Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-05-24 15:57:53    
Barua0524

cri

Hotuba ya Bwana Xavier L. Telly-Wambwa

Nachukua nafasi hii kwanza kumshukuru mwenyezi mungu aliyeumba mbingu na dunia na kila kitu kiliomo. Namshukuru kwa kuiwezesha kusafiri salama salimini hadi hapa nchini China.

Kwanza kabisa pokeeni salamu kutoka kwa wasikilizaji wenzangu wa CRI nchini Kenya na Bara la Afrika kwa ujumla.

Kwa majina ni Bw. Xavier L Telly Wambwa na nilizaliwa mwaka wa 1972 katika kijiji cha Nalondo, wilaya ya Bungoma, mkoani magharibi nchini Kenya.

Nimeoa na nina watoto sita na pia ningependa kuwajulisheni kuwa wazazi wangu ni Bw. Joseph Martin Khisa na Bi. Hilda Nakhumicha Khisa. Mimi ndiye mtoto wa kwanza katika familia ya watoto wanne.

Baada ya kumaliza masomo ya shule ya upili, niliendelea na masomo ya Diploma. Baadaye niliweza kuajiriwa kazi katika wizara ya serikali ya wilaya kwenye baraza la wilaya ya Bungoma.

Hata hivyo matakwa yangu ya kila siku ni kuwa siku moja nipate kufanya kazi na idara ya Kiswahili ya CRI.

Nilianza kuwa msikilizaji wa CRI nikiwa kidoto chakwanza katika shule ya upili ya Cheptais, mnamo mwaka wa 1989. Ingawa sikuwa na bidii ya kutosha wakati huo, nilijitahidi kuanzia mwaka wa 1997 ambapo kila mwaka nimepewa vyeti na zawadi kutoka CRI.

Bungoma ndio mji mkubwa wa karibu ukiwa Kilo Mita kumi na tatu (13) kutoka kijiji nilipozaliwa ilihali kutoka mji mkuu wa Kenya-Nairobi ni karibu kilo mita mia nne (400). Idadi ya watu katika wilaya hii ya Bungoma ni kiwango cha watu milioni moja na nusu (1,500,000). Mji wa Bungoma ni takribani kilo mita hamsini (50) kutoka nchi jirani ya Uganda, na kilo mita karibu themanini (80) kutoka Mlima Elgon uliyo wa tatu kwa ukubwa Afrika Mashariki.

Katika eneo hili kuna ukulima. Mazao ya mahindi hupendwa kwa wingi, viazi vitamu, maharagwe, njugu, ndizi na matunda aina mbalimbali

Chakula kinachopendwa sana ni Ugali ambao huliwa na mboga za kienyeji kama kunde, saka na murere.

Ningependa kuwafahamisha kwamba CRI imekuwa ya manufaa kwa wananchi wa Kenya. CRI husikika saa kumi na moja jioni hadi unusu kupitia idhaa ya kiswahili ya KBC. Kama wananchi, tumpata fursa ya kujua mengi yanayotendeka nchini China na mataifa mengine ya kigeni, kupitia kwa vipindi kemkem vya CRI.

Mambo kadha wa kadha ambayo ningependa kuangazia kuhusu nchi yangu ni kama yafuatayo.

1. Ustawi wa uchumi baina ya Kenya na China

ningependa kuwafahamisheni kuwa nchi yetu ya Kenya imepokea misaada mingi sana kutoka hapa China. Baadhi ya yale mambo ambayo China imepata kutekeleza ni kama, kujenga uwanja wa michezo wa Kimataifa wa Kasarani, barabara kadha wa kadha na Hospitali ya Nyayo ya Webuye. Kuna mengi ambayo China imefanya, nami nashukuru sana kwa niaba ya nchi ya Kenya.

2. Hali ya Uchumi

naangazia kuwa Kenya ni nchi ambayo haijastawi. Hata hivyo inajikakamua vilivyo kuhakikisha kuwa wananchi wanaepuka jamga la umaskini ambalo limekithiri mahala pangi nchini. Serikali ya muungano wa NARC inajaribu kuhakikisha kuwa vyakula, malazi, mavazi na nyumba zapatikana kwa wakenya wote. Mapato ya wastani ya kila Mkenya ni chini ya Dola Moja ya Marekani kwa siku.

3. Elimu

Serikali ya Muungano wa NARC ilifanya jambo la maana sana kuanzisha elimu ya bure kwa wanafunzi wa shule za msingi kwote nchini. Sasa wazazi wamepumzishwa mzigo wa kulipa karo. Hata hivyo, idadi kubwa ya wanafunzi imechagia pakubwa ukosefu wa madarasa ya kutosha na walimu. Jambo hili linatiliwa maanani na Wizara ya Elimu. Sehemu nitokako yahitaji vyuo vikuu ili kurahisisha usajili wa wanafunzi wanaofuzu kujiunga na vyo hivyo. Tayari kuna sehemu ambayo imetengwa kwa ujenzi wa chuo kikuu cha Kibabii. Kadhalika katika wilaya ya Bungoma tunahitaji kwa dharura jumba la maktaba la kissasa. Shirika la moja ambalo bado halijastawi limejaribu kuanzisha huduma za maktaba lakini linahitaji usaidizi ili kuwa dhabiti.

