Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-06-01 20:49:03    
China yazingatia zaidi mahitaji ya watu katika usimamizi wa vyuo vikuu

cri

Hivi sasa, China ina vyuo vikuu karibu 2000, na idadi ya wanafunzi wa vyuo vikuu imezidi laki 1.3. Ili kuhakikisha wanafunzi hao wanakua kwa afya, hivi karibuni, wizara ya elimu ya China ilitoa kanuni mpya za usimamizi wa wanafunzi wa vyuo vikuu na kuamua zianze kutekelezwa kuanzia muhula mpya utakaoanza tarehe 1 mwezi Septemba mwaka huu.

Katika miaka zaidi ya 10 iliyopita, uchumi na jamii ya China vimeendelea kwa kasi, na mabadiliko makubwa yametokea nchini China. Hali hiyo imeathiri sana mtizamo na mfumo wa elimu ya juu. Aidha, kutokana na kuwa wanafunzi wa vyuo vikuu wa hivi sasa wote walizaliwa baada ya China kuanza kutekeleza sera ya mageuzi na ufunguaji mlango, hivyo mtizamo wao ni wa wazi zaidi kuliko wanafunzi wa zamani. Lakini kanuni za usimamizi wa wanafunzi wa vyuo vikuu zinazotekelezwa hivi sasa zilitungwa kabla ya miaka 15 iliyopita, kanuni zake nyingi zimekuwa haziendani na hali halisi ya hivi sasa.

Ili zilingane na umaalum wa wanafunzi wa hivi sasa, kanuni hizo zimerekebishwa sana, ili ziweze kulinda haki na maslahi halali ya wanafunzi. Mkuu wa idara ya wanafunzi katika wizara ya elimu ya China Bi. Lin Huiqing alieleza:

"katika kanuni hizo mpya, vigezo na utaratibu wa kuwaadhibu wanafunzi waliokiuka kanuni hizo vimekuwa dhahiri zaidi, pia kanuni hizo zimeongeza haki za wanafunzi kujitetea, na ni muhimu katika kulinda haki halali za wanafunzi."

Bi. Lin Huiqing alisema kuwa, zamani, vyuo vikuu vilipowaadhibu wanafunzi waliokiuka kanuni, vigezo na utaratibu vilikuwa ni tofauti na havikulingana. wanafunzi hawakuwa na haki ya kujitetea. hali hiyo iliathiri maslahi ya wanafunzi. Lakini kanuni mpya zimeondoa tatizo hilo. Kabla ya kutoa uamuzi wa adhabu, vyuo vikuu ni lazima visikilize maoni ya wanafunzi au mawakala wao; vyuo vikuu vikiwaadhibu wanafunzi, lazima vifuate utaratibu sahihi, kuwa na ushahidi wa kutosha, na kutoa adhabu zinazostahili. Kanuni hizo zimeweka mipaka kwa haki ya vyuo vikuu kuwaadhibu wanafunzi.

Mwanafunzi wa shahada ya pili wa chuo kikuu cha siasa na sheria cha China Bw. Li Bing alisifu sana vifungu hivyo katika kanuni hizo mpya. alisema:

"adhabu wanazopewa wanafunzi kwenye vyuo vikuu zinaathiri maisha yao katika siku za baadaye, hivyo ninaunga mkono kuwapa wanafunzi haki za kujitetea."

Vifungu kuhusu wanafunzi wa vyuo vikuu kufunga ndoa pia vimefuatiliwa sana na watu wa jamii hivi karibuni. Kanuni za zamani zilisema wazi kuwa, wanafunzi wa vyuo vikuu hawaruhusiwi kufunga ndoa. Lakini baadhi ya vyuo vikuu vilichukua hatua zenye unyumbufu zaidi na kuwaruhusu wanafunzi wa shahada ya pili wenye umri mkubwa kufunga ndoa. Kanuni mpya zimeacha vifungu hivyo. Kuhusu marekebisho hayo, mwanafunzi wa shahadi ya kwanza wa chuo kikuu cha Qinghua Bi. Wang Lingjing alisema:

"hivi sasa, miundo ya wanafunzi katika vyuo vikuu vya China imebadilika sana, hivyo, sera hiyo mpya imezingatia maslahi ya wanafunzi na kuwapa haki ya kujiamulia. Kutokana na hali ya hivi sasa, wanafunzi wanaonekana kuwa na moyo tulivu kuhusu marekebisho hayo."

Bi. Wang Lingjing mwenye umri wa miaka 21 alisema kuwa, ingawa ana mchumba wake, na wametimiza umri wa kisheria wa kufunga ndoa, lakini anaona bado ni mapema kufunga ndoa, na anataka kutumia muda huo mzuri katika masomo. Baadhi ya wanafunzi walipohojiwa walisema kuwa, wanafunzi wa shahada ya kwanza bado hawajapevuka kiakili, wala hawajaanza kujitegemea kiuchumi, hivyo hawawezi kufunga ndoa. Lakini kwa wanafunzi wa shahada ya pili wana umri mkubwa na uwezo mkubwa zaidi, hivyo kama wakitaka, wanaweza kufunga ndoa.

Aidha, kanuni hizo mpya pia zimevikabidhi vyuo vikuu haki kubwa zaidi ya kujiamulia kuhusu shughuli za masomo. Kama vile, zimerahisisha utaratibu wa wanafunzi kubadilisha michepuo, na kuondoa kanuni kuhusu wanafunzi kuachishwa shule na kuwafanya warudie darasa. Katika siku za baadaye, vyuo vikuu vitaweza kujiamulia kuhusu shughuli hizo kutokana na hali halisi ya vyuo hivyo.

Wakati wa kusistiza usimamizi kwa kuzingatia mahitaji ya watu, na kuongeza haki ya kujiamulia ya vyuo vikuu, kanuni hizo mpya pia zimeweka kanuni kali katika baadhi ya mambo. Kama vile, zimeongeza kanuni kuhusu kuwafukuza shule wanafunzi waliodanganya kwenye mitihani, au kuiba matokeo ya utafiti wa wanafunzi wengine. Mwalimu wa Chuo kikuu cha Beijing Bw. Zhang Shaolin aliona:

"katika miaka ya hivi karibuni, hali ya wanafunzi kudanganya kwenye mitihani imekuwa mbaya sana, kama tukipuuza hali hiyo, inaweza kupunguza sifa ya shahada za chuo kikuu. Hivyo naona ni lazima zichukuliwe hatua kali kuwaadhibu wanaofanya vitendo hivyo."

Wanafunzi na walimu wa vyuo vikuu waliohojiwa wote waliona kuwa, baada ya kuanza kutekelezwa, kanuni hizo mpya zitazidi kusukuma mbele maendeleo ya elimu ya juu ya China.

Idhaa ya Kiswahili 2005-06-01