Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-05-18 19:00:39    
Kugundua mapema ni muhimu kwa kutibu ugonjwa wa saratani

cri

Pamoja na maendeleo ya sayansi na teknolojia na kuinuka kwa kiwango cha matibabu, magonjwa mengi makali yamekuwa yanaweza kutibika, lakini bado ni vigumu kutibu ugonjwa wa saratani. Ugonjwa huo umekuwa suala kubwa la afya ya umma duniani. Kwa mujibu wa takwimu husika, katika mwaka 2000, wagonjwa zaidi ya milioni 6.2 walikufa kutokana na ugonjwa huo.

Ugonjwa wa saratani uliogunduliwa mapema zaidi unaweza kutibiwa vizuri zaidi. kwa mujibu wa shirika la afya duniani, kama ugonjwa huo ukiweza kugunduliwa na kutibiwa mapema, theluthi moja ya saratani za aina mbalimbali zinaaweza kutibika.

Ugonjwa wa saratani ni ugonjwa wenye umaalum wa ukuaji usio wa kawaida na kuhama kwa chembechembe. Kugunduliwa na kutibiwa mapema kuna umuhimu mkubwa sana kwa matibabu ya ugonjwa huo. kwa mfano, saratani ya utumbo mkubwa ikitibiwa mapema, asilimia 90 ya wagonjwa wa ugonjwa huo wanaweza kuendelea kuishi kwa zaidi ya miaka 5; lakini matibabu yake yakichelewa, asilimia 5 hadi 7 tu wataweza kuendelea kuishi kwa miaka 5.

Daktari mkuu wa Hospitali ya ugonjwa wa saratani katika taasisi ya sayansi ya udaktari ya China Bw. Shi Yuankai alisema:

"pamoja na maendeleo ya sayansi na teknolojia na kuinuka kwa kiwango cha maisha ya wananchi, mbinu na dawa za kutibu ugonjwa wa saratani zimeendelea kuongezeka, na pia zimeleta matokea mazuri zaidi."

alisema kuwa, baadhi ya magonjwa ya saratani yatakuwa na dalili fulani mwilini katika kipindi cha awali. Ingawa dalili hizo zinafanana na magonjwa ya kawaida, lakini kama madaktari na wagonjwa wakiweza kuzingatia dalili hizo, wataweza kusaidia kugundua ugonjwa huo mapema.

China ni moja ya nchi zinazoathiriwa sana na ugonjwa wa saratani. Mwaka 2000, idadi ya watu wa China waliokufa kutokana na ugonjwa huo ilifikia milioni 1.5. Hivi sasa, asilimia 20 ya vifo vya wachina vinatokana na ugonjwa wa saratani. Hivyo, serikali ya China imezingatia sana kazi ya kukinga na kutibu ugonjwa wa saratani. Kugundua mapema kama mtu ana ugonjwa wa saratani kumekuwa mbinu muhimu ya kukinga na kutibu ugonjwa huo, na kumeenezwa nchini China.

China ilianza kufanya kazi ya kutambua mapema ugonjwa wa saratani tangu miaka ya 50 katika karne ya 20. kwa mfano, wilaya ya Ci mkoani Hebei ni sehemu yenye idadi kubwa ya wagonjwa wa saratani ya koromeo. Mwaka 1973, kituo cha kukinga na kutibu ugonjwa huo kilianzishwa huko na kutekeleza utaratibu wa jumla wa kutambua mapema ugonjwa huo, na hatua hiyo imepunguza kwa kiasi kikubwa idadi ya wagonjwa na vifo vinavyotokana ugonjwa huo. Mkuu wa hopspitali ya saratani ya mkoa wa Hebei Bw. Wang Shijie alisema:

"kutokana na juhudi kubwa za kukinga na kutibu ugonjwa wa saratani katika miaka 30 iliyopita, idadi ya wagonjwa na vifo imepungua hatua kwa hatua. Kwa mfano, idadi ya wagonjwa wanaume kilikuwa ni mia mbili katika laki moja katika mwaka 1974, na kiasi hicho kilipungua na kufikia 130 katika laki moja katika mwaka 2002."

Hivi sasa, idadi ya wachina wanaokufa kutokana na ugonjwa wa saratani imekuwa inaendelea kuongezeka. Ili kukabiliana na changamoto ya ugonjwa huo na kulinda afya ya umma, idara husika za China zimeweka mpango mpya wa kukinga na kutibu ugonjwa wa saratani. Ofisa wa idara ya kudhibiti magonjwa katika wizara ya afya ya China Bi. Kong Lingzhi alisema:

"mpango wa kukinga na kudhibiti ugonjwa wa saratani wa China uliotolewa na wizara ya afya ya China mwezi Desemba mwaka 2003, unasisitiza kugundua na kutibu mapema ugonjwa huo."

Baada ya kutolewa kwa mpango huo, idara husika za China zimefanya kazi nyingi. Kwa mfano, ziliwashirikisha wataalamu wa eneo hilo kuandaa kitabu cha mbinu sanifu za kupima, kutambua na kutibu mapema ugonjwa wa saratani.

Mbinu ya kupima na kutambua mapema saratani ya mlango wa kizazi imepevuka, hivyo China imeweka mkazo katika upimaji na matibabu ya ugonjwa huo; upimaji wa saratani ya maziwa na saratani ya utumbo mkubwa unahitaji raslimali za kutosha, hivyo China itafanya kazi ya kupima na kutambua mapema magonjwa hayo katika miji inayotimiza masharti; kuhusu upimaji mepema wa saratani ya koromeo, maini, pua na koo, ingawa hakuna mbinu nzuri zinazotumika na kukubalika kote duniani, lakini baada ya uzoefu na utafiti kwa miaka mingi, China imepata uzoefu mkubwa katika eneo hilo unaolingana na hali halisi nchini China. hivyo, China itaanzisha vituo vya kupima na kutambua mapema saratani za aina hizo kwenye maeneo yenye idadi kubwa ya watu wenye magonjwa hayo, na kukamilisha mbinu hizo hatua kwa hatua, ili kutafiti na kupata utaratibu bora.

Aidha, China pia imechagua sehemu kadhaa na kujenga vituo vya mfano vya kupima na kutambua mapema ugonjwa wa saratani. Ofisa wa idara ya kudhibiti magonjwa katika wizara ya afya ya China Bi. Kong Lingzhi alisema:

"mwaka 2004, China ilichagua sehemu tatu za vijijini katika mikoa ya Henan, Hebei na Shanxi, na eneo la makazi mjini Shenzhen, na kujenga vituo vya mfano vya kupima na kutambua mapema saratani ya mlango wa kizazi na koromeo, na katika siku za baadaye, China itaanzisha vituo vya mfano vya kupima na kutambua mapema saratani ya utumbo mkubwa, maini, pua na koo katika sehemu kadhaa zilizochaguliwa."

Kwenye vituo hivyo, idara husika za China zitafanya kazi ya upimaji wa saratani husika ili kutambua mapema wagonjwa; pia vitaeneza ufahamu kuhusu kukinga na kuzuia ugonjwa wa saratani kwa wakazi, na kuwaelekeza watu wawe na mwenendo mzuri wa maisha; aidha, vituo hivyo pia vinafanya utafiti wa kisayansi kuhusu ugonjwa wa saratani.

Idhaa ya Kiswahili 2005-05-18