Katibu wa Kamati ya Usalama ya Iran ambaye pia ni mjumbe wa kwanza wa mazungumzo Bw. Hassan Rowhan tarehe 12 kwenye kituo cha televisheni alisisitiza kuwa hivi karibuni Iran hakika itaanza tena shughuli za kusafisha uranium, na wakati huo huo Umoja wa Ulaya unaonya kuwa shughuli hizo ziteleta matokeo mabaya na kusababisha mazungumzo ya pande mbili kuhusu suala la nyuklia la Iran kuvunjika kabisa. Na kwamba kama hivyo ndivyo, Umoja wa Ulaya utaiunga mkono Marekani kuwasilisha suala la nyuklia la Iran kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Kutokana na pande zote mbili kushikilia msimamo wake, hali imebadilika kuwa ya wasiwasi zaidi. Vyombo vya habari vinaona kuwa suala la nyuklia la Iran huenda likawa hatarini.
Hivi karibuni Iran mara nyingi ilidokeza kuwa itaanza tena shughuli za kusafisha uranium katika kituo kilichopo Ispahan. Hivi sasa mjumbe mwandamizi wa mazungumzo wa Iran Bw. Sirous Nasseri tayari amefika Vienna kutoa taarifa rasmi kwa Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki kuhusu kuanzisha tena shughuli za kusafisha uranium.
Mwanadiplomasia wa Umoja wa Ulaya mjini Vienna alidokeza kuwa, nchi tatu zinazowakilisha Umoja wa Ulaya, Ufaransa, Ujerumani na Uingereza, ziliwasilisha barua kwa Iran na kuionya kuwa endapo tu Iran itaanzisha shughuli za kusafisha uranium Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki litafanya mkutano mara moja na kujadili kuwasilisha suala la nyuklia la Iran kwenye Baraza la Usalama. Kama Iran itakuwa mkaidi na kuanza tena shughuli za kusafisha uranium, basi "hali itakuwa mbaya kabisa". Kwenye barua hiyo nchi hizo zilitoa pendekezo la kufanya mazungumzo mengine katika siku za karibuni.
Tokea mwishoni mwa mwaka jana hadi tarehe 29 mwezi Aprili, nchi za Uingereza, Ufaransa na Ujerumani zimefanya mazungumzo na Iran mara nyingi, lakini mazungumzo yote hayakuwa na matokeo mazuri. Nchi hizo tatu zinataka Iran iache kabisa shughuli za kusafisha uranium na kama ni fidia ya kuacha shughuli hizo nchi hizo ziliahidi kuisaidia Iran teknolojia husika za maji mepesi na nyuklia kwa ajili ya kuzalisha umeme na kustawisha ushirikiano na Iran katika nyanja za uchumi na teknolojia.
Lakini Iran inapinga "biashara" hiyo tokea mwanzo. Inaona kuwa haki yake ya kuendeleza nishati ya nyuklia lazima iipate ikiwa ni pamoja na teknolojia yote na kujenga kituo chake cha kupata maji mepesi kwa kujitegemea. Kwani inaona kuwa hii ni haki yake iliyopo kwenye mkataba wa kimataifa, na nchi wanachama wengi wa Umoja wa Ulaya wanaelewa msimamo huo wa Iran.
Ili kukwamua mazungumzo yliyokwama, mwishoni mwa mwezi Machi Iran ilitoa "mpango wa majaribio", ikisema kuwa ama Umoja wa Ulaya uukubali ama Iran ijitoe kwenye mazungumzo. Si muda mrefu uliopita Iran ilitoa mapendekezo manne kwa Umoja wa Ulaya. Kama inavyojulikana kwa wote kwamba mnamo mwezi Desemba mwaka 2003 Iran ilitia saini waraka wa nyongeza wa "mkataba wa kutoeneza silaha za nyuklia", lakini waraka huo mpaka sasa haujapata idhini. Moja katika mashauri manne yaliyotolewa na Iran ni kuomba bunge lake lipitishe waraka huo. Na kwamba katika mashauriano Iran iliahidi kuwa baada ya kuanza tena shughuli za kusafisha uranium, Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki linaweza kuchunguza shughuli zote na kukagua siku zote na wakati wote.
Hivi sasa misimamo ya Umoja wa Ulaya na Iran ni wazi kabisa, na kila upande unaelewa nini upande mwingine unachotaka. Magazeti ya Ulaya yanaona kuwa kwa sasa ni vigumu kugundua kitu kinachokubalika kwa pande zote. Ingawa hivi sasa bado ni mapema kidogo kusema kuwa mazungumzo hayawezi kuendelea lakini ni hakika kwamba kama mazungumzo yakivunjika na suala la nyuklia la Iran kupelekwa kwenye Baraza la Usalama, basi pande zote mbili hazitaambulia chochote.
Idhaa ya kiswahili 2005-05-13
|