Mkutano wa 58 wa afya duniani uliofanyika kwa siku 10 ulifungwa tarehe 25 huko Geneva baada ya kupitisha nyaraka mbili kuhusu "Azimio la kinga na tiba ya saratani" na "Mikakati ya dunia nzima ya kutoa chanjo".
Mkutano huo ulihudhuriwa na wajumbe 2200 kutoka nchi 193. Mkutano huo ulifanya majadiliano kuhusu kudhibiti magonjwa ya ukimwi, SARS, homa ya mafua ya ndege na malaria ambayo ni magonjwa maambukizi yanayotishia zaidi afya za binadamu, pia kujadili namna ya kukabiliana na matukio yanayoibuka kwa ghafla katika sekta ya afya kote duniani, na kuitisha maazimio husika.
Kauli mbiu ya mkutano huo ni "kuthamini kila mama mzazi na kila mtoto". Mkutano huo unaona kuwa, suala la afya za akina mama na watoto linahusiana moja kwa moja na maendeleo ya nchi na siku za usoni za dunia. Kila mtu mwenye busara anayeshughulikia kazi za afya anapaswa kuzingatia kwanza suala la afya za akina mama na watoto, kuhamasisha nguvu za serikali na pande mbalimbali na kufanya juhudi za kuinua kiwango cha afya za akina mama na watoto.
Mafanikio makubwa zaidi ya mkutano huo ni kupitishwa kwa "vifungu vipya vya afya vya kimataifa". Vifungu hivyo vipya vimeongeza utaratibu mpya na hatua za uratibu kuhusu dunia nzima kukabiliana na magonjwa ya maambukizi yanayoibuka kwa ghafla na kuambukiza kwa kuvuka mpaka, na kuongeza mambo yanayosistiza upimaji na udhibiti wa magonjwa ya SARS, homa ya mafua ya ndege na ukimwi. Vifungu hivyo vipya vimesistiza kuwa, ni lazima kuongeza mawasiliano kati ya shirika la afya duniani na nchi wanachama wake, na nchi wanachama wanapaswa kuimarisha kazi ya ufuatiliaji na utoaji tahadhari juu ya magonjwa ya maambukizi, kuongeza uwezo wa kukabiliana na hali ya dharura na ujenzi wa miundo mbinu ya afya za umma. Kuhusu matukio ya dharura ya afya za umma, vifungu hivyo vipya vinazitaka nchi wanachama kutoa ripoti na kupashana habari kwa wakati na kuchukua hatua za lazima za afya, ambapo shirika la afya duniani linapaswa kutoa mapendekezo ya muda na mapendekezo ya muda mrefu, kuzuia na kupunguza maambukizi ya kimataifa ya magonjwa, na kuepusha usumbufu usio wa lazima juu ya mawasiliano ya kimataifa.
Vyombo vya habari vinaona kuwa, vifungu hivyo vipya ni silaha zenye ufanisi kwa jumuiya ya kimataifa katika kulinda afya ya umma katika hali ya hivi sasa ambayo mawasiliano ya kimataifa yanaendelea kwa haraka, na magonjwa ya aina mpya ya maambukizi yanatokea mara kwa mara ambayo huenda yanaweza kuambukiza kwa haraka, vifungu hivyo vitafungua ukurasa mpya wa historia ya afya za umma duniani.
Azimio la kinga na tiba ya magonjwa ya saratani lililopitishwa kwenye mkutano huo limezitaka nchi wanachama wa shirika la afya duniani zitunge mipango ya kinga na tiba ya saratani na kuchukua hatua za kuboresha hali ya tiba na utunzaji kwa wagonjwa.
Waraka wa Mikakati ya dunia nzima ya kupiga chanjo umesisitiza kuwa lazima mikakati ya dunia nzima ya kutoa chanjo kuanzia mwaka 2006 hadi 2015 itekelezwe, ili kupunguza magonjwa ya aina mbalimbali duniani.
Kwa kuchokozwa na utawala wa Taiwan, nchi chache pamoja na Sao tome na Principe ziliomba tena kuweka pendekezo la kuialika Taiwan kuwa mchunguzi kwenye mkutano wa afya duniani, lakini pendekezo hilo lilikataliwa na nchi nyingi kama miaka iliyopita. Waziri wa afya wa China Bwana Gao Qiang alidhihirisha kwenye mkutano huo kuwa, China inashikilia kanuni ya kulinda kithabiti mamlaka ya nchi na ukamilifu wa ardhi, na kutoruhusu mtu yeyote kufanya shughuli za ufarakanishaji kwa kisingizio cha mkutano wa afya duniani, aidha haiwezi kubadilisha sera yake ya kulinda haki na maslahi halali ya ndugu wa Taiwan.
Idhaa ya Kiswahili 2005-05-26
|