Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-05-16 15:23:48    
Upigaji kura wa uchaguzi mkuu nchini Ethiopia wamalizika

cri

Upigaji kura wa uchaguzi wa baraza la wajumbe wa umma la bunge la shirikisho la Ethiopia na mabunge ya mikoa minane ulimalizika tarehe 15. Huu ni uchaguzi wa tatu wa kidemokrasia wa vyama vingi katika historia ya Ethiopia. Wapiga kura walimiminika kwenye vituo vya upigaji kura kwa uchangamfu.

Idadi ya wapiga kura walioshiriki kwenye uchaguzi huo ilifikia milioni 25.6 ambayo ni kubwa kabisa katika wapiga kura walioorodheshwa nchini humo. Habari zilisema kuwa vyama 36 vilishiriki kwenye uchaguzi huo na vyama vitatu vyenye ushindani mkubwa ni chama cha demokrasia ya mapinduzi ya umma, chama cha nguvu ya demokrasia na chama cha umoja na demokrasia. Kati yao, chama cha demokrasia ya mapinduzi ya umma ni chama tawala na chama kikubwa kabisa nchini humo.

Wananchi wa Ethiopia walifuatilia sana uchaguzi huo. Upigaji kura ulianza saa kumi na mbili asubuhi, na wapiga kura wengi walifika kwenye vituo vya upigaji kura mapema kabla ya kufunguliwa kwa vituo hivyo. Kijana mmoja alihojiwa na mwandishi wa habari akisema nimesimama kwenye safu ya kupiga kura kwa muda wa saa saba, lakini nitaweza kupiga kura baada ya muda wa saa mbili, hata hivyo nitasubiri hadi mwisho.

Kutokana na takwimu, asilimia 85 ya wapiga kura walishiriki kwenye upiga kura wa siku hiyo. Kutokana na kuwa idadi ya wapiga kura ilizidi ile iliyokadiriwa, ofisa wa tume ya uchaguzi wa taifa ya Ethiopia alitangaza usiku huo kuwa muda wa upiga kura utarefushwa kwa muda wa saa tatu hadi saa nne, ili wapiga kura wote watumie haki zao.

Ni kinyume cha uchangamfu wa wapiga kura, vyama vya upinzani vya kugombea uchaguzi huo vililalamikia upigaji kura wa siku hiyo. Kiongozi wa chama cha umoja na demokrasia cha Ethiopia Bw. Hailu Shawel alieleza kabla ya kumalizika kwa upigaji kura kuwa msongamano na furugu katika vituo vya upigaji kura hauwezi kuhakikisha uhuru na haki ya uchaguzi huo. Kwa hiyo alitaka chama chake kipinge matokeo ya uchaguzi huo.

Kuhusu jambo hilo, mwenyekiti wa tume ya uchaguzi wa taifa ya Ethiopia Bw. Kemal Bedri alisema kuwa usemi huo sio wa kuwajibika kwa wapiga kura waliosimama kwenye safu ya kupiga kura kwa saa kumi hadi saa kumi na mbili. Baadhi ya maofisa wa serikali walishutumu kuwa vitendo hivyo vya vyama vya upinzani vilitafuta kisingizio cha kususia uchaguzi huo. Wachunguzi wa kimataifa pia walikosoa msimamo huo wa Hailu Shawel. Mkaguzi wa uchaguzi huo wa Umoja wa Ulaya Bi. Ana Gomes alisema kuwa tunashindwa kuelewa kwa kutoa mashaka sasa hivi kwa uchaguzi huo uliofanikiwa kufanyika. Alisema kuwa ingawa kulitokea hali ya msongamano katika baadhi ya vituo vya upigaji kura, lakini kwa jumla, mchakato wa upigaji kura uliendelea katika hali tulivu. Habari zilisema kuwa ili kuongeza uhalali wa uchaguzi huo, serikali ya Ethiopia iliwaalika wachunguzi wa kimataifa wapatao zaidi ya 300.

Kutokana na ratiba ya tume ya uchaguzi, matokeo ya mwisho ya uchaguzi huo yatatolewa tarehe 8 mwezi Juni. Bila kujali matokeo ya uchaguzi huo yatakuwa namna gani, kujitokeza kwa raia wa Ethiopia kwenye mchakato wa demokrasia kumewawezesha watu duniani watambue nia yao ya kushiriki siasa za taifa lao.

Idhaa ya kiswahili 2005-05-16