Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-06-02 15:46:32    
Mkuu mpya wa benki ya dunia asema lengo la benki hiyo la hivi sasa ni kusaidia Afrika

cri

Mkuu mpya wa benki ya dunia anayeshika madaraka kuanzia tarehe mosi Juni Bw. Paul Wolfowitz alisema kuwa, lengo la benki hiyo ni kulisaidia bara la Afrika kuwa "bara lenye matumaini".

Bw. Wolfowitz alisema, dalili njema zimeonekana katika juhudi za kupunguza umaskini barani Afrika, uchumi katika baadhi ya nchi za Afrika umeanza kukua kwa nguvu. Hata hivyo nchi nyingi za Afrika bado zinakabiliwa na changamoto kubwa katika juhudi za kupunguza umaskini. Anatumai kuwa katika kipindi chake benki ya dunia itafanikiwa kuifanya Afrika liwe "bara lenye matumaini" badala ya "bara linalokata tamaa".

Bw. Wolfowitz pia alisema kuwa atatumia njia mbalimbali ili kuhakikisha benki ya dunia inashirikiana na sehemu mbalimbali duniani na kutoa misaada ya fedha na teknolojia zinazohitajika katika sehemu hizo na kuinua maisha ya watu walio maskini sana.

Aidha, Bw. Wolfowitz alisema, kuna haja kufanya mageuzi ya "muundo" wa benki ya dunia. Alimsifu mkuu aliyemtangulia wa benki hiyo kuwa mafanikio makubwa yalipatikana katika kipindi chake cha miaka 10, na hasa mafanikio dhidi ya ufisadi, kuhimiza usawa wa kijinsia na kutoa mwongozo kwa nchi zinazoendelea katika juhudi za kuondoa umaskini.

Bw. Wolfowitz mwenye umri wa miaka 61 alipendekezwa na rais George Bush kuwa mkuu wa benki hiyo mwezi Machi mwaka huu, na alikubaliwa na benki hiyo tarehe 31 Machi. Tokea Machi mwaka 2001 alikuwa naibu waziri wa ulinzi wa Marekani, alionelewa kuwa ni mmoja wa waamuzi wa kuanzisha vita dhidi ya Iraq. Kutokana na hali hiyo alitiliwa shaka kama anafaa kuwa mkuu wa benki hiyo.

Bw. Wolfowitz alizaliwa tarehe 22 Desemba, 1943 mjini New York, baada ya kumaliza masomo katika chuo kikuu aliendelea na masomo yake, mwaka 1967 na mwaka 1972 alipata shahada ya pili ya fasihi na shahada ya udaktari katika siasa kutoka Chuo Kikuu cha Chicago. Katika miaka ya 70 aliwahi kuwa mhadhiri na msaidizi katika Chuo Kikuu cha Yale.

Mwishoni mwa miaka ya 80 alikuwa balozi wa Marenani nchini Indonesia na baadaye katika miaka kati ya 1989 na 1993 alikuwa naibu waziri wa ulinzi na mwaka 1994 alikuwa mkuu wa taasisi ya masuala ya kimataifa katika chuo kikuu kimoja nchini Marekani.

Mwezi Februari mwaka 2001, kwa mara nyingine tena alikuwa naibu waziri wa ulinzi wa Marekani, alikuwa ni mmoja kati ya waamuzi wa mambo ya kijeshi ya Marekani.

Tarehe 16 Machi mwaka huu rais George Bush alimpendekeza kuwa mkuu wa benki ya dunia, kutokana na mapendekezo hayo Bush alishutumiwa na baadhi ya nchi na mashirika ya kimataifa. Lakini Bw. Wolfowitz alipohojiwa na waandishi wa habari alisema, kama akikubaliwa na bodi la wakurugenzi la benki ya dunia "hakika hatashinikiza benki ya dunia kwa ratiba ya Marekani" na kuahidi kwamba atajitahidi kadiri awezavyo kuondoa umaskini.

Hivi sasa benki ya dunia ina nchi wanachama 184 na raslimali dola za Kimarekani bilioni 188.22. Kazi yake ni kutoa mikopo kwa miradi ya uzalishaji mali na kutoa mwongozo kwa mpango wa mageuzi na kusaidia nchi zilizo nyuma kiuchumi kupata maendeleo.

Idhaa ya kiswahili 2005-06-02