Hivi karibuni waziri wa ulinzi wa Marekani Bw.Donald Rumsfeld alitangaza kufikiria kufunga na kuwahamisha wanajeshi walioko katika vituo vya kijeshi nchini Marekani. Maneno yake hayo yalisababisha mara moja majadiliano makali. Kutokana na kuwa vituo vya kijeshi vinamaanisha nafasi za kazi kwa wakazi wa huko, hivyo wabunge wa taifa "wanaowakilisha maslahi ya sehemu waliko" waliulalamikia sana mpango wa Bw. Rumsfeld.
Tarehe 13, waziri wa ulinzi wa Marekani Bw. Rumsfeld alitoa "Orodha ya majina ya mageuzi" kwa tume ya kurekebisha na kufunga vituo vya kijeshi. Kutokana na orodha hiyo, vituo vya kijeshi 150 nchini vitafungwa na vingine 29 vitarekebishwa. Hii ni mara ya kwanza kwa Marekani kupunguza kwa wingi idadi ya vituo vya kijeshi toka zaidi ya miaka 10 iliyopita.
Bw. Rumsfeld ana lengo lake kuhusu hatua hizo anazochukua. Katika taarifa moja alisema kuwa nia ya jeshi la Marekani kujenga vituo vingi vya kijeshi hapo awali ilitokana na kukabiliana na vita baridi. Lakini hali ya hivi sasa imekuwa na mabadiliko makubwa. Alisema kuwa kufunga 5% hadi 11% ya vituo vya kijeshi ambavyo havina kazi kwa hivi sasa, wataweza kuokoa dola za kimarekani bilioni 48.8 katika miaka 20 ijayo.
Wachambuzi wanaona kuwa wizara ya ulinzi ya Marekani inatarajia kufunga vituo visivyo na ufanisi mwingi na kuhamisha fedha zinazookolewa katika vituo vikubwa muhimu ili kuleta ufanisi mkubwa zaidi. Aidha, wizara ya ulinzi ya Marekani inatarajia jeshi la ardhini, jeshi la angani na jeshi la baharini yatumie baadhi ya vituo kwa pamoja ili kupunguza matumizi ya fedha na kuimarisha ushirikiano wao.
Lakini mpango huo wa kupunguza idadi ya vituo vya kijeshi umepingwa vikali na baadhi ya wabunge wa Marekani. Vituo vya kijeshi husifiwa kuwa ni "injini ya uchumi" nchini Marekani, hususan katika sehemu ya kaskazini mashariki ya nchi hiyo, hivyo kufunga vituo vya kijeshi kutapoteza baadhi ya ajira. Inakadiriwa kuwa mpango huo wa Bw. Rumsfeld utafanya watu karibu elfu 30 wapoteze nafasi za kazi.
Mbunge wa Jimbo la Maine kutoka chama cha Republican Bw. Olympia Snow siku hiyo aliukosoa mpango huo na kuuita kuwa ni "wenye uangamizaji" na ni "makosa ya kisiasa ya wizara ya ulinzi". Habari zinasema kuwa kiwanda cha manowari kilichojengwa miaka 200 iliyopita kitafungwa na kufanya watu zaidi ya 4,500 wapoteze nafasi za ajira, hali ambayo itaathiri maisha ya wakazi wa huko.
Lakini mpango huo wa upunguzaji wa vituo vya kijeshi utaleta ajira kwa baadhi ya majimbo mingine. Kwa mfano, upanuzi wa ujenzi wa vituo vya kijeshi katika majimbo ya Maryland na Virginia utaongeza ajira karibu elfu 10.
Ukweli ni kuwa wakati wizara ya ulinzi ya Marekani ilipobuni mpango huo ilifikiria matokeo ya aina mbalimbali. Bw. Rumsfeld alisema kuwa walipotathimini thamani ya kijeshi ya kituo fulani, walifikiria pia athari itakayoletwa kuhusu uchumi wa huko, matumizi ya fedha katika siku za baadaye na gharama itakayoweza kupunguzwa. Alisisitiza kuwa idadi ya vituo vya kijeshi vinavyofungwa ni ndogo sana ikilinganishwa mapendekezo waliyotoa.
Habari zinasema kuwa endapo mpango huo utapitishwa, utekelezaji wake utakamilika kwa muda wa miaka 6 kutoka mwaka 2006. Hatua halisi zinazochukuliwa ni kama ifuatavyo: Kwanza "Tume ya Kurekebisha na Kufunga vituo" itatathmini mpango huo, na kutoa mapendekezo yake kwa rais mwezi Septemba, baada ya kuidhinishwa na rais, utawasilishwa kwenye bunge la taifa, ambalo litaweza kuyakubali au kuyakataa, lakini haliwezi kuyafanyia marekebisho. Inakisiwa kuwa kutakuwa na malumbano makali ya kisiasa kabla ya bunge kufanya uamuzi.
Idhaa ya Kiswahili
|