Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-05-16 21:41:34    
Klabu za aina nyingi za utamaduni katika vyuo vikuu mjini Beijing

cri

Mjini Beijing kuna vyuo vikuu zaidi ya 70 na wanafunzi wako zaidi ya laki tano. Nje ya masomo wanafunzi hao hushiriki katika klabu za aina nyingi za utamaduni.

Wasikilizaji wapendwa, mliyosikia ni sauti ya mchezo wa dansi ya barabarani katika maonesho ya michezo ya sanaa katika Chuo Kikuu cha Utangazaji, mchezaji anatoka klabu ya dansi ya DE. Dansi yake ilichezwa kwa uhodari kwa kuambatana na midundo ya muziki wa HIP-HOP na ilishangiliwa sana na watazamaji.

Klabu ya Dansi ya DE ni klabu ya kueneza dansi ya barabarani katika chuo kikuu hicho, ilianzishwa mwaka 2003, na kuna watu 30 katika klabu hiyo ambao wanatoka idara mbalimbali, na wote wana msingi wa kucheza dansi na wanapenda utamaduni wa HIP-HOP. Mkuu wa klabu hiyo Bw. Xia Rui alisema,

"Kwa sababu napenda utamaduni wa HIP-HOP na napenda kucheza daansi, kwa hiyo nilianzisha klabu hiyo ili niwapatie wapenda dansi nafasi ya kupeana maarifa na kucheza pamoja. Kutokana na kuwa HIP-HOP ni utamaduni wa kisasa, wanaopenda utamaduni huo ni wengi."

Klabu hiyo kila alasiri Jumamosi ina shughuli yake, baadhi ya wakati wanafanya mazoezi ya dansi, na baadhi wanawakaribisha wachezaji wa vyuo vikuu vingine kujadiliana stadi. Klabu hiyo mara nyingi inashiriki katika mashindano ya aina mbalimbali ya dansi yaliyoandaliwa na kituo cha televisheni na inapata tuzo nyingi katika mashindano kama hayo.

Mwanafunzi anayetoka Japan, Miyaxita Takunoli, ni mmoja wa wacheza dansi katika klabu hiyo. Alijiunga na chuo kikuu hicho miaka miwili iliyopita katika somo la utangazaji wa redio, anasoma na kuishi pamoja na wanafunzi wa China. Kuhusu kucheza dansi na maisha yake ya miaka miwili iliyopita alisema,

"Jambo muhimu ni kuwa nimepata marafiki. Mimi ni Mjapan, lakini wanafunzi wa China wananitendea kama ni mwenzao, nilipohisi upweke nacheza au kutalii pamoja nao, na nikiwa na shida wananisaidia."

Klabu ya picha za katuni ni klabu nyingine ya wanafunzi katika chuo kikuu hicho. Klabu hiyo ina wanafunzi 40, mara kwa mara wanafanya maonesho ya picha zao zikionesha maisha ya wanafunzi wenzao na hali nzuri na mbaya inayotokea katika jamii. Mkuu wa klabu hiyo, Xu Xiaoqing, alisema,

"Mwaka 2003 tulifanya maonesho ya picha za katuni kwa mada ya kuimarisha China. Mwaka 2004 tulifanya maonesho kwa mada ya kuhifadhi mazingira safi, na baadaye tulifanya maonesho ya picha za katuni za wanafunzi wa vyuo vikuu wa China na Japan."

Wasikilizaji wapendwa, mliyoisikia ni sauti ya kusoma mashairi katika tamasha la mashairi katika chuo Kikuu cha Beijing. Klabu ya mashairi katika Chuo Kikuu cha Beijing ilianzishwa mwaka 1956 ili kushughulikia utungaji wa mashairi na riwaya. Klabu hiyo iliwahi kuandaa washairi wengi mashuhuri. Kuanzia mwaka 2000, kila mwaka klabu hiyo inafanya "mwezi wa mashairi". Katika mwezi huo klabu hiyo hufanya mihadhara, tamasha na mashindano ya mashairi, na shughuli hizo zinawakutanisha marafiki. Mkuu wa klabu hiyo, Huang Qian, alisema,

"Mashairi ya siku hizi licha ya kuwa na tofauti na mashairi ya kale kwa kina, muhimu yanaeleza fikra na hisia za vijana wa sasa, na waandishi wa chuo kikuu chetu wanaandika zaidi maisha ya wanafunzi wenzetu, na mashairi huandikwa kwa uhuru zaidi bila kanuni kali."

Bendi ya Chuo Kikuu cha Sayansi na Uhandisi cha China ni bendi iliyoanzishwa mwaka 2000 na inayojulikana katika vyuo vikuu mjini Bejing. Licha ya kuwa bendi hiyo inashiriki katika sherehe mbalimbali za vyuo vikuu, pia inapiga muziki wake vijijini na katika kambi za jeshi.

Wasikilizaji wapendwa, mliousikia ni muziki uliopigwa na bendi hiyo wa "Polka" uliotungwa na Johann Strauss, unaonesha vilivyo jinsi wanawake walivyojawa na nderemo.

Katika muda wa miaka mitano iliyopita bendi hiyo ilifanikiwa kupiga muziki wa Webber wa karne ya 19 hadi muziki wa Shostakovich wa karne ya 20, tokea muziki wa Blauen Donau wa Johann Starauss mpaka muziki wa Huanghe wa Xian Xinghai. Kwa kupiga muziki huo uhodari wa bendi hiyo umeinuka sana.

Bw. Zhu Dong ni mwanafunzi wa somo la injini ya gari, alianza kujifunza kupiga fidla alipokuwa na umri wa miaka minane, sasa ni mkuu wa bendi hiyo. Katika miaka miwili tokea alipoanza kushiriki katika bendi hiyo amepata elimu nyingi, alisema,

"Elimu yangu kuhusu muziki nimeielewa kwa kina zaidi, kwa sababu kabla ya kupiga muziki lazima nielewe mazingira ya muziki huo ulipotungwa, pili nimefahamiana marafiki wengi, na kutokana na majadiliano yetu kuhusu muziki fulani nimepata mambo mengi nisiyoyajua."

Kila mwaka bendi hiyo inafanya maonesho ya muziki katika sikukuu ya mwaka mpya na kufanya maonesho ya muziki mara mbili "muziki wa chumbani". Kuingiza muziki kama huo wa hali ya juu katika maisha ya wanafunzi ili kuwafanya wanafunzi wauelewe muziki wa kale, ni jambo la maana sana.

Idhaa ya Kiswahili 2005-05-16