Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-06-02 20:18:15    
Mlipuko watokea katika msikiti nchini Afghanistan na kusababisha vifo na majeruhi ya watu makumi kadhaa

cri

Tarehe 1 mwezi Juni, mlipuko ulitokea kwenye msikiti mmoja ulioko huko Kandahar, mji wa kusini wa Afghanistan, na kusababisha vifo vya watu 19 na watu wengine zaidi ya 50 kujeruhiwa. Mlipuko huo ni shambulizi kikatili kabisa la kimabavu kutokea nchini humo katika mwaka huu, na tukio hilo limewafanya watu waingiwe na wasiwasi tena kuhusu hali ya usalama nchini humo.

Tarehe 1 asubuhi, mamia ya wa-Afghanistan walikwenda kwenye msikiti mmoja mjini Kandahar kama kawaida, ili kuomboleza kifo cha kiongozi wa kidini Mawlavi Abdullah Fayaz aliyeuawa na Taliban tarehe 29 mwezi Mei. Wakati watu waliposali, mshambulizi mmoja wa kujiua alizusha mlipuko mkubwa ndani ya msikiti huo, na kusababisha vifo vya watu 14 papo hapo, wakiwemo mkuu wa polisi wa mji wa Kabul Akram Khakrezwal, na watu watano wengine walikufa baada ya kupelekwa kwenye hospitali. Mara baada ya mlipuko huo, jeshi la ulinzi wa taifa la Afghanistan lilizingira sehemu zilizo karibu mji huo.

Waziri wa mambo ya ndani wa Afghanistan Bw. Ali Ahmad Jalali siku hiyo kwenye mkutano na waandishi wa habari alisema kuwa, mshambulizi huyo si m-Afganistan, lakini alikataa kudokeza taarifa nyingine kuhusu mshambulizi huyo. Alilaani kuwa, mashambulizi ya kigaidi yaliyotokea hivi karibuni yote yamepangwa na wageni. Wakati huohuo, gavana wa mkoa wa Kandahar Bw. Gul Agha Sharzai pia alisema kuwa, kundi la Al-Qaeda na kundi la kigeni yanahusika na tukio hilo, na mshambulizi huyo ni mwanachama wa kiarabu wa kundi la Al-Qaeda. Ingawa maiti yake imebomolewa vibaya, lakini polisi wamepata nyaraka kadhaa kutoka kwenye maiti yake, kikiwemo kitambulisho chake. Bw. Sharzai pia alisema kuwa, hivi karibuni, baadhi ya wa-Arab wenye msimamo mkali wameingia kwenye sehemu ya kusini ya Afganistan, na wametishia kuwa wataanzisha mashambulizi mengi zaidi dhidi ya serikali ya nchi hiyo.

Mpaka sasa, bado hakuna jumuiya au mtu binafsi yeyote aliyetangaza kuwajibika na tukio hilo. Msemaji wa kundi la Taliban Latif Allah Hakimi tarehe 1 alitangaza kuwa, kundi la Taliban halihusiki na tukio hilo,na hawatafanya milipuko ya kujiua kwenye misikiti. Pia alisema kuwa, mlipuko huo ni matokeo ya migongano ya ndani ya serikali ya nchi hiyo.

Baada ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu wa nchi hiyo mwezi Oktoba mwaka jana, hali ya nchini humo iliwahi kutulia kwa muda, lakini hivi karibuni, matukio mbalimbali ya kimabavu yametokea mara kwa mara. Hali hiyo inaonesha kuwa, bado kuna matatizo mengi yatakayovurugu utulivu na usalama nchini humo. Kwanza, nguvu ya kundi la Al-Qaeda iliyobaki nchini humo na wanachama wa Taliban bado wanafanya kempeni mbalimbali. Habari zinasema kuwa, kundi la Taliban linapanga kuanzisha mashambulizi ya majira ya Spring, na kuvuruga uchaguzi wa bunge unaotarajiwa kufanyika katika nusu ya pili ya mwaka huu; pili, mabwana vita wa sehemu mbalimbali za Afghanistan bado wanadhibiti uchumi, fedha na utozaji wa kodi kwenye sehemu hizo, na mapambano yanatokea mara kwa mara kati yao na kuvuruga utaratibu wa kijamii na kuharibu utulivu wa kisiasa nchini humo. Aidha, kabla ya hapo, kutokana na tukio la jeshi la Marekani kudhalilisha Korani, maandamano ya kuipinga Marekani yalifanyika nchini humo na kusababisha vifo vya watu zaidi ya 15. hali hiyo inadhihirisha kuwa, hisia za kuipinga Marekani na kutoridhika na serikali bado zipo mioyoni mwa wa-Afghanistan. mambo hayo yote yataathiri hali ya usalama nchini humo, na kuathiri uchaguzi wa bunge la nchi hiyo unaotarajiwa kufanyika katika nusu ya pili ya mwaka huu. Hivyo, serikali ya Afghanistan bado inakabiliana na changamoto kubwa.

Idhaa ya Kiswahili 2005-06-02