Chama cha Ndugu wa Kiislamu, Ikhwan, pamoja na vyama vingine vitatu nchini Misri tarehe 17 vilitangaza kupinga upigaji kura za maoni dhidi ya marekebisho ya kifungu cha 76 cha katiba. Hii inaonesha kuwa mgongano kati ya vyama vya upinzani na serikali umekuwa mkali.
Kwenye mkutano na waandishi wa habari uliofanyika katika makao makuu ya Chama cha New Wafd, vyama vikubwa vitatu vya upinzani vya New Wafd, Umoja wa Maendeleo ya Kitaifa na Chama cha Demokrasia ya Waarabu cha Nasser vilitangaza kuwa ingawa kifungu cha 76 kinachorekebishwa kinaruhusu watu wengi zaidi kushiriki katika uchaguzi mkuu, kifungu hicho kimeviwekea kikwazo kisichoweza kuvukwa vyama visivyo tawala, hakikutoa nafasi sawa na chama tawala, kwa hivyo vyama hivyo vitatu vimeamua kususia upigaji kura utakaofanyika tarehe 25, na kuahirisha bila tarehe maalumu kuteua wagombea wao wa urais na vinataka watu wa Misri wasijitokeze kupiga kura. Isitoshe, vyama hivyo vitatu vinaona kuwa kutokana na Chama tawala cha Demokrasia ya Taifa kupuuza mapendekezo ya vyama vya upinzani, mazungumzo ya pande mbili hayatakuwa na maana, kwa hiyo vimejitoa kutoka kwenye mazungumzo hayo.
Mwaka huu Misri itafanya uchaguzi mkuu wa kila baada ya miaka 6, uchaguzi huo umesababisha hali ya wasiwasi nchini humo. Tokea mwezi Desemba vyama vya upinzani mara nyingi vilifanya maandamao ya kupinga rais Mubarak kuendelea na wadhifa wake. Katika siku za karibuni Chama cha Ikhwan na vyama vingine vya upinzani viliisumbua serikali katika masuala ya uchaguzi mkuu na mageuzi ya siasa. Ili kutuliza hali ya wasiwasi serikali ya Misri ilichukua hatua nyingi na iliwakamata waandamanaji mia kadhaa.
Wachambuzi wanaona kuwa chanzo cha vyama vya upinzani kufanya matata kinatokana na sababu nyingi. Kwanza, baada ya tukio la "Septemba 11" nchi za Kiarabu na dunia ya Waislamu zimekuwa shabaha ya kupigwa na Marekani, na nchi hizo zimesukumwa pembeni katika mambo ya siasa ya kimataifa, hali yao imekuwa mbaya. Ili kueneza "mpango wa kueneza demokrasia katika eneo la Mashariki ya Kati" Rais Bush wa Marekani alishinikiza nchi hizo ikiwemo Misri, nchi ambayo ni mshirika wake, kufanya mageuzi. Msimamo huo wa Marekani ni kama sindano ya kuchangamsha vyama vya upinzani vya Misri na nchi za Mashariki ya Kati. Vitendo vya vyama vya upinzani nchini Misri kwa kweli ni jibu la vyama hivyo kwa "mpango wa kueneza dimokrasia" wa Bush. Pili, uchumi wa Misri unakwenda taratibu, bei za bidhaa zinapanda, watu wanaokosa ajira ni wengi na madeni ya serikali ni lukuki humu nchini na nchi za nje, maisha ya wananchi yanashuka. Malalamiko ya wananchi kuhusu maisha yao ni sababu nyingine ya vyama vya upinzani kufanya fujo.
Wachambuzi wanaona kuwa ingawa vyama vya upinzani vinashughulika sana kuipinga serikali lakini havijawa vitisho kwa serikali. Kwanza, ingawa Marekani inajitahidi kadiri iwezavyo kutekeleza mpango wake wa kueneza demokrasia katika Mashariki ya Kati, haitaki vyama vya upinzani nchini Misri viongeze nguvu hadi kuidhibiti hali ya Misri ili visiathiri utekelezaji wa "mpango" wake. Pili, vyama hivyo ni dhaifu na haviungwi mkono sana na wananchi, na miongozo ya kisiasa ya vyama hivyo haipokelewi sana na wananchi. Tatu, Chama tawala cha Demokrasi ya Taifa kina viti vingi katika bunge na rais Mubarak ana uwezo wa kudhibiti hali ya siasa.
Kwa hiyo, endapo serikali ya Misri ikirekebisha hatua za mchakato wa demokrasia na kuongeza nguvu katika mageuzi ya uchumi, mvutano wa kisiasa nchini Misri unaweza kupungua. Kutokana na heshina na hadhi ya Mubarak nchini Misri na nchi za nje, kama akitangaza kuwa mgombea urais hakika atashinda na kuwa rais wa kipindi kingine mfululizo.
Idhaa ya kiswahili 2005-05-18
|