Tarehe 12 maandamano makubwa ya kuipinga Marekani yalifanyika huko Kabul, mji mkuu wa Afghanistan. Wanafunzi karibu elfu moja walifanya maandamano barabarani wakilipinga jeshi la Marekani kuikashifu Kurani na kuwaua wapinzani. Kuanzia tarehe 10, wanafunzi na raia wa Afghanistan wamefanya maandamano ya kuipinga Marekani katika sehemu mbalimbali nchini humo, na mgogoro ulitokea kati yao na polisi, na kusababisha vifo vya watu 7 na wengine 76 kujeruhiwa. Maandamano hayo ni makubwa kabisa tangu jeshi la Marekani lianzishe vita nchini humo mwezi Desemba mwaka 2001.
Maandamano hayo yalisababishwa na ripoti ya Gazeti la Newsweek la Marekani. Gazeti la Newsweek lililotolewa tarehe 9 lilisema kuwa, kuikashifu Kurani ni njia inayotumiwa mara kwa mara na jeshi la Marekani ya kuwaadhibu wafungwa wa kiislamu huko Guantanamo. Ili kuwaadhibu na kuwafedhehesha wafungwa wa kiislamu, jeshi la Marekani liliitupa Kurani chooni. Baada ya jambo hilo kufichuliwa, waislamu wa Afghanistan walikasirika sana. Habari zinasema kuwa, baada ya tukio la Septemba 11, watuhumiwa wapatao 530 wa ugaidi ambao ni waislamu kutoka Afghanistan na Pakistan, walifungwa na jeshi la Marekani huko Guantanamo.
Maandamano ya kwanza yalifanyika huko Jalalabad, mji mkuu wa mkoa wa Nangarhar, mashariki mwa Aghanistan. Tarehe 10 mamia ya wanafunzi wa chuo kikuu mjini Nangarhar walifanya maandamano wakitoa mwito wa kuipinga marekani kuanzia chuo kikuu chao hadi kufika kwenye barabara kuu ya kuelekea mji mkuu Kabul. Raia wa huko pia walishiriki kwenye maadamano hayo. Waandamanaji waliitaka Marekani ikiri kosa la kuikashifu Kurani, na kulitaka jeshi la Marekani liondoke kabisa kutoka Afghanistan. Tarehe 11, maandamano mjini humo yalipamba moto. Maelfu ya raia waliandamana barabarani wakitoa mwito wa "iangamie Marekani". Maandamano hayo yalisababisha mgogoro barabarani, watu walivitupia mawe vioo vya magari na maduka na gari moja la jeshi la Marekani. Majengo ya serikali ya Jalalabad, ubalozi mdogo wa Pakistan na ofisi mbili za Umoja wa Mataifa mjini humo pia zilishambuliwa. Serikali ya huko iliwatuma polisi kuzuia mgogoro huo, na jeshi la Marekani lilipeleka helikopta huko. Katika mgogoro huo watu wanne waliuawa na wengine 71 kujeruhiwa. Tarehe 12, ili kuwazuia watu kutoka sehemu nyingine wasiende Jalalabada kujiunga na maandamano, mgogoro ulitokea tena kati ya waandamanaji na polisi, na kusababisha vifo vya watu watatu na watano kujeruhiwa. Siku hiyo, maandamano pia yalizuka katika mikoa mingine 10 ikiwemo Parwan, Kandahar na Khost.
Baada ya mgogoro huo, Rais Hamid Karzai wa Afghanistan ambaye yuko ziarani katika nchi za nje alisema kuwa, mgogoro uliotokea mjini Jalalabad si kitendo cha kuipinga Marekani, bali ni kuwa wakazi wa huko wanapinga kitendo cha Marekani cha kuikashifu Kurani.
Lakini wachambuzi wanaona kuwa, mgogoro huo na maandamano makubwa yaliyozuka katika sehemu mbalimbali nchini Afghanistan ni matokeo ya hasira ya Waafghanistan katika siku zilizopita. Vimeonesha kuwa Waafghanistan wanapinga ushirikiano wa kijeshi kati ya serikali ya Afghanistan na Marekani. Ripoti zinasema kuwa, jeshi la marekani litajenga kituo cha kijeshi cha kudumu nchini Afghanistan. Jambo hilo linapingwa na Waafghanistan wengi. Na hatua zilizochukuliwa na jeshi la Marekani linapowasaka wanachama wa makundi ya Al-Qaeda na Taliban zilisababisha vifo vya raia wengi wa Afghanistan, jambo hilo pia linasababisha hasira ya Waafghanistan wengi.
Idhaa ya Kiswahili 2005-05-13
|