Kutokana na Marekani kutopinga tena kuanzisha mazungumo kuhusu Iran kushiriki kwenye Shirika la Biashara Duniani, baraza la shirika hilo tarehe 26 lilikubali kuanzisha mchakato wa Iran kushiriki kwenye shirika hilo. Inajulikana kuwa Iran ni moja ya "nchi ovu" kwa maoni ya Marekani. Siku zote Marekani inatekeleza sera ya kuizuia. Lakini ni sababu gani inayoihimiza Marekani kubadili msimamo wake na kutopinga kuanzisha mchakato wa Iran kushiriki kwenye Shirika la Biashara Duniani?
Watu wametambua kuwa, tarehe 25 mawaziri wa Ufaransa, Ujerumani, na Uingereza wakiuwakilisha Umoja wa Ulaya walifanya mazungumzo na mwakilishi wa kwanza wa mazungumzo ya suala la nyuklia la Iran Bw. Hassan Rowhani. Baada ya mazungumzo hayo walitangaza kuwa, mazungumzo kuhusu suala la nyuklia kati ya Iran na nchi hizo tatu yataendelea. Umoja wa Ulaya utatoa mapendekeo kamili kabla ya mwishoni mwa mwezi Julai, ili kuondoa vikwazo vya mazungumzo ya nyuklia. Habari zinasema kuwa, mapendekezo hayo yatakuwa ni pamoja na pendekezo kuhusu Iran kushiriki kwenye Shirika la Biashara Duniani. Wanadiplomasia wa nchi za magharibi wamedokeza kuwa, Mabadiliko ya msimamo wa Marekani yameonesha kuwa Marekani inaunga mkono Umoja wa Ulaya na Iran kuendelea kufanya mazungumzo, na kuihimiza Iran kuendelea kutekeleza ahadi yake ya kusimamisha vitendo vya kusafisha uranium.
Iran ilitoa ombi la kushiriki kwenye Shirika la Biashara Duniani mwaka 1996, lakini mwakilishi wa Marekani alipinga katika mikutano iliyopita ya baraza la shirika hilo. Takwimu zimeonesha kuwa, tangu mwezi Mei mwaka 2001, Marekani ilipinga kuanzisha mchakato wa Iran kushiriki kwenye Shirika la Biashara Duniani mara 21. Maoni ya raia yanaona kuwa, Marekani inabadili msimamo wake kutokana na mbinu yake.
Kwanza, Marekani inatekeleza makubaliano kati ya Marekani na Ulaya kuhusu suala la nyuklia la Iran, makubaliano hayo ni pamoja na Marekani kutoipinga Iran kushiriki kwenye Shirika la Biashara Duniani. Hivi sasa mazungumzo ya nyuklia kati ya Ufaransa, Ujerumani, Uingereza na Iran yako katika kipindi muhimu. Kama Marekani haiungi mkono juhudi za Umoja wa Ulaya, Umoja wa Ulaya hautaamini udhati wa Marekani wa kuboresha uhusiano kati yao baada ya vita vya Iraq. Hivi sasa Marekani inahitaji uungaji mkono wa Umoja wa Ulaya katika masuala mengi ya kimataifa, hivyo lazima ichukue hatua halisi kuboresha uhusiano kati yake na Ulaya. Ingawa Marekani haina matumaini makubwa kuhusu kutatua suala la nyuklia la Iran kwa njia ya mazungumzo, lakini kama haiungi mkono juhudi za Umoja wa Ulaya hivi sasa, basi mazungumzo hayo yakishindwa baadaye, Marekani itafanyaje ikitaka Umoja wa Ulaya kuiunga mkono na kuliwasilisha suala hilo kwenye baraza la usalama la Umoja wa Mataifa?
Pili, Iran ni nchi inayozalisha mafuta mengi. Akiba yake ya mafuta na mauzo ya mafuta katika nchi za nje inachukua nafasi ya pili duniani. Iran ilisema kwa mara nyingi kuwa, kama suala la nyuklia la Iran likiwasilishwa kwenye baraza la usalama la Umoja wa Mataifa, hali ya usalama wa Mashariki ya Kati na utoaji wa mafuta duniani vitakabiliwa na matatizo makubwa. Hivi sasa bei ya mafuta duniani bado ni kubwa, Marekani ikiihimiza jumuiya ya kimataifa iiadhibu Iran, haitapata faida nyingi.
Mwisho, kutokana na msimamo wa Iran katika miaka miwili iliyopita, Marekani imetambua kuwa Iran imeamua kulinda haki yake ya kutumia nishati ya nyuklia kwa amani kwa mujibu wa makubaliano ya kutoeneza silaha za nyuklia. Marekani ilichukua msimamo mgumu kwa Iran katika muda mrefu uliopita, lakini haikutimiza lengo lake. Hii si kama tu ilipunguza sifa yake ya kidiplomasia katika suala la kuzuia kueneza kwa silaha za nyuklia, bali pia ilizuia mpango wake wa "mageuzi ya kidemokrasia" katika Mashariki ya Kati. Lakini Marekani inaelewa vizuri matumizi ya ujanja wa ukali na upole. Katika wakati mwafaka, upole utaleta matokeo mazuri zaidi kuliko ukali.
Maoni ya raia wa Ulaya yanaona kuwa, kutokana na sababu hizo, Marekani inaziunga mkono juhudi za Umoja na Ulaya, na kutopinga tena kuanzisha mchakato wa Iran kushiriki kwenye Shirika la Biashara Duniani.
Idhaa ya Kiswahili 2005-05-27
|