaka ya kuwahudumia wazee majumbani.

Kuwahudumia wazee majumbani kunamaanisha kuwa, serikali za sehemu mbalimbali kugharamia kuwaandaa na kuwatuma watumishi kuwahudumia majumbani kwao wazee wasiokuwa na watoto au wenye matatizo ya kiuchumi ili kuwasaidia waishi kwa furaha.

Bwana Tan Jianzhou mwenye umri wa miaka 79 mwaka huu na mke wake wanaishi Dalian, mji wa pwani wa kaskazini mashariki mwa China. Mji wa Dalian una nyumba kumi kadhaa za wazee, lakini Bw. Tan na mke wake wanashikilia kuishi nyumbani kwao badala ya kwenda kuishi kwenye nyumba za wazee. Anasema:

"Naona huru zaidi kuishi nyumbani, kwangu kwani naweza kutoka nje, kuangalia televisheni na kusikiliza Radio kama nipendavyo. Nikienda kuishi katika nyumba za wazee, japokuwa pia naweza kutazama televisheni, lakini siwezi kutazama mashindano ya mpira kwenye televisheni usiku wa manane kama ninavyokuwa nyumbani kwangu."

Mzee Tan alisema kuwa, wameishi katika mtaa huo kwa muda wa miaka kumi kadhaa, na wanasikilizana vizuri na majirani zao. Kila siku akitoka nje, huamkiana na majirani na kupiga sogo nao bila ya wasi wasi hata kidogo. Lakini katika nyumba za wazee, si rahisi kwake kuwasiliana vizuri na wageni wengine kwa muda mfupi. Mzee Tan anapenda kula mboga zaidi kuliko nyama, akienda kuishi katika nyumba za wazee hawezi kuchagua vyakula apendavyo.

Tofauti na wazee wengine wanaotunzwa na wanafamilia, mzee Tan na mke wake hawataki kuathiri maisha na kazi za watoto wao, hivyo wanamwajiri mtumishi kuwasaidia kufanya kazi za nyumbani. Kwa mujibu wa utaratibu wa mji wa Dalian, mzee anayezidi umri wa miaka 70 kila mwezi atapewa yuan 100 na serikali kwa matumizi ya kumwajiri mtumishi wa nyumbani.

Katika miji mingine kama Guangzhou na Ningpo kusini mwa China, wazee wengi wasiokuwa na watoto au wenye matatizo ya kiuchumi wameanza kutunzwa kabisa na serikali .

Mkazi wa Guangzhou Tang Huifang mwenye umri wa miaka 90 mwaka huu hana watoto, na mume wake alifariki dunia miaka kadhaa iliyopita. Japokuwa mzee Tang ana afya nzuri, anaweza kujisaidia kimaisha, lakini hawezi kufanya kazi nzito za nyumbani. Muda si mrefu uliopita, serikali ya kienyeji ilimtumia mtumishi wa nyumbani.

Mwandishi wa habari alipomtembelea mzee Tang alimkuta mtumishi wake Bibi Liang Kunyan. Mzee Tang alisema kuwa, Bi.Liang licha ya kumsaidia kusafisha nyumba na kufanya shughuli za kawaida, pia anamsindikiza hospitalini kuonana na daktari, na hayo yote yanagharimiwa na serikali . Mzee Tang anasema:

"Nasikia furaha kweli. Nina umri wa miaka 90 mwaka huu, japokuwa sina jamaa, lakini majirani wananitendea vizuri, sasa serikali imenitumia mtumishi kunisaidia kufanya kazi za nyumbani."

Mtumishi Bi. Liang Kunyan ana umri wa miaka 39 mwaka huu, aliwahi kufanya kazi katika duka lililouza chakula na vinywaji, lakini mwaka jana alipunguzwa kazini. Anasema:

"Kuanzia mwezi Januari mwaka huu namsaidia mzee Tang kwa kazi za nyumbani. Kabla ya kufanya kazi hiyo, nilijiunga na mafunzo yaliyoandaliwa na idara inayoshughulikia huduma za jamii ya Guangzhou, ili kujifunza na kufahamu magonjwa yanayotokea mara kwa mara kwa wazee kwa ajili ya kuwahudumia vizuri wazee."

Bi. Liang anapowahudumia wazee, yeye mwenyewe pia amepata kuajiriwa. Kila mwezi anaweza kupata mshahara kutoka idara ya mambo ya raia.

Kuwahudumia wazee nyumbani kwao si kama tu kumewaridhisha wazee matakwa yao ya kuishi nyumbani, bali pia kumeleta nafasi nyingi za ajira kwa jamii, pia kumepunguza matumizi ya serikali ikilinganishwa na kuwatunza wazee katika nyumba za wazee.

Naibu mkurugenzi wa idara husika ya wizara ya mambo ya raia ya China Bwana Yan Qingchun anasema:

"Hivi sasa China bado haiwezi kujenga nyumba za kutosha za wazee, hivyo kuwahudumia nyumbani kwao ni njia mwafaka inayoambatana na hali halisi ya China."

Bw. Yan alisema kuwa, hivi sasa ni kiasi kidogo tu cha wazee wanaoweza kupata huduma hiyo inayogharamiwa na serikali. Kutokana na maendeleo ya uchumi na huduma hiyo inavyopevuka, katika siku za usoni serikali zitatenga fedha nyingi zaidi kuwasaidia wazee walio wengi manyumbani kwao.

Idhaa ya kiswahili 2005-05-12