Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-05-20 19:59:28    
Mabadiliko ya hali ya hewa duniani huenda yatasababisha kuongezeka kwa sehemu zinazokumbwa na ugonjwa wa malaria nchini Afrika ya Kusini

cri

Ripoti mpya iliyotolewa na taasisi ya utafiti wa aina nyingi za viumbe ya Afrika ya Kusini inaona kuwa, mabadiliko ya hali ya hewa duniani huenda yatasababisha kupanuka kwa sehemu zinazokumbwa na ugonjwa wa malaria nchini humo. Jambo hilo si kama tu litatishia afya za wananchi, bali pia litaathiri sekta ya utalii ya huko.

Taasisi ya utafiti wa aina nyingi za viumbe ya Afrika Kusini tarehe 5 ilitoa ripoti hiyo mjini Capetown, ikisema kuwa katika miaka 50 ijayo, wastani wa joto nchini humo yataongezeka kwa nyuzi 3 sentigredi. Kuongezeka kwa joto katika majira ya baridi kutasababisha sehemu zinazokumbwa na ugonjwa wa malaria ziongezeke kutoka sehemu ndogo iliyoko kaskazini mashariki mwa nchi hiyo ya hivi sasa hadi kufikia sehemu nzima ya kaskazini na mikoa ya mashariki, pamoja na majimbo ya Mpumalanga, Limpopo, Kaskazini Magharibi, Kwazulu-Natal na Gauteng. Kama ugonjwa huo utaenea katika eneo kubwa, si kama tu utahatarisha afya za wakazi wa huko, bali pia utasababisha kupungua kwa idadi ya watalii kutoka nchi za nje, na kuathiri vibaya sekta ya utalii ambayo ni sekta muhimu ya uchumi wa Afrika ya Kusini.

Ingawa ugonjwa wa malaria unaweza kukingwa na kudhibitiwa, lakini kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO), watu milioni 1 wanakufa kila mwaka kutokana na ugonjwa huo barani Afrika, na wengi wao ni watoto wadogo.

Ripoti ya taasisi ya aina nyingi za viumbe pia inaonya kuwa, Afrika ya Kusini ni nchi ambayo ni rahisi kwake kuathiriwa na mabadiliko ya hali ya hewa. Kuongezeka kwa joto duniani katika miaka 50 ijayo kutasababisha upungufu wa maji, kupungua kwa mavuno ya nafaka, hali mbaya ya hewa yakiwemo mafuriko, mvua ya mawe na tufani, na kutoweka kwa aina nyingi za viumbe nchi kavu na baharini.

Waziri wa mazingira na utalii wa Afrika ya Kusini Bw. Marthinus van Schalkwyk alisema kuwa, mabadiliko ya hali ya hewa yataipatia Afrika ya Kusini mabadiliko makubwa katika miaka 20 hadi miaka 30 ijayo. Mabadiliko hayo huenda yatatokea mapema zaidi katika sehemu ya magharibi, yaani yatatokea baada ya miaka 10 hadi miaka 15. Anaona kuwa, ingawa hivi sasa wananchi hawana haja ya kuwa na wasiwasi kubwa, lakini suala la mabadiliko ya hali ya hewa lazima lizingatiwe.

Bw. Marthinus van Schalkwyk alisema kuwa, serikali ya Afrika ya Kusini inapanga kuunda tume ya kushughulikia kufanya utafiti kuhusu njia ya kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa, na kufanya mkutano utakaohudhuriwa na wanasayansi wa nchi mbalimbali za Afrika mwezi Oktoba mwaka huu, ili kujadili suala la mabadiko ya hali ya hewa.

Idhaa ya Kiswahili 2005-05-20