4. Michezo

nchi yetu ya Kenya imejulikana kwa michezo mbalimbali. Baadhi ya michezo ni kama mbio, Kandanda, Ndondi, Karate, Tae-Kwo-Ndo, Uogeleaji, Sarakasi na mchezo wa Magongo. Michezo hii ni ya manufaa sana kwani hutumiwa mara kwa mara kuwaelimisha vijana na wazee juu ya ugonjwa hatari wa ukumwi. Kwa hivyo tunahitaji vifaa zaidi vya kuimarisha michezo hii.

5. Utalii

Kenya ni nchi inayojivunia mazingira bora sana ya utalii. Mwongozo mzuri wa serikali yetu ya Muungano wa NARC umevutia mamilioni ya watalii kutoka nchi tofauti tofauti ikiwemo China wanaozuru sehemu mbalimbali nchini Mwetu. Sehemu za utalii ni kama Mbuga za Maasai-Mara, Tsavo, Amboseli, na pia Mlima Kilimanjaro, Kenya na Elgon. Nyote mwakaribishwa Kenya. Wanyama wanaopatikana katika Mbuga zetu ni kama Wafwatao: Simba, Nyati, Ndovu, Kifaru, Punda Milia, Swara Nyekundu, Mbuni na Kadhalika.

6. Mazingira, ukulima na viwanda.

Waziri wetu msaidizi wa mazingira Bi. Profesa Wangare Maathai alituletea sifa nzuri aliposhinda tuzo la Amani. Hii ni dhihirisho kuwa nchi yetu inanuia kulinda mazingira yetu na kuhifadhi amani pote.

Nikiangazia ukulima tunafanya vyema sana. Mfano ni kuwa wilaya ya Bungoma inajihusisha na ukulima wa aina mbalimbali ya mazao.

Kuna viwanda viwili, kimoja ni cha kusaga Miwa cha Nzoia na cha pili ni cha kutengeneza karatasi cha Pan Paper kule Webuye. Hata hivyo tunahitaji viwanda vingine vya kushughulikia haya mazao mengine.

7. Usalama

ningelipenda kuwajulisheni kuwa hali ya usalama nchini Kenya imeimarishwa na sasa wananchi na wageni wanatekeleza majukumu yao bila wasiwasi wowote. Waziri wa usalama Bw. John Michuki amehakikisha Polisi wana jukumu la kulinda maslahi ya watu wote kwa hivyo wachina wote mnakaribishwa kuzuru Kenya nchi ya amani, upendo na umoja.

8. Dini

Nchini Kenya kuna aina mbalimbali za dini. Kati ya hizi ni Kikristo, Kiislamu, Kihindi na nyingine mbalimbali. Dini ya kikristo ndiyo kubwa zaidi nchini kote, lakini kuna uhuru wa kuabudu kwa dini mbalimbali.

9. Lugha

Kiswahili ni lugha ya kibantu ambayo uzungumzwa na mataifa mengi barani Afrika. Lugha rasmi nchini Kenya ni Kiswahili na Kingereza. Hata hivyo kuna makabila arobaini na mbili (42) nchini Kenya. Watu wengi hupenda sana lugha hizi lakini hivi sasa kwa ajili ya ushirikiano mewma baina ya nchi ya China na Kenya, basi wananchi wengi wameanza kujifunza, kuongea na kuandika lugha ya kichina. Hata pia siku hizi waafrika na wachina huoana.

10. Kutamatisha

Kulingana na maangazio haya yote nachukua nafasi hii kuwakaribisheni Kenya mkazuru na kujionea mengi. Pia wawekezaji wote wakaribishwa Bungoma kuiendeleza wilaya hii kwa njia yoyote ile. Ingekuwa bora zaidi kama Redio China Kimataifa inejenga ofisi mtambo wa kurushia matangazo Barani Afrika nchini Kenya, na kama ni hivyo basi Wakenya wengi watapata kuajiriwa.

Pia nachukua nafasi hii kuwajulisheni kuwa, tunahitaji maktaba ya jamii wilayani Bungoma. Maomba wahisani wajitokeze kuanzisha mradi huu ambao utakua wa manufaa kwa wanafunzi, wakazi wa Bungoma na nchi nzima kwa jumla. Kwa sasa kuna maktaba ambayo haijastawi barabara kwa ukosefu wa fedha. Shirika ambalo linaendesha mradi huo halijastawi vilivile kutimiza shughuli hiyo. Hivyo basi naomba wawekezaji na wahisani wajitokeza kuleta maendeleo Bungoma.

Vilevile Kenya inajivunia uhusiano mzuri ulioko baina yake na nchi ya China chini ya balozi Guo Chongli. Udiplomasia kati ya China na Kenya ukapate kudumu.

Idhaa ya kiswahili 2005-05-24