Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-05-31 15:53:13    
Msikilizaji wetu Telly Wambwa aliyekuwa Beijing, China

cri

      Msikilizaji wetu Xavier Telly Wambwa aliyepata ushindi katika shindano la chemsha bongo kuhusu ujuzi wa China mpya, alialikwa kuja Beijing, ambapo alikuwa mgeni wa Radio China kimataifa. Alipokuwa China alipata fursa ya kutembelea sehemu mbalimbali hapa Beijing, na kwenda mjini Xian kutembela maonesho ya sanamu za askari na farasi wa mfalme wa zamani Qinshihuang, tarehe 26 aliondoka Beijing na kurudi nyumbani Kenya. Kabla ya kuondoka kwake tulizungumza naye na alitueleza jinsi alivyoiona safari yake ya hapa Beijing.

Mwandishi: Kwanza napenda nikupe fursa hii uwaambie wasikilizaji wetu kuwa mpaka sasa umepata picha gani ya China?

Wambwa: Tangu siku nilipofika mjini Beijing, kusema kweli Nimekuwa katika hali ya mshangao kila sehemu nilipokwenda. Mjini Beijing yamejengwa majengo marefu ya kuchomoza na ya kupendeza kabisa. Mgeni unapotembea wakati wa usiku ama mchana utajikuta hujui ulipo, lakini jambo kubwa ni kwamba nikilinganisha mji wa Nairobi na mji wa Beijing, Nairobi bado ni mji mdogo, naona maendeleo ya China yamekuwa ni ya manufaa sana kwa maendeleo yaBeijing.

Mwandishi: Hivi karibuni, umerudi Beijing kutoka kwenye mji wa Xian ambao naweza kusema ni mji wa kale wa China, unaweza kutuelezea nini ambayo umeona mjini Xian?

Wambwa: Ah, kabla sijaeleza jambo lolote kuhusu mji wa Xian, nataka kulinganisha mji huo na mji wa Bungoma. Bungoma ni mdogo sana kabisa, lakini Xian umejengwa kama mji wa Beijing. Nilipofika huko, nilipozuru katika sehemu mbalimbali za mji huo unaojulikana kama ni mji wa historia ambao umehifadhi shughuli nyingi za kila sehemu kwa upande wa utamaduni, kilimo na uchumi. Niliweza kutembelea sehemu moja ya sanamu za askari na farasi wa mfalme Qinshihuang, ambapo ni sehemu inayohifadhiwa na UNESCO. Kwa jinsi nilivyozoiona Sanamu hizo za askari na farasi, niliweza kufahamu jinsi walivyokuwa, ni kitu cha maajabu sana, nilishangaa sana kuona vile walivyopangwa, na vile walivyoumbwa, nashindwa hata kuteleza kwa jinsi nilivyoona, lakini ni kitu cha maajabu sana. Kwa sababu nilipokuwa mahali pale, kwa jinsi walivyo wengi sikuweza hata kuona vizuri, kwani hata watalii kutoka sehemu mbalimbali nchini China walikuwa wamejaa sana.

Mwandishi: Leo tuliambatana na wewe kwenda ubalozi wa Kenya nchini China, unaweza kuwaelezea wasikilizaji wetu hali ya matembezi hayo?

Wambwa: Siku ya leo, nimepata fursa ya kutembelea ubalozi wa Kenya nchini China. Niliona kwamba ni vizuri kabla ya sijarudi nyumbani niweze kukutana na balozi wa Kenya nchini China. Nina furaha kuwaelezea wasikilizaji wenzangu pamoja na wananchi wenzangu kutoka Kenya na Afrika kwa ujumla kwamba ni fursa kubwa niliweza kupata. Nilipoingia katika ofisi ya ubalozi wa Kenya nchini China, niliweza kumkuta balozi Bibi Ruth Sereti Solitei pamoja na ofisa Fred Ondieki ambao waliweza kunikaribisha kwa furaha, tuliweza kujadiliana mambo kadha wa kadha hasa kuhusu namna nilivyopata mwaliko wa kuja China kwa matembezi. Nilipowaelezea walikuwa na furaha kubwa, waliona kuwa uhusiano kati ya Kenya na China ni mzuri, tunastahili tuzidi kushirikiana katika siku zijazo ili kuendeleza ushirikiano wetu. Waliweza kunielezea furaha yao kuhusu jambo hilo, nami pia nashukuru sana. Kusema kweli sio jambo la rahisi kama vile watu wanavyodhani kwamba kwenda sehemu fulani kutokana na mwaliko ni jambo rahisi.

Mwandishi: Kitu kingine ningependa kujua, wewe labda ni mmoja kati ya wasikilizaji wachache ambao wamepata fursa ya kufika kwenye studio yetu na ofisi yetu, na unaona utendaji wetu wa kazi jinsi ulivyo? Sasa kwa wasikilizaji hao ambao hawafahamu ofisi yetu na studio yetu unaweza ukawaambia vipi jinsi kazi zetu zinavyoendelea?

Wambwa: Kwanza kabisa, hivi sasa ni mara ya pili naongea nikiwa katika studio ya CRI. Studio hii imepambwa vilivyo, kuna mashine ambazo sikuwahi kuziona, lakini hivi sasa nina fursa, hata nilivyoongea hivi ninaongea kwa kutumia mashine yenye nguvu. Pia nimepata fursa ya kutembelea ofisi ya idhaa ya kiswahili ya CRI, niliweza kukutana na wafanyakazi wa idhaa ya kiswahili ya CRI, ambao hao ni wakarimu na wamenikaribisha vizuri kwenye ofisi yao. Lakini kulingana na vile nilivyoona katika ofisi yao, sisi wasikilizaji tunapaswa kuelewa wafanyakazi hao ni watu ambao wanajitahidi vilivyo, sio kwamba wamejitosheleza kwa kila hali, lakini wanajitahidi kuhakikisha kwamba sisi wasikilizaji tukapata matangazo kwa wakati unaofaa. Kwa hiyo baadhi ya malalamiko tunatoa bila kujua hali halisi ya ofisi. Hata pia kuna sehemu fulani ambazo nimeweza kuitembelea leo asubuhi kila idara ya CRI na kuona sehemu ambazo barua pamoja na zawadi ambazo CRI ilitumwa kutoka kwa wasikilizaji wake wa sehemu mbalimbali duniani.

Mwandishi: Ungependa kuwaambia nini watu wanaosikiliza kipindi hiki huko Bungoma kuhusu safari yako kwa ujumla hapa China?

Wambwa: Kusema kweli ninayo furaha kubwa ya kuwaelezea kwamba China ni nchi ambayo imeendelea, na watu wa China ni watu wenye umoja, ni wakarimu sana, hawajali kwamba huyu ni mwafrika, au huyu ni mzungu, mwarabu ama huyu ni nani, hasa kama vile sisi wasikilizaji washindi tulipokuwa hapa, tunatoka sehemu mbalimbali duniani, lakini tulichukuliwa kama kitu kimoja, jambo ambalo ningeweza kuwaelezea wasikilizaji wenzangu pamoja na wananchi wote wa Kenya ni kwamba na sisi tuwe kitu kimoja. Na sisi wasikilizaji tukiwa na umoja, natumai kwamba Radio China kimataifa itasonga mbele kwa urahisi zaidi.

Idhaa ya kiswahili 2005-05-31