Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-05-16 15:20:06    
Iran haitaacha nia yake ya kutumia nyuklia kwa matumizi ya amani

cri

Hivi karibuni suala la nyuklia la Iran limepata maendeleo kidogo. Ofisa wa Iran alidokeza kuwa mazungumzo kati ya Iran na nchi tatu za Ufaransa, Ujerumani na Uingereza zinazowakilisha Umoja wa Ulaya yamekaribia kufikia makubaliano. Kisha bunge la Iran lilipitisha sheria ya kuihimiza serikali iendelee na shughuli za kuendeleza teknolojia ya nyuklia. Tokea tarehe 30 Aprili serikali ya Iran mara nyingi ilieleza kuwa itarudisha shughuli za nyuklia. Vyombo vya habari vya Ulaya vinaona kuwa Iran imekuwa na nia imara ya kulinda haki yake ya nyuklia kwa ajili ya matumizi ya amani, hata suala hilo likipelekwa kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Habari kuhusu mazungumzo kati ya Iran na Umoja wa Ulaya kumekaribia kufikia makubaliano ilidokezewa na mjumbe mwandamizi wa mazungumzo wa Iran Bw. Nasseri tarehe 14. Kabla ya hapo Bw. Nasseri alikuwa ameshafanya mazungumzo mengi huko Vienna na maofisa wa Umoja wa Ulaya kuhusu suala la nyuklia. Baada ya mazungumzo alisema kuwa kikwanzo kwa Umoja wa Ulaya kukubali Iran irudishe shughuli za nyuklia kinatokana na shinikizo la Marekani. Tarehe 15, katika hali ya kelele ya "iamgamie Marekani!" bunge la Iran lilipitisha azimio la kuitaka serikali iendelee na shughuli za kuendeleza nishati ya nyuklia kwa msingi wa "mkataba wa kutoeneza silaha za nyuklia". Na katika siku hiyo msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Iran Bw. Assefi alitangaza kuwa kwa kufuata matakwa ya katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bw. Kofi Annan na nchi nyingi, Iran imekubali kufanya tena mazungumzo ya viongozi waandamizi ili kuupatia Umoja wa Ulaya fursa nyingine ya mazungumzo. Alisisitiza kuwa Iran haiogopi kama suala lake la nyuklia litapelekwa kwenye Baraza za Usalama la Umoja wa Mataifa.

Kwa ajili ya duru hilo jipya la mazungumzo, Iran imeamua kuahirisha utekelezaji wa mpango wake wa kuendeleza nyuklia kwa siku kati ya wiki moja hadi siku kumi ili kupunguza hali ya wasiwasi iliyotokea katika siku za karibuni. Vyombo vya habari vinaona kuwa msimamo mgumu wa Iran sio ujanja wa mazungumzo bali umeonesha kuwa Iran kweli inataka kurudisha shughuli za nyuklia.

Wachambuzi wanaona kuwa msimamo mgumu wa Iran unatokana na sababu mbili:

Kwanza, kuendeleza teknolojia ya nyuklia kunalingana na maslahi ya taifa ya hivi sasa na ya mbali, kwa jili ya watu wa Iran wasidhibitiwe na wengine Iran lazima idhibiti teknolojia yote ya kupata nishati ya nyuklia.

Pili, msimamo wa Iran unatokana na haki iliyotolewa katika "Mkataba wa Kutoeneza Silaya za Nyuklia", kwa hiyo msimamo wa Iran kuhusu kuendeleza nishati ya nyuklia kwa jili ya matumizi ya amani ni wa haki, na unaungwa mkono na nchi nyingi ikiwemo Russia.

Isitoshe, Iran ikiwa nchi kubwa inayozalisha mafuta ina uzito wake wa kisiasa. Iran ni nchi ya pili ya inayozalisha mafuta kwa wingi baada ya Saudi Arabia, na sasa bei ya mafuta ni kubwa, hata nchi za Magharibi zikitaka kuushawishi Umoja wa Mataifa uiwekee Iran vikwazo vya uchumi lazima utafakari uzito wa Iran katika uzalishaji mafuta, achilia mbali kuwa nchi za Ulaya ni nchi zinazohitaji sana mafuta. Kama Iran inavyosema kuwa suala la nyuklia la Iran ikiwasilishwa kwenye Baraza la Usalama waathirika wakubwa ni nchi za Ulaya tu.

Vyombo vya habari vinaona kuwa kutokana na sababu hizo, Iran itashikilia msimamo wake wa kunufaisha taifa na haitashawishika, na hata ilitangaza wazi kuwa haitaogopa kushambuliwa na Marekani. Habari nyingine zinasema kuwa, baadhi ya maofisa wa Ufaransa wanapendelea kukubali Iran iendelee na shughuli zake chini ya uangalizi wa Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki, lakini msimamo huo unapingwa na Uingereza. Kwa hiyo mazungumzo yatakayoanza hivi karibuni yatavutia zaidi.

Idhaa ya kiswahili 2005-05-16