Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-05-26 18:36:31    
Madaktari vipofu wanaofanya kazi katika hospitali ya kukanda ya Beijing

cri

Kati ya watu bilioni 1.3 wa China kuna walemavu milioni 60. Nchini China, walemavu wanafuatiliwa sana na serikali na jamii. Kila Jumapili ya tatu ya mwezi Mei ni siku ya kuwasaidia walemavu nchini China, serikali imeweka siku ya walemavu kwa kulenga kuwahimiza wananchi kuwafuatilia zaidi walemavu ili kuboresha mazingira ya kazi na maisha ya walemavu.

Hospitali ya kukanda ya Beijing ni hospitali kubwa kabisa ya aina hiyo nchini China, ina madaktari zaidi ya 100, kati ya madaktari hao, zaidi ya 40 ni vipofu au wenye matatizo ya kuona.

Hospitali hiyo iko katika majengo yasiyokuwa na ghorofa na kujengwa kwa kuzunguka ua, katikati ya mji wa Beijing. Mwandishi wetu wa habari alipoitembelea hospitali hiyo alimkuta daktari kipofu Bw. Zheng Li akimkanda mgonjwa. Mgonjwa huyo aliumia kiuno chake kutokana na kubeba mzigo mzito. Bw. Zheng Li anasema:

"Mgonjwa huyo anaumiwa kiuno, ninamkanda kutoka pembe ya uti wa mgongo ulioumia, uti wa mgongo, kiuno hadi sehemu ya mwisho ya uti wa mgongo, ili kulegeza na kurekebisha misuli yake."

Daktari Zheng Li ana umri wa miaka 35, alipoteza uwezo wake wa kuona kutokana na ugonjwa wa mtoto wa jicho. Bw Zheng Li alipokuwa mwanafunzi katika shule ya msingi ya watoto wasioona alikuwa na hamu kubwa ya kujifunza matibabu ya jadi ya kichina. Alipoingia katika shule ya sekondari, alianza kujifunza jinsi ya kukanda, baada ya kuhitimu masomo ya sekondari, aliendelea kujifunza mambo ya kukanda katika chuo kikuu. Sasa amefanya kazi katika hospitali hiyo kwa miaka zaidi ya kumi.

Bw. Zheng Li na wenzake wamewahudumia wagonjwa wengi wenye maradhi sugu kama vile ya pingili nyembamba ya uti wa mgongo. Kutokana na matibabu yao mazuri, wagonjwa wengi wamepona bila kufanyiwa operesheni, Bw. Wang Minhuan ni mmoja wa wagonjwa hao. Anasema:

"Mimi nimeumia vibaya uti wa mgongo katika sehemu ya kiuno, hata sikuweza kwenda haja. Ingenigharimu fedha nyingi kama ningefanyiwa operesheni. Madaktari wasingaji wa hospitali hiyo wananitibu kwa njia ya kukanda, sasa nimeanza kupona."

Hivi sasa hospitali ya kukanda ya Beijing kila siku inawapokea wagonjwa zaidi ya 400. Mkuu wa hospitali hiyo Bw. Lai Wei alisema kuwa, maendeleo ya hospitali hiyo yanatokana na juhudi za kila daktari hasa madaktari vipofu, ambao wana juhudi kubwa katika kazi zao.

Imefahamika kuwa, madaktari vipofu wenye kiwango cha kitaalamu kila mwezi wanapata mshahara yuan elfu nane au tisa, hata wale wanaohitimu tu kutoka shule wanaweza kupata yuan elfu tano kwa mwezi.

Mkuu Lai Wei alisema kuwa, madaktari vipofu wameleta manufaa kwa hospitali, kwa upande mwingine hospitali inawatendea vizuri kikazi na kimaisha. Ili kuinua kiwango chao cha ukandaji, hospitali kila mwaka inamlipia na kumtuma daktari mmoja kipofu kusomea shahada ya pili katika chuo kikuu cha matibabu ya kichina cha Beijing.

Bw. Xiang Dong mwenye umri wa miaka 37 ni daktari kipofu wa hospitali hiyo na pia ni mshabiki wa kompyuta, licha ya kutafuta data kwenye mtandao wa Internet, yeye pia anapenda "kusoma" habari au riwaya, na "kusikiliza" muziki kwenye kompyuta. Akiwa kipofu hawezi kutumia kompyuta ya kawaida, kwa hiyo anatumia software maalum iliyonunuliwa na hospitali. Anasema:

"Kompyuta yetu ina software maalum ya kusoma maneno yanayooneshwa kwenye screen. Pia tunaweza kurekodi sauti hizo kwenye kinasasauti au MP3 na kusikiliza tena baadaye."

Bw. Xiang Dong alisema kuwa, ili kuboresha maisha yao baada ya kazi, hospitali mara kwa mara inaendesha shughuli za kiutamaduni kama vile kucheza dansi, madaktari wa kawaida huwaalika madaktari vipofu na kuwafundisha kucheza dansi.

Katika hospitali ya kukanda ya Beijing, madaktari vipofu na madaktari wa kawaida wanasaidiana na kufundishana, na wanasikilizana vizuri. Bi. Yang Yang ni daktari wa kawaida, alisema anaishi na kufanya kazi pamoja na madaktari vipofu bila kuwaona kama ni walemavu. Kutokana na kuzoea kuishi pamoja na vipofu, hivyo kila akiwakuta vipofu mtaani huwasaidia.

Idhaa ya Kiswahili 2005-05-26