Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-06-01 15:59:28    
Bado kuna njia ndefu hadi kufikia lengo la kutokomeza uvutaji wa tumbaku duniani

cri
    Kukomesha uvutaji wa tumbaku bila shaka ni mwelekeo duniani, lakini utekelezaji wa lengo hilo unatokana na pande tatu za usimamizi wa serikali, wafanyabiashara wa tumbaku wabadilishe shughuli za uzalishaji na wavutaji wa tumbaku wajizuie.

    Takwimu mpya za Shirika la Afya Duniani zinaonesha kuwa uvutaji tumbaku umekuwa mwuuaji wa pili duniani ukifuata ugonjwa wa shinikizo la damu. Hivi sasa duniani kuna wavutaji wa tumbaku bilioni 1.3, wakati idadi ya wavutaji tumbaku imechukua 20% kati ya jumla ya idadi ya watoto wenye umri wa miaka ya kutoka 13 hadi 15, na kila mwaka kuna idadi ya watu milioni 5 wanaofariki dunia kutokana na maradhi yanayohusika na uvutaji wa tumbaku.

    Kutokana na kukabiliwa na hali ngumu ya namna hiyo, dunia inafanya usimamizi mkali dhidi ya uzalishaji wa tumbaku na sigara. "Mkataba wa kanuni za udhibiti wa uzalishaji wa tumbaku" umeanza kufanya kazi rasmi toka tarehe 27 mwezi Februali mwaka huu. Nchi zilizosaini mkataba huo zinapaswa kuchukua hatua zifuatazo: Kuinua bei na kodi za sigara; Kupiga marufuku kutoa matangazo kuhusu sigara; Kupiga marufuku shughuli za udhamini za wafanyabiashara wa sigara; kupambana na biashara ya magendo ya sigara; kupiga marufuku kuwauzia sigara watoto, kuweka onyo kwenye paketi za sigara kuwa "Uvutaji sigara unadhuru afya" na kuchukua hatua kuzuia watu wasivute tumbaku kwenye sehemu za umma.

    Wafanyabiashara wa sigara kubadilisha mtindo wa uzalishaji imekuwa mwelekeo duniani. Ili kulinda maslahi yao, baadhi ya kampuni za sigara za Ulaya na Marekani zilitenda vitendo visivyo vya busara na kudidimia kwenye kiwango cha chini kabisa cha maadili ya uchumi wa soko huria. Kwa kukabidhiwa na Shirika la Afya Duniani, kundi la uchunguzi la wataalamu lililoongozwa na mwanasayansi wa Uswisi Bw. Tomas Tsrtener lilitoa taarifa yenye kurasa 248 mwishoni mwa karne iliyopita. Taarifa hiyo ilisema, "nyaraka za kampuni za sigara zinasema kuwa kampuni za sigara zimelichukulia Shirika la Afya Duniani kuwa mmoja wa adui yao mkubwa. Yameingiza watu wao kwenye Shirika la Afya Duniani, aidha yanapata habari kuhusu shughuli za Shirika la Afya Duniani kwa kutumia mashirika mengine ya Umoja wa Mataifa. Kuna sababu ya kuamini kuwa uharibifu wa kampuni hizo za sigara umefikia kiwango cha kushangaza watu."

    Baada ya kupewa adhabu kutokana na vitendo vyao visivyo halali, kampuni za sigara za Ulaya na Marekani zililazimika kusetiri uhusiano kati yao na uzalishaji wa sigara. Kampuni ya sigara ya Philip Moris ambayo ni ya kwanza kwa ukubwa nchini Marekani, ilibadilisha jina la kampuni kuwa kampuni ya Altria. Lakini shirika la kupinga uzalishaji wa sigara lilisema, "jina la Altria haliwezi kufunika ukweli wa kukithiri kwa sigara ya Marlboro duniani, ambayo inatakiwa kusimamisha uzalishaji wake haraka iwezekanavyo hata kama imebadilisha jina lake la zamani na kutumia jina gani lingine."

    Wavutaji sigara kujizuia na kuacha uvutaji sigara pia ni hatua moja muhimu katika shughuli za kukomesha uvutaji sigara duniani. Mratibu mkuu wa Shirika la Afya Duniani Bw. Lee Jong wook alisema, "Licha ya kudhuru afya ya mvutaji sigara yeye mwenyewe, uvutaji sigara pia unaathiri afya ya watu wengine. Kutokana na mtazamo huo, kuvuta sigara katika mahali pa umma ni suala linalohusu maadili na uungwana wa binadamu."

    Ingawa kudhibiti uvutaji sigara kumekuwa maoni ya watu karibu wote duniani, lakini matumizi ya sigara yalianzia zamani sana, hivyo ni vigumu kutokomezwa duniani kuanzia kesho. Sababu zake ni kama ifuatavyo: Kwanza, uzalishaji wa tumbaku na sigara unaleta pato kubwa la kodi; Pili, sekta ya uzalishaji wa tumbaku na sigara inaleta nafasi nyingi za ajira na Tatu, hivi sasa kuna idadi kubwa ya watu wanaovuta sigara. Hivyo bado kuna njia ndefu hadi kufikia lengo la kutokomeza uvutaji wa sigara duniani.

Idhaa ya Kiswahili