Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-05-19 15:53:36    
Wasala wanaoishi mjini Beijing

cri
Wasala ni wa kabila lenye idadi ya watu wasiozidi laki moja, wengi wao wanaishi katika mkoa wa Qinghai, kaskazini magharibi mwa China. Wasala waliohamia kutoka Asia ya kati wanapenda kuhamahama, hivyo wametapakaa katika sehemu nyingi nchini China, hata katika mji mkuu Beijing wanaishi watu zaidi ya 3000 wa kabila la Sala.

Katika sehemu ya mashariki ya Beijing kuna mkahawa unaoitwa "Nyumba ya Salar". Japokuwa mkahawa huo sio mkubwa sana, lakini biashara yake ni nzuri sana, hasa wakati wa usiku hujaa wateja, na wengine wanapaswa kusubiri meza. Nyama ya ng'ombe na mbuzi na vyakula vya unga wa ngano vilivyotengenezwa kwenye mkahawa huo vina ladha maalum, na vinakaribishwa sana na wateja.

Anayeendesha mkahawa huo Bw. Han Chenfu ni mzaliwa wa kabla la Sala, ambaye alikuja Beijing kutoka maskani yake miaka zaidi ya kumi iliyopita. Mwanzoni alifanya kazi katika mkahawa ulioendeshwa na jamaa yake. Baada ya kujifunza kwa miaka 6, Bw. Han Chenfu aliweza kuanza kuendesha mkahawa wake mwenyewe. Hivi sasa Bw. Han Chenfu amekuwa na familia, amenunua nyumba, na anaishi kwa furaha mjini Beijing.

Bw. Han Chenfu anaona kuwa, Beijing ni mji unaoweza kuwapokea watu wa aina mbalimbali. Marafiki zake walitoka sehemu mbalimbali hata nchi za nje. Wakati mwingi wanaweza kusikilizana vizuri, lakini wakati mwingine kutokana na tofauti za uamini wa dini na desturi, wanakuwa na matatizo kidogo. Bw. Han anasema:

"Mara nyingi marafiki zangu wakifika kwangu, hunilazimisha kunywa pombe. Sisi wasala hatunywi pombe, hivyo sina budi kukataa, au nakunywa chai badala ya pombe."

Kabila la Sala ni moja ya makabila 10 yenye waumini wa dini ya kiislamu. Kutokana na kanuni za kiislamu, waumini hawaruhusiwi kunywa pombe. Japokuwa wameishi mjini Beijing kwa miaka mingi, lakini Bw. Han na familia yake siku zote wanashikilia kufuata mila na desturi ya kidini. Siku za kawaida anafanya swala nyumbani kutokana na biashara ya mkahawa, lakini kila Ijumaa ni lazima aende kuswali kwenye msikiti wa karibu.

Tofauti ya Bw. Han Chenfu, Bi. Ma Xiuying alikuja Beijing mwaka jana. Yeye alikuwa mwalimu wa shule ya msingi huko maskani yake, alipata nafasi ya kuja Beijing na akaupenda mji wa Beijing mara moja. Hivyo aliacha kazi yake ya kufundisha na kuja Beijing pamoja na mtoto wake mwenye umri wa miaka 6. Anapenda maisha yenye pilikapilika, na hali ya kiutamaduni ya mji wa Beijing. Kama wasala wengine walivyofika Beijing mwanzoni, sasa changamoto kubwa inayomkabili Bi. Ma Xiuying ni kutafuta kazi .

"Tumainio langu kubwa ni kuwa mtoto wangu atapata elimu hapa Beijing, ili apate elimu ya kisasa."

Japokuwa wasala waliokuja Beijing wana malengo tofauti, lakini wote wanaupenda mji wa Beijing. Bw. Han Jishang alisoma katika chuo kikuu cha Beijing katika miaka ya 80 ya karne iliyopita. Baada ya kuhitimu aliamua kubaki Beijing. Hivi sasa anafanya kazi katika shirikisho la dini ya kiislamu la China. Shirikisho hilo linashughulikia mambo yanayohusiana na waislamu. Kutokana na bidii yake na kazi bora, Bw. Han Jishang aliwahi kutumwa nchini Saudi Arabia kwa mafunzo. Anaona kazi yake ni yenye maana sana. Anasema:

"Niliambiwa nitunge utaratibu wa kuthibitisha maimamu, utaratibu wa kusimamia misikiti, na utaratibu wa kuthibitisha vyakula vya kiislamu, nafurahia kuzifanya kazi hizo."

Kutokana na umaalum wa kazi yake, Bw. Han Jishang anakutana mara kwa mara na jamaa waliotoka maskani yake. Wanapokusanyika pamoja hupenda kuimba wimbo wa kikabila ambao ni maarufu huko kwao. Wimbo huo unasimulia hadithi ya kabila la Sala na ngamia mweupe. Inasemekana kuwa, miaka zaidi ya 700 iliyopita, wahenga wa kabila moja lililoko sehemu ya Asia ya kati walikuwa wakimkokota ngamia mweupe aliyebeba Kuran, maji na udongo wa maskani kuhamia upande wa mashariki. Walipofika katika mkoa wa Qinghai, China, ngamia mweupe alitoweka gizani. Wahenga hatimaye walimkuta ngamia huyo akiwa amelala kwenye dimbwi la maji. Wakaona kuwa hapo ndipo mahali walipokuwa wanapatafuta, na wakaamua kukaa. Kabila hilo lililohamia hapo ndilo kabila la Sala. Hivyo hadi leo, wasala bado wanamheshimu sana ngamia, na wanaendelea kufuata desturi ya wahenga wao ya kuhamahama, na wanapenda kutafuta sehemu zinazowafaa.

Idhaa ya kiswahili 2005-05-19