Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-06-01 19:08:41    
China yaongeza nguvu ya kusaidia maendeleo ya makabila madogo madogo yenye watu wachache

cri

Ili kuongeza zaidi nguvu ya kuyasaidia makabila madogo madogo yenye watu wachache, serikali ya China hivi karibuni imetoa mpango wa miaka mitano wa kutatua kihalisi matatizo makubwa yaliyoko katika maendeleo ya makabila madogo madogo yenye watu wachache, ili kuyawezesha maendeleo ya uchumi na jamii ya makabila hayo yafikie kiwango cha kati au juu ya kiwango cha kati.

China ni nchi yenye makabila mengi ya muungano, mbali na kabila la wahan, pia kuna makabila 55 madogo madogo. Miongoni mwa makabila hayo madogo madogo, kuna makabila 22 yenye idadi ya watu chini ya laki moja, watu wa makabila hayo wengi kabisa wanaishi katika sehemu za milimani za mbali au sehemu zilizoko kando ya mipaka.

Tokea sera ya mageuzi na ufunguaji mlango ianze kutekelezwa nchini China mwishoni mwa miaka ya 70 ya karne ya 20, makabila madogo madogo yenye watu wachache yamepata maendeleo ya haraka kiasi, hali ya maisha ya watu wa makabila hayo imeboreshwa kidhahiri. Lakini kutokana na sababu za kihistoria na kimaumbile, hivi sasa kiwango cha jumla cha maendeleo ya uchumi na jamii ya makabila hayo madogo madogo yenye watu wachache bado kiko nyuma sana, na suala la umaskini bado linaonekana dhahiri. Katika hali hiyo, China imetoa "Mpango wa mwaka 2005 hadi 2010 wa kusaidia maendeleo ya makabila madogo madogo yenye watu wachache", ambao unaeleza hatua halisi za kuyasaidia makabila madogo madogo yenye watu wachache kujiendeleza kwa haraka.

Naibu mkurugenzi wa Idara ya maendeleo ya uchumi katika Kamati ya mambo ya makabila madogo madogo ya China Bwana Yue Zhanghong akimwambia mwandishi wa habari alisema:

Hivi sasa baadhi ya makabila madogo madogo yenye watu wachache bado yana hali duni katika uzalishaji mali na maisha yao, hata baadhi ya sehemu hazina hali ya kimsingi ya kimaisha, kwa mfano sehemu nyingi wanakoishi watu makabila hayo hakuna barabara, vijijini hakuna umeme, na suala la lishe la asilimia 20 ya watu wa sehemu hizo bado halijatatuliwa.

Katika miaka ya hivi karibuni, ili kuyasaidia makabila madogo madogo yenye watu wachache kujiendeleza, China imechukua hatua kadha wa kadha, kwa mfano katika miaka mitatu iliyopita, serikali ilitenga fedha zaidi ya yuan milioni 110 katika kuboresha hali ya miundo mbinu ya maji, umeme na barabarani katika vijiji vya sehemu wanakoishi watu wa makabila madogo madogo yenye watu wachache, na kuendeleza mambo ya elimu, afya na utamaduni ya sehemu hizo.

Mpango uliotolewa hivi karibuni na serikali ya China umeainisha kuwa serikali itachukua hatua mbalimbali za kuharakisha maendeleo ya makabila madogo madogo yenye watu wachache.

Bwana Yue Changhong alisema:

Tunatumai kutumia muda wa miaka mitano kutatua kihalisi matatizo yanayoyakabili makabila madogo madogo yenye watu wachache katika sekta za uchumi, jamii, utamaduni, elimu na afya, na kuyasaidia makabila hayo yafikie kiwango cha kati au juu ya kati cha maendeleo ya uchumi na jamii, na kuwasaidia watu wa makabila hayo wajiendeleze na kufuata njia ya kujitajirisha.

Hivi sasa idara husika za China zinafanya utafiti na kutunga mpango husika na hatua halisi ili zitekelezwe mapema iwezekanavyo.

Idhaa ya Kiswahili 2005-06-01