Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-05-27 14:56:59    
Umoja wa Afrika waomba misaada ya fedha na vitu kwa ajili ya utekelezaji wa kusimamisha vita huko Darfur

cri

Mkutano wa siku moja wa Umoja wa Afrika ulifanyika huko Addis Ababa tarehe 26. Huu ni mkutano wa kutafuta misaada ya fedha na vitu kwa ajili ya vikosi vya Umoja huo kusimamia utekelezaji wa mkataba wa kusimamisha vita katika sehemu ya Darfur.

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bw. Kofi Annan alihudhuria mkutano huo, kwenye hotuba yake Bw. Kofi Annan alisema kuwa vikosi vya Umoja wa Afrika ni muhimu sana kwa ajili ya kusimamisha vita katika sehemu ya Darfur kutokana na kuwa hali ya Darfur inazidi kuwa mbaya siku hadi siku, wakazi na wasaidizi wa nchi za nje hawana uhakika wa usalama. Bw. Kofi Annan aliomba nchi wafadhili ziendelee kuchangia fedha ili kuhakikisha vikosi hivyo vinafanya kazi bila tatizo na kumaliza mapema hali ya wasiwasi huko Darfur.

Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika Bw. Konare kwenye mkutano alitangaza kuwa, pande mbili za serikali ya Sudan na vikosi vya upinzani zitarudisha mazungumzo ya amani tarehe 10 Juni huko Abuja, mji mkuu wa Nigeria. Bw. Konare alisema, Umoja wa Afrika unazingatia kuongeza idadi ya wachunguzi na askari wake huko Darfur, anatumai jumuyia ya kimataifa ijitahidi kutoa misaada ya watu, fedha na vitu ili kuhakikisha vikosi vyake vinalinda amani bila tatizo.

Hivi sasa Umoja wa Afrika una wachunguzi na askari jumla ya 2300 wakisimamia mkataba wa kusimamisha vita kati ya serikali ya Sudan na vikosi vya upinzani unatekelezwa. Kutokana na kuwa hali ya huko Darfur inazidi kuwa mbaya siku hadi siku Umoja huo umeamua kuongeza wachunguzi na askari hadi 7700 kabla ya mwishoni mwa mwezi Septemba na mwakani utaongeza hadi 12,000. Kwa makadirio, mpango huo unahitaji dola za Kimarekani milioni 723, laniki sasa bado kuna pengo la dola za Kimarekani milioni 350, na mpango huo pia unahitaji silaha nyingi na vitu vya maisha.

Kabla ya mkutano huo, Umoja wa Ulaya na NATO iliwahi kuonesha nia yao ya kutoa misaada kwa ajili ya shughuli za kusimamisha vita. Mjumbe mwandamizi anayeshughulikia mambo ya nje na usalama wa Umoja wa Ulaya Bw. Solana tarehe 23 mwezi huu huko Brussels alisema, Umoja wa Ulaya utatoa misaada ya huduma za maisha, uchukuzi. NATO tarehe 24 iliamua kutoa misaada ya ndege ya uchukuzi, na kuwaandaa watu wakiwemo wachambuzi wa habari.

Kwenye mkutano huo wa tarehe 26 nchi za Umoja wa Ulaya na Nato zilitoa ahadi kuwa zitatoa msaada wa dola za Kimarekani milioni 200, kati ya fedha hizo Marekani itatoa dola milioni 50, Uingereza dola milioni 12, na zilizobaki zitatolewa na Ufaransa, Ujerumani na Canada.

Licha ya msaada wa fedha, Umoja wa Ulaya na NATO pia ziliahidi kutoa msaada wa huduma za maisha. Katibu mkuu wa NATO aliyehudhuria mkutano huo Bw. Scheffer alisema, Nato tayari imeweka ratiba ya kupeleka msaada wake huku Bw. Scheffer alikana usemi usemao jeshi la NATO litashiriki moja kwa moja kwenye shughuli za kusimamisha vita huko Dafur.

Mgogoro wa huko Darfur, magharibi mwa Sudan, ulianza mwezi Februari mwaka 2003, hadi sasa mgogoro huo umesababisha vifo vya watu laki moja na elfu 80 na watu zaidi ya milioni mbili kupoteza makazi. Kutokana na usuluhishi wa jumuyia ya kimataifa serikali ya Sudan na vikozi vya upinzani viliwahi kufanya mazungumzo mara nyingi lakini hayakupata matokeo yoyote ya kukomesha vita.

Idhaa ya kiswahili 2005-05-27