Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-05-23 14:59:52    
Mwandishi mashuhuri wa vitabu Lan Huaichang

cri

Mwandishi mashuhuri wa vitabu Lan Huaichang ni mtu wa kabila la Wayao ambalo lina jumla ya watu milioni mbili tu nchini China. Miaka 30 iliyopita kabila hilo lilikuwa halina riwaya ndefu, hadi riwaya yake ya "Mto Bonu" ilipochapishwa.

Bw. Lan Huaichang ametimiza umri wa miaka 60, ni mwenyekiti wa Shirikisho la Waandishi wa Vitabu la Wilaya Inayojiendesha ya Kabila la Wayao mkoani Guangxi, kusini mwa China. Alihitimu katika idara ya lugha ya Kichina mwaka 1968 katika Chuo Kikuu cha Makabila Madogo Madogo cha Zhongnan, na kuwa mtunzi wa michezo katika Kundi la Nyimbo na Dansi la Kijeshi katika mji wa Guangzhou. Kutokana na kuwa wakati huo kilikuwa kipindi cha Mapinduzi ya Utamaduni nchini China, alikuwa hana uhuru wa mkubwa wa kuandika mpaka mwishoni mwa miaka ya 70, ndipo alipoanza kuandika. Bw. Lan Huaichang alisema, "Baada ya kuwa mtunzi wa michezo katika Kundi la Nyimbo na Dansi la Kijeshi kwa miaka saba, niliondoka kutoka kundi hilo na kuwa mwandishi wa vitabu nikishiriki katika maandishi ya historia ya fasihi ya kabila la Wayao, niligundua kuwa kabila hilo halikuwa na riwaya ndefu katika historia yake ya fasihi, nikaamua kuandika riwaya ndefu kutokana na wazo ambalo kama kabila fulani halina riwaya yake ndefu katika historia yake ya fasihi, uzito wa utamaduni wa kabila hilo unapungua."

Kitabu kilichompatia umaarufu mwandishi huyo ni riwaya yake ndefu "Mto Bonu". Riwaya hiyo imeziba pengo la kukosa riwaya ndefu katika historia ya fasihi ya kabila la Wayao, na ilipata tuzo ya kwanza katika mashindano ya maandishi mkoani Guangxi mwaka 1988.

Riwaya hiyo ilitungwa katika mazingira ya miaka ya 80 ambapo China ilianza kufungua mlango kiuchumi na kufanya mageuzi, ikisimulia kuhusu Wayao wanaoishi katika bonde la Mto Ponu walivyofanya juhudi kuondokana na umaskini. Riwaya hiyo ikiwa na dhamira hiyo imeeleza vituko mbalimbali vilivyotokea maishani katika siku za mwanzo wa mageuzi. Riwaya hiyo ilisifiwa sana na wasomaji na waandishi. Kuhusu riwaya hiyo, Bw. Lan Huaichang alisema, "Katika riwaya yangu hii nilieleza mambo mengi ya mila, desturi na utamaduni wa kabila langu, mambo ambayo yaliniathiri sana tokea utotoni mwangu, kwa hiyo niliandika kwa mfululizo bila kufikiri sana."

Bw. Lan Huaichang ni mwandishi asiyechoka, baada ya riwaya yake ya "Mto Ponu" kuchapishwa alifululiza kumaliza riwaya zake za "Roho Iliyokatika katika Kisiwa Kilichotengwa", "Harusi ya Marehemu", "Machafuko ya Bahari ya Kaskazini" na riwaya nyingine na mashairi. Hivi sasa riwaya zake nyingi zimejulishwa na waandishi nchini Japani.

Akiwa mwandishi mkubwa Bw. Lan Huaichang anaona kuwa riwaya zinapaswa kuonesha mambo yaliyomo mioyoni mwa watu na yaliyo mazuri ya kufundisha katika maisha ya watu, kwa hiyo waandishi wanapaswa kuchuja habari walizo nazo na kutunga riwaya kwa utu. Alisema, "Naona tungo za fasihi ni bora ziandikwe kwa mambo ya kweli ambayo yanaonesha asili ya binadamu, sipendelei kuandika yale yanayoambatana sana na siasa, hata kama mageuzi yanayofanyika sasa ni bora yaandikwe kuambatana na asili ya binadamu, maandishi kama hayo yanaweza kusomwa miaka hadi miaka." bila kupitwa na wakati.

Licha ya kushughulika na maandishi, Bw. Lan Huaichang anashiriki kwenye shughuli nyingi za utamaduni, "Kamusi ya Makabila Madogo Madogo-Kabila la Wayao" iliyoihariri imechapishwa, mchezo wa televisheni alioutunga "Mtoto Shupavu" ulipata tuzo, pia aliandika maneno mengi ya nyimbo. Watu husema yeye ni mwandishi wa sanaa za aina nyingi.

Idhaa ya kiswahili 2005-05-23