Watoto duniani wanapozama katika furaha ya sikukuu yao duniani, mtoto wa kike Sushan mwenye umri wa miaka minane, kama kawaida yake anakaa kando ya dampo akinyoosha mikono midogo akiomba msaada. Huyo ni mmoja tu kati ya watoto wa mitaani elfu 30 mjini Nairobi.
Kutokana na Ukimwi, vurugu za vita na umaskini, barani Afrika watoto kama Sushan ni wengi. Inaripotiwa kuwa kuna watoto elfu 10 wa mitaani nchini Afrika Kusini, nchini Jamhuri ya Demokrasi ya Congo elfu 15 mjini Kinshasa, na katika mji mkuu wa Ethiopia, Addis Ababa, watoto kama hao wanafurika mjini.
Mtoto wa kiume mrefu aliyesimama pembeni mwa Sushan alimwambia mwandishi wetu, kwamba wazazi wa Sushan wamekuwa kitandani kutokana na kuwa na Ukimwi, na yeye wazazi wake wamekufa zamani kutokana na ugonjwa huo. Kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa, katika sehemu ya kusini mwa Sahara miongoni mwa watoto yatima milioni 34, milioni 12 ni watoto yatima kutokana na wazazi wao kufariki kwa Ukimwi. Ili kutafuta maisha watoto hao wamekuwa ombaomba na hata kushughulika na kazi nzito na za hatari, afya yao na maisha yao yako hatarini. Ripoti kutoka Shirika la Watoto la Umoja wa Mataifa inakadiria kuwa hadi kufikia mwaka 2010 watoto yatima barani Afrika watafikia milioni 20.
Katika nchi zilizokumbwa na vita watoto yatima ni wengi zaidi. Katika nchi za Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, Sudan, Liberia, Angola, Rwanda, Burundi na Uganda, kutokana na vita vya miaka miongo kadhaa watoto wengi wamepoteza familia zao. Mjini Luanda, mji mkuu wa Angola, kuna watoto yatima elfu kumi wanaolala barabarani.
Maisha ya barabarani ni maisha ya namna gani? Mwombaji Nansi, mwenzake Sushan alisema, kwa kawaida kila siku anaweza kupata Shilingi 50 za Kenya (kiasi cha senti 60 za dola ya Marekani), na kwa bahati anaweza kupata Shilingi mia moja ambayo inaweza tu kushibisha tumbo lake. Njaa iliwalazimisha kuishi kwa kuiba, na watoto wengine wenzake wa kike walijitosa kwenye ukahaba, na baadhi ya watoto wametumbukia katika matumizi ya dawa za kulevya.
Licha ya watoto wa mitaani, tatizo la kuwaajiri watoto pia ni kubwa. Ripoti ya Shirika la Kazi Duniani inasema kwamba barani Afrika kuna wafanyakazi wenye umri wa miaka kati ya mitano hadi 14 kiasi cha milioni 80, na kwa makadirio hadi kufikia mwaka 2015 wafanyakazi hao watafikia milioni 100. Watoto hao wanalipwa kidogo sana, wanalemewa na kazi nzito na kuteswa vibaya.
Kitu kinachotisha zaidi ni kuwa miongoni mwa watoto wa skauti laki tatu duniani, laki 1.2 ni watoto wa Afrika. Kazi ya maskauti ni pamoja na kushiriki kwenye vita au kazi zinazohusika na vita kama upelelezi, kuondoa mabomu ya kutegwa ardhini na kulinda doria katika vituo. Na watoto wa kike wanalazimishwa kuwahudumia kijinsia askari watu wazima. Maskauti hao wameharibika vibaya kiafya na kimawazo kutokana na kuona mapema mauaji, mateso na unyanyasaji wa kijinsia, na kusababisha matumizi ya dawa za kulevya, ulevi na hata kuwatesa wanafamilia wao.
Tatizo la watoto wa Afrika limekuwa kama bomu la kulipuka wakati maalumu, lakini jambo linalofajiri ni kuwa baadhi ya nchi za Afrika zimeanza kuchukua hatua kukabiliana na tatizo hilo la kijamii.
Katika miaka ya karibuni, Kenya imefanya juhudi nyingi zikiwa ni pamoja na kutunga sheria ya kulinda haki za watoto, kuwaondolea ada ya shule ya msingi na kurekebisha sheria ya kazi. Mwezi Aprili Wizara ya Kazi ya Kenya imeorodhesha kazi zisizofaa kwa watoto wenye umri kati ya miaka 5 hadi 14 ili kuhakikisha watoto wanapata haki ya elimu na kukua kwa afya.
Lakini kazi ya kuwasaidia na kuwalinda haki za watoto hao sio kazi ya muda mfupi tu. Giza lilianza kugubika mji wa Nairobi, Sushan, na Nansi pamoja na watoto wenzao walio karibu na dampo walimwambia mwandishi, "Hatukuwahi kufikiria kama kuna siku ya watoto duniani, kitu tunachotaka ni upendo wa familia."
Idhaa ya kiswahili 2005-06-01
|