Jeshi la Marekani lililoko nchini Iraq tarehe 25 liliendelea kuyasaka makundi yanayoipinga Marekani mjini Haditha, magharibi mwa Iraq. Hii ni mara ya pili kwa jeshi la Marekani kuyasaka makundi yanayopambana na Marekani mwezi huu katika sehemu ya magharibi nchini humo.
Jeshi la Marekani lilitoa taarifa likisema kuwa askari 1000 wa jeshi la Marekani wakisaidiwa na helikopta na maderaya walifanya operesheni ya msako uitwao "New Market" mjini Haditha, kaskazini magharibi mwa mji wa Baghdad. Jeshi la Marekani sio tu liliweka vituo cha ukaguzi pembezoni mwa mji wa Haditha, ili kuuzingira mji huo, bali pia liliingia mjini humo kuwasaka askari waliojificha huko na kupambana na jeshi la Marekani. Kikosi kidogo cha jeshi la Iraq pia kilishiriki kwenye operesheni hiyo. Jeshi la Marekani lilisema kuwa jeshi hilo lilipambana na kundi moja mjini Haditha na kuwaua askari wake wasiopungua 10 na askari wawili wa jeshi la Marekani walijeruhiwa.
Baada ya kuundwa kwa serikali ya mpito ya Iraq, makundi yenye silaha yalifanya mashambulizi mfululizo dhidi ya jeshi la Marekani na kikosi cha polisi na maofisa waandamizi wa Iraq, na kusababisha vifo vya watu zaidi ya 620. Ili kukomesha mashambulizi hayo yanayoongezeka siku hadi siku, kuanzia tarehe 7 hadi tarehe 14 mwezi huu, jeshi la Marekani lilianzisha operesheni iitwayo "Matador" ya kuyasaka makundi yanayolipinga jeshi la Marekani, watu wenye silaha wasiopungua 125 waliuawa, mia kadhaa kujeruhiwa na 39 walikamatwa. Kuanzia tarehe 22, jeshi la muungano wa Marekani na Iraq liliyasaka makundi yenye silaha magharibi mwa Baghdad, watu 440 walikamatwa.
Vyombo vya habari vya kiarabu vinaona kuwa katika mwezi mmoja uliopita, jeshi la Marekani lilifululiza kufanya shughuli kubwa za usakaji kutokana na hali ya usalama ya Iraq kuwa mbaya. Kama jeshi la Marekani halitazuia shughuli za makundi yenye silaha ya Iraq, basi mchakato wa ukarabati wa demokrasia wa Iraq ulioendeshwa na jeshi la Marekani utaathiriwa sana.
Kufanya shughuli za usakaji kwa jeshi la Marekani kulipata mafanikio, idadi kubwa ya askari wa makundi yanayoipinga Marekani walitiwa nguvuni. Kundi la Al-Qaeda la Jihad tarehe 25 ilithibitisha kuwa kiongozi wa jumuiya hiyo Abu Al-Zarqawi alijeruhiwa kifuani na kupelekwa nchi za nje kwa kutibiwa.
Kwa upande mwingine, msako wa jeshi la Marekani ulirejeshewa pigo kali na makundi ya kupambana na jeshi la Marekani. Tarehe 23, milipuko minne ilitokea nchini Iraq na kusababisha vifo na majeruhi ya watu zaidi ya 200.
Wachambuzi wanaona kuwa kwa kuwa msako unaofanywa na jeshi la Marekani hauungwi mkono na watu wa Iraq, na hali ya usalama bado ni hatari nchini Iraq.
Idhaa ya kiswahili 2005-05-26
|