Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-05-27 16:11:15    
China yasaidia kuboresha hali ya uzalishaji mali na maisha ya kina mama wa sehemu ya magharibi ya China

cri

Tarehe 24 mwezi Mei, China ilianzisha harakati ya "kutoa upendo", ambayo inawahimiza watu wa fani mbalimbali kusaidia kuboresha hali ya uzalishaji mali na maisha ya kina mama na familia zao wa sehemu ya magharibi, iliyokumbwa na ukame kwa njia ya kujenga mashimo ya maji. Harakati hiyo ni mwendelezo wa harakati ya "shimo la maji la mama" iliyoanzishwa mwaka 2000.

Kutokana na sababu za kimaumbile na kihistoria, baadhi ya sehemu za magharibi za China zina upungufu mkubwa wa maji, wastani wa matumizi ya maji kwa kila mtu ni mita za ujazo 110 tu kwa mwaka, ukiwa unachukua asilimia 3.7 tu ya ule wa duniani. Wakazi na wanyama wa huko wanategemea sana maji ya mvua yaliyokingwa, na kina mama wanapaswa kuchukua jukumu kubwa zaidi la kimaisha kuliko wanawake wengine wanaoishi katika mazingira ya kawaida. Harakati ya "shimo la maji la mama" iliyotekelezwa na shirika la maendeleo ya wanawake la China, ni kuchangisha fedha kutoka kwa jamii kusaidia kujenga mashimo ya maji kwa saruji ili kuwawezesha kina mama hao kukinga mvua kwa ufanisi zaidi, na kutatua kimsingi tatizo la maji ya matumizi ya kila siku.

Katika miaka mitano iliyopita, harakati ya "shimo la maji la mama" imepata mafanikio mazuri. Bi. Wen Xiaorong ni mwanamke wa kawaida kutoka sehemu ya mlimani yenye ukame ya mkoa wa Sichuan, kusini magharibi mwa China, alimwambia mwandishi wetu wa habari kuwa, sasa familia zote zimefikishiwa maji ya bomba, wanavijiji wote wazee kwa watoto wamefurahishwa sana na harakati hiyo. Zamani wanavijiji hawakuthubutu kufuga nguruwe zaidi ya wawili kutokana na ukosefu wa maji, hivi sasa wanaweza kufuga nguruwe wengi wapendavyo ili kujipatia pato la nyongeza.

Takwimu zinaonesha kuwa, ilipofika mwishoni mwa mwaka 2004, harakati ya "shimo la maji la mama" kwa jumla iligharimu Yuan milioni 250 na kujenga mashimo ya maji elfu 90 na miradi zaidi ya 110 ya maji ambayo inawanufaisha watu milioni moja wa wilaya au miji 22. Harakati hiyo imeboresha hali ya afya na imeinua kiwango cha maisha ya kina mama walionufaika.

Harakati ya "kutoa upendo" iliyoanzishwa hivi karibuni, inalenga kuwasaidia kina mama wengi zaidi wa sehemu ya magharibi inayokumbwa na ukosefu wa maji. Naibu katibu mkuu wa mfuko wa maendeleo ya wanawake wa China Bwana Qin Guoyin alisema:

"Kama tulivyofanya zamani, tunawahimiza watu wenye uwezo kuchanga Yuan 1000 kujenga shimo moja la maji, ili kuisaidia familia moja kutatua tatizo la maji. China ina eneo kubwa linalokumbwa na ukosefu wa maji, hivyo tutaendelea kusukuma mbele harakati hiyo katika miaka kadhaa ijayo."

Bi. Qin alifahamisha kuwa, harakati ya "kutoa upendo" pia itawasaidia wanawake wenye matatizo ya kiuchumi wa sehemu ya magharibi kupanda miti, kufuga mifugo, kupanua uzalishaji wa kilimo ili kuongeza mapato yao. Harakati hiyo inafuatiliwa sana na jamii, katika siku ya ufunguzi, harakati hiyo ilipokea mchango wa Yuan milioni 10 kutoka kwa makampuni ya China. Wachezaji wengi wa filamu na vipindi vya televisheni pia walieleza kuwa, watachangia fedha kuwasaidia kina mama na familia zao kuondokana na umaskini.

Idhaa ya kiswahili 2005-05-27