Tangu chama tawala cha Ethiopia yaani chama cha "Ethiopian People's Revolutionary Democratic Front (EPRDF)" kitangaze kuwa kimeshinda kwenye uchaguzi wa tatu wa bunge la umma la nchi hiyo na kitaunda serikali mpya hivi karibuni, chama kikubwa cha upinzani cha nchi hiyo yaani chama cha "Coalition for Unity and Democracy (CUD)" tarehe 18 pia kilitangaza kuwa, chama hicho kimepata viti vya kutosha kuunda serikali. Hali hiyo imedhihirisha kuwa, uchaguzi wa bunge la nchi hiyo umesababisha vurugu ya kisiasa nchini humo.
Ethiopia ilifanya uchaguzi wa tatu wa bunge la umma na uchaguzi wa mabunge ya majimbo 8 ya nchi hiyo tarehe 15 mwezi huu. Huo ni uchaguzi wa tatu wa vyama vingi ulioshirikisha wapigaji kura wengi zaidi katika historia. Kwa mujibu wa katiba ya Ethiopia, chama kinachopata viti vingi zaidi kwenye bunge la nchi hiyo kina haki ya kuunda serikali. Habari zinasema kuwa, uchaguzi huo ulivishirikisha vyama 36, vikiwemo vyama vitatu vikubwa. Chama cha EPRDF kimetawala nchi hiyo kwa miaka 14, na hivi sasa, chama hicho kimepata viti 481 kwenye bunge la nchi hiyo.
Tarehe 16 usiku, chama cha EPRDF kilitoa taarifa, kikisema kuwa, ingawa chama hicho hakikupata viti vyovyote kwenye mji mkuu Addis Ababa, lakini kimepata viti vingi kwenye majimbo mengine yenye idadi kubwa ya watu, yakiwemo majimbo ya Kusini Ethiopia, Oromia, Amhara na Tigray, hivyo chama hicho dhahiri kimepata viti vingi zaidi kwenye bunge la nchi hiyo na kitaunda serikali hivi karibuni. Kiongozi wa chama hicho, ambaye pia ni waziri mkuu wa hivi sasa wa nchi hiyo Bw. Meles Zenawi, alitaka chama cha upinzani kikubali "uamuzi wa umma", na pia alisema kuwa atashirikiana na vyama vya upinzani.
Lakini vyama vya upinzani havikubali matokeo yaliyotangazwa na chama cha EPRDF. Kiongozi wa chama cha CUD alisema kuwa, bado ni mapema kutangaza ushindi kabla kazi ya kuhesabu kura haijamalizika. Mara baadaye, naibu mwenyekiti wa chama hicho Bw. Berhanu Nega tarehe 18 alitoa taarifa, akisema kuwa, katika kura zilizohesabiwa, chama hicho kimepata kura nyingi zaidi. takwimu za mwanzo zimeonesha kuwa, chama hicho kimepata viti vyingi vya kutosha kwa kuunda serikali.
Taarifa hiyo imefanya hali ya kisiasa nchini Ethiopia iwe ya utatanishi zaidi. Maoni ya umma yanaona kuwa, tokea wakati wa kampeni za uchaguzi mpaka hivi sasa, vyama hivyo viwili vilikuwa vinaendelea kushindana nguvu kwa njia mbalimbali, na hali ya hivi sasa ni mashindano mapya kati ya vyama hivyo viwili.
Hivi sasa, Tume ya taifa ya uchaguzi ya Ethiopia ikiwa ni idara ya kisheria ya uchaguzi, bado haijatoa maoni yoyote kuhusu vitendo vya vyama hivyo viwili. Kutokana na mpango uliowekwa, matokeo ya uchaguzi huo yatatangazwa tarehe 8 mwezi Julai. Lakini kutokana na hali ya hivi sasa, vyovyote matokeo ya uchaguzi huo yatakavyokuwa, hali ya kisiasa ya nchi hiyo bado haitatulia.
Idhaa ya Kiswahili 2005-05-19
|