Katika hali ambayo pande mbalimbali zina maoni tofauti kabisa, "Umoja wa Nchi Nne" unaoundwa na Japan, Ujerumani, Brazil na India tarehe 16 ulifanya harakati ya kusambaza kwa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa mswada wa azimio la mageuzi ya baraza la usalama.
Kutokana na mswada huo wa azimio, upanuzi wa baraza la usalama utafanyika kwa hatua tatu, ya kwanza ni kupitisha azimio la programu, pili ni kuchagua nchi wajumbe wa kudumu la baraza jipya la usalama na tatu ni kupitisha azimio kuhusu marekebisho ya katiba. Mswada wa azimio unataka kuongeza viti 6 vya wajumbe wa kudumu, viti vinne vya wajumbe wasio wa kudumu wa miaka 2. Mswada huo wa azimio pia umependekeza Baraza kuu la Umoja wa Mataifa kujadili na kupitisha mswada huo wa azimio mwezi Juni, kuchagua nchi wajumbe wa kudumu wa baraza jipya la usalama katikati ya mwezi Julai na kupitisha azimio la marekebisho ya katiba katika wiki mbili zinazofuata.
Kutokana na kukabiliwa na hali ya kimataifa yenye mabadiliko mengi, utaratibu wa Umoja wa Mataifa unaonekana kuwa na kasoro nyingi, na ni lazima mageuzi yafanyike. Lakini mageuzi ya Umoja wa Mataifa ni kazi moja kubwa na yenye matatizo mengi hususan mageuzi ya baraza la usalama. Hivyo Umoja wa Mataifa hususan baraza la usalama halifai kutenda vitendo haraka na kuweka kikomo cha muda kwa upigaji kura katika hali yenye maoni tofauti kabisa kuhusu mpango wa mageuzi, bali inatakiwa kutenda vitendo hatua kwa hatua, kuwa na mashauriano ya pande mbalimbali ili kufikia mwafaka.
Kwa hivi sasa bado hakuna mpango mmoja wa mageuzi ya baraza la usalama, ambao unaungwa mkono na wanachama wengi. Mwezi Machi mwaka huu Bw. Kofi Annan alitoa mipango miwli ya mageuzi ya baraza la usalama, mmoja unapendekeza kuongeza viti 3 vya wajumbe wa kudumu wasio na haki ya kupiga kura ya turufu pamoja na viti 3 vya wanachama wasio wa kudumu, mpango mwingine ni kupendekeza kuongeza viti 8 vya muda wa miaka minne vya wajumbe wa kudumu ambao wanaweza kugombea nafasi ya ujumbe wa kudumu kwa mfululizo pamoja na kiti kimoja cha muda wa miaka 2 cha mwanachama mjumbe wa kudumu. Nchi za Ujerumani, Japan, India na Brazil zinazotarajia kuwa wajumbe wa kudumu wa baraza la usalama zinajitahidi kuhimiza mpango wa kwanza, lakini zinapingwa vikali na Italia, Hispania, Korea ya Kusini, Pakistan na Mexico ambazo zinataka kuanzisha majadiliano kwa msingi wa mpango wa pili na kupinga kulazimisha kufanya upigaji kura katika muda uliowekwa.
Wachambuzi wanasema kuwa ni hali ya kawaida kuweko maoni tofauti kuhusu mageuzi ya baraza la usalama, jambo lililo muhimu ni kuwa na mazungumzo ili kutafuta maoni ya namna moja na kujitahidi kuafikiana kwenye msingi wa kuwa na maoni mengi ya namna moja. Mpango wowote wa mageuzi ambao unashindwa kupata uungaji mkono wa 90% ya idadi ya nchi wanachama, mpango huo hauwi mpango ulioafikiana kwa pamoja, ama njia ya kuupachika kwa nguvu mpango wake juu ya wanachama wengine ni mbaya zaidi.
Ni dhahiri kuwa kuweka kikomo cha muda wa mageuzi au kufanya upigaji kura kwa nguvu hakuendani na maslahi ya umoja na ya muda mrefu ya Umoja wa Mataifa. Hivi sasa nchi nyingi zaidi na zaidi zina wasiwasi kuwa huenda malumbano kuhusu mageuzi ya baraza la usalama yatafarakanisha nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa, tena yatapunguza nguvu ya kushughulikia masuala mengine, hususan mashauriano na mchakato wa utatuzi wa suala la maendeleo. Hivyo wanachama wengi wanaona kuwa haifai kuweka wakati wa kufanyika kwa mkutano wa wakuu wa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa mwezi Septemba kuwa kikomo cha muda wa mageuzi ya Umoja wa Mataifa. Kwani mkutano huo ni mwanzo tu wa mageuzi ya Umoja wa Mataifa wala siyo mwisho wa mageuzi.
Idhaa ya Kiswahili 2005-05-18
|