Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-06-02 16:24:27    
Mtu aliyeshuhudia mauaji makubwa ya Nanjing

cri

Tarehe 13 Desemba mwaka 1937, wanajeshi laki mbili wa Japan waliushambulia na kuukalia mji wa Nanjing, ambao wakati ule ulikuwa ni mji mkuu, na kufanya mauaji makubwa dhidi ya wakazi wa Nanjing wasiokuwa na hatia yoyote na askari wa China waliosalimisha silaha. Katika muda wa wiki sita, wanajeshi wa Japan waliwaua wachina zaidi ya laki tatu, miongoni mwao, elfu 90 walikuwa ni mateka wa kivita. Mauaji makubwa ya Nanjing yalikuwa moja ya matukio makubwa yaliyojulikana duniani katika vita kuu ya pili.

Bi. Xia Shuqin mwenye umri wa miaka 77 mwaka huu ni mmoja kati ya watu wachache walionusurika katika mauaji hayo. Alipokumbusha alfajiri ile ya siku za baridi ya miaka 69 iliyopita, mzee Xia Shuqin akilengwa na machozi alisema kuwa, ni asubuhi moja tu, wavamizi wa Japan waliangamiza familia yake yenye watu 9. Anasema:

"Wavamizi wa Japan waligonga mlango kwa nguvu. Baba yangu alifungua mlango akipigwa risasi na akafa papo hapo. Mama yangu akimbeba dada yangu mdogo aliyejificha chini ya meza pamoja na mama wa jirani na watoto wake wawili. Wanajeshi wa Japan walimvuta mama yangu, wakamwua dada yangu mdogo kwa upanga, halafu wakamvua mama nguo zote na kumbaka. Baadaye walimlaza dada yangu mkubwa kwenye meza, na dada yangu wa pili kitandani na kuwabaka, mimi nilichomwa kwa upanga mara tatu."

Kwa hivyo, wanajeshi wa Japan waliingia nyumbani mwa Xia Shuqin kwa nguvu na kuwaua wanafamilia 7 bila ya sababu yoyote. Miongoni mwao, mama yake na dada wakubwa wawili wake walibakwa kabla ya kuuawa. Bi. Xia Shuqin aliyekuwa na umri wa miaka 8 wakati ule na mdogo wake aliyekuwa na umri wa miaka 4 tu walinusurika. Wasichana hao wawili waliishi kwa siku 14 kwenye maiti za jamaa zao wakitegemea chakula kidogo kilichobaki nyumbani, hadi walipogunduliwa na majirani.

Katika miaka 60 iliyopita, mzee Xia Shuqin kila akikumbusha msiba huo huwa hawezi kujizuia kulia, mpaka akaanza kuumwa macho. Lakini linalomsikitisha ni kwamba, nchi ya Japan iliyozusha msiba huo inajaribu kukanusha historia hiyo ya uvamizi, baadhi ya watu wa mrengo wa kulia wa Japan hata walimsingizia Bi. Xia Shuqin kuwa anatunga historia kwa makusudi. Alisema , atakuwa shahidi hai wa mauaji hayo kama yu hai hata kwa siku moja, atapambana na nguvu za mrengo wa kulia za Japan zinazokanusha mauaji ya Nanjing, na kuwaambia walimwengu ukweli wa mambo ya historia.

Licha ya Bi. Xia Shuqin aliyeshuhudia mauaji makubwa ya Nanjing, pia kuna ushahidi mwingine kama vile picha na maandishi yaliyorekodi tukio hilo. Picha zilizohifadhiwa na mzee Ruo Qing ni mashahidi bayana kabisa. Picha hizo zilipigwa na wanajeshi wa Japan wenyewe wakati wa kuwaua raia wa China.

Mzee Ruo Qing kabla ya kufariki dunia mwaka jana aliwahi kuhojiwa na mwandshi wetu wa habari, akisimulia alivyoshuhudia. Alisema kuwa, wakati wanajeshi wa Japan waliposhambulia Nanjing, alikuwa anafanya kazi katika studio ya upigaji picha ya Huadong mjini Nanjing. Siku moja, alikuja ofisa wa jeshi la Japan aliyetaka kusafisha mikanda miwili ya picha. Mzee Ruo Qing aliposafisha picha hizo alishtushwa akisema:

"Kumbe picha hizo zilipigwa wakati wauaji wa Japan walipokata vichwa vya wachina. Nilikimbia kumwambia mjomba wangu kuhusu picha hizo, akaniambia nisiongee kuhusu jambo hilo. Kutokana na picha zilizopigwa na wajapan hao niliona jinsi wanajeshi wa Japan walivyowaua wachina, kuwabaka wanawake na kuchoma moto nyumba. Nikaamua kusafisha picha hizo mara mbili na kuzihifadhi."

Kuanzia hapo, Bw. Ruo Qing alifuatilia sana picha zilizoletwa na wanajeshi wa Japan, na kuchagua picha zaidi ya 30 kuziweka katika albam ya picha aliyoitengeneza mwenyewe. Baada ya ushindi kupatikana katika vita dhidi ya wavamizi wa Japan, picha hizo zilikabidhiwa kwenye mahakama ya kijeshi ya Nanjing kama ushahidi wakati wa kuwahukumu wahalifu wa kivita wa Japan.

Historia haiwezi kusahaulika wala kubadilika, binadamu wakisahau historia, huenda msiba utarudi tena. Kwa hivyo, kila baadhi ya wajapan walipojaribu kukanusha historia hiyo, Wachina waliokumbwa na balaa la vita na Wajapan wanaoifahamu historia hiyo huiamsha serikali ya Japan na watu wake washughulikie suala la kihistoria kwa usahihi. Mwanafunzi wa Japan anayesoma mjini Beijing Bwana Yoshi Kazu Kato anasema.

"Mimi nakiri kuwa Japan iliwahi kuivamia China. Huu ni ukweli wa historia. Naona kuwa, Japan na China zinapaswa kufanya maingiliano na ushirikiano kwenye msingi wa kutambua historia na kupata mafunzo kutoka kwa historia. Hili ni jambo la muhimu sana katika kukuza uhusiano kati ya nchi zetu mbili."

Idhaa ya kiswahili 2005-06-02