Tarehe 25 Irani itafanya mazungumzo na nchi tatu za Umoja wa Ulaya kwa mara ya mwisho kuhusu suala la nyuklia la Iran mjini Geneva. Viongozi waandamizi wa pande mbili walifanya maadalizi tarehe 24 kwa ajili ya mazungumzo hayo. Kutokana na kuwa Iran imekwisha eleza msimamo wake kuwa vyovyote matokeo ya mazungumzo yatakavyokuwa Iran lazima itaanza tena shughuli za kusafisha uranium, kwa hiyo mazungumzo hayo ni fursa ya mwisho kwa suala la nyuklia la Iran.
Suala la nyuklia la Iran linatokea mbali. Mapema katika miaka ya 50 ya karne iliyopita, Iran iliingiza teknolojia ya nyuklia kutoka Marekani na nchi za Ulaya. Mwaka 1979 baada ya mapinduzi ya Kiislamu, mradi wa nishati ya nyuklia nchini Iran ulisimama. Mwanzoni mwa mwaka 2003 Iran ilipotangaza kuwa imefanikiwa kupata nishati ya uranium ya kuzalisha umeme mara ilipingwa na Marekani na ilisababisha ufuatiliaji mkubwa wa jumuyia ya kimataifa. Kwa kusuluhishwa na jumuyia ya kimataifa na hasa nchi tatu za Ufaransa, Ujerumani na Uingereza, Iran ilitia saini waraka wa nyongeza wa "mkataba wa kutoeneza silaha za nyuklia". Kisha nchi hizo tatu zilitoa mapendekezo ya kuisaidia Iran kwa teknolojia na nyenzo za nyuklia, na kuweka ushirikiano wa pande mbalimbali kwa sharti la Iran iache kusafisha uranium. Baada ya kufanya mazungumzo mara nyingi, pande mbili ziliafikiana makubaliano.
Ili kutekeleza makubaliano hayo, kuanzia mwezi Desemba mwaka jana, nchi hizo tatu zilifanya mazungumzo na Iran mara saba. Ingawa mazungumzo yalipata matokeo fulani, lakini kila upande unashikilia uzi wake katika masuala muhimu, kwa hiyo mpaka sasa hayakupata mafanikio yoyote ya maana. Msimamo wa Umoja wa Ulaya ni kuwa Iran lazima iache kabisa shughuli za kusafisha urniumu kwa sababu teknolojia hiyo ni rahisi kutumika katika matengenezo ya silaha za nyuklia. Msimamo wa Iran ni kuwa kusafisha uraniumu ni haki yake. Kwa hiyo tarehe 30 Aprili ilitangaza kuwa itarudisha shughuli hizo.
Wachambuzi wanaona kuwa Iran inaona haina kosa lolote kuendeleza uranium kwa ajili ya matumizi ya amani, na msimamo huo unaungwa mkono na nchi nyingi ikiwemo Russia. Pili ni kuwa Iran ni nchi ya pili katika uzalishaji wa mafuta ikifuata Saudi Arabia, katika hali ya sasa ambapo bei ya mafuta imepanda juu, nchi za Magharibi lazima zitafakari vya kutosha kabla ya kuomba Baraza la Usalama kuiwekea vikwazo vya uchumi. Zaidi ya hayo nchi za Ulaya ni wateja wakubwa wa mafuta ya Iran, kama zikiichukulia hatua, walioathirika zaidi ni nchi za Magharibi. Kutokana na hali ambapo Marekani imetopea katika matope ya Iraq haiwezi kuichukulia Iran hatua za kijeshi.
Msimamo mgumu wa Irani umezidisha wasiwasi wa nchi za Ulaya. Mawaziri wa nchi tatu za Umoja wa Ulaya waliionya Iran iache kabisa shughuli za kusafisha uranium, vinginevyo "mazungumzo yatamalizwa". Umoja wa Ulaya hauwezi kukubali hata kidogo Irani kurudisha shughuli za kusafisha uranium kwa sababu hii inakwenda kinyume na lengo la nchi za Magharibi katika suala la nyuklia la Iran. Kadhalika, Marekani haitakukubali pia.
Marekani inashutumu kwamba Iran inataka kutengeneza silaha za nyuklia kisiri kwa kisingizio cha "matumizi ya amani". Inasisitiza kuwa kuachilia mbali daima shughuli za kusafisha uranium ni kigezo pekee cha kupima uaminifu wa Iran. Si muda mrefu uliopita Marekani ilirekebisha sera zake kuhusu Iran lakini kuhusu suala la nyuklia la Iran haikubadilika. Hivi sasa Marekani inapounga mkono nchi za Umoja wa Ulaya kufanya mazungumzo na Iran haina matumaini yoyote kuhusu mazungumzo hayo, inaona kuwa tatizo hilo hakika litawasilishwa kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Katika miaka mingi iliyopita pande zote mbili za Umoja wa Ulaya na Iran zinaelewana sana msimamo wa kila upande, na zinaelewa nini unachotaka kila upande. Ingawa mazungumzo ya tarehe 25 ni "fursa ya mwisho", yumkini mazungumzo yataendelea, kwani mazungumzo yakimalizwa na suala la nyuklia la Iran likipelekwa kwenye Baraza la Usalama, pande zote hazitaambulia chochote.
Idhaa ya kiswahili 2005-05-25
|