Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-05-17 15:47:44    
Barua 0517

cri
Msikilizaji wetu Mussa Balele ambaye barua zake huhifadhiwa na Stephen Kumalija wa sanduku la posta 1421 Mwanza Tanzania ametuletea barua akisema kuwa, yeye ni mzima wa afya njema na anaendelea kuitegea sikio Radio China kimataifa anayoipenda ambayo inawaletea matangazo kabambe kutoka Beijing, China.

Anasema anapenda kutumia fursa hii ili kuwapongeza wafanyakazi wote wa Radio China kimataifa kwa kumuunga mkono au kwa kumkaribisha kwa mikono miwili, kuwa msikilizaji wa Radio China kimataifa. Alifurahi sana mara tu baada ya kupata barua kutoka kwetu ikihusu kuwa amekubaliwa kuwa mwanachama wa Radio China kimataifa.

Vilevile anapenda kuwashukuru wafanyakazi wote wa Radio China kimataifa kwa kumtumia bahasha iliyokwishalipiwa stempu, kalenda ya mwaka huu wa 2005, kadi za salamu pamoja na picha ya alama ya kuku ambayo inawakilisha mwaka huu katika kalenda ya kichina. Na anatushukuru kwa kumfahamisha kwamba mwaka huu tutachapisha jarida dogo la daraja la urafiki, ambalo hilo linahusu urafiki kati ya Radio China kimataifa na wasikilizaji wake wote walioko sehemu zote duniani kote.

Jarida hilo dogo ndani yake wasikilizaji wa Radio China kimataifa watakuwa wakitoa michango yao mbalimbali ambayo itakuwa inahusu maoni, barua, makala, mashairi mafupi, hadithi hata mapendekezo yao mbalimbali na kadhalika. Anautakia urafiki kati yake na Radio China kimataifa uendelee miaka hadi milele.

Leo tunapenda kuwaarifu wasikilizaji wetu kuwa, jarida letu hilo tayari limechapishwa, na hivi sasa tunaendelea na pilikapilika za kuwatumia jarida hilo wasikilizaji wetu waliotuletea barua, ni matumaini yetu kuwa wasikilizaji wetu wakipokea jarida hilo, watatoa maoni na mapendekezo yao ya kutusaidia kuboresha jarida hilo. Wasikilizaji wetu wengi wamefurahishwa na kuchapishwa kwa jarida hilo na sasa wanalisubiri kwa hamu, na wengi kati yao wametoa mashauri mbalimbali kuhusu jarida hilo, mashauri hayo tunaweza kuyazingatia kwa makini katika kazi yetu.

Msikilizaji wetu Kaziro Dutwa wa sanduku la posta 209 Songea Ruvuma Tanzania ametuletea barua akisema kuwa amefurahi kupata fursa hii ili aweze kutuandikia barua kwa mara nyingine huku akiweka matumaini kuwa sote hatujambo tukiendelea kuchapa kazi kwa juhudi kubwa, pia anatuarifu kuwa hali yake ni nzuri Kabisa.

Tunamshukuru kwa salamu zake, sisi sote hapa hatujambo kama alivyosema tunachapa kazi kwa juhudi kubwa, kwani tokea mwishoni mwa mwaka 2003, mbali na kuandaa vipindi mbalimbali vya matangazo ya kila siku, pia tunaweka makala na vipindi mbalimbali kwenye tovuti.

Bwana Dutwa anasema kuwa, hivi karibuni amewasikia wasikilizaji wengi wakilalamika kuwa muda wa vipindi hautoshi, hakika walilalamika kwa uchungu mkubwa sana. Hata hivyo, japo malalamiko ambayo yamekuwa yakitolewa na wasikilizaji wengi huwa yanajibiwa na wahusika hasa dada Chen amekuwa akiyajibu kwa kinaganaga kabisa, na kueleza wazi kuwa tatizo ni muda ulilopangwa na ngazi za juu; hivyo vipindi hufuata muda uliowekwa bila kuongeza wala kupunguza.

Anasema wasikilizaji wamekuwa wakitolea mfano wa kipindi cha salamu zenu kuwa hakiridhishi kutokana na kusomwa kwa kadi chache,

na kadi nyingine hubaki zikisubiri muda. Bwana Dutwa anasema anavyoona yeye, si lengo la watangazaji kuziweka tu hizo kadi na kuzisoma wenyewe wakiwa wamekufa, kama alivyolalamika msikilizaji mmoja. Sababu ni ileile; muda hautoshi na ukishindana na muda utaumia mwenyewe. Pia msikilizaji mmoja aliulalamikia usomaji wa kadi, yaani kurudiwa kwa takriban siku tatu mfululizo, na kusema kuwa utaratibu huo haufai. Yeye Bwana Dutwa anasema kila mtu ana mtizamo wake kuhusu mambo tofauti, bila shaka utaratibu huo unawavutia baadhi ya watu na hauwavutii baadhi.

Idhaa ya kiswahili 2005-05-17