Chansela wa Ujerumani Bw. Gerhard Schroeder tarehe 2 mwezi Juni alikwenda Luxembourg ambayo ni nchi mwenyekiti wa zamu wa Umoja wa Ulaya kujadiliana na waziri mkuu wa nchi hiyo Bw. Jean-Claude Junchker, pia ameamua kufanya mkutano na Rais Jacques Chirac wa Ufaransa huko Berlin. Hii imeonesha kuwa, baada ya Ufaransa na Uholanzi kupinga mkataba wa katiba ya Umoja wa Ulaya kwenye upigaji kura wa wananchi wote, Umoja wa Ulaya na viongozi wa nchi wanachama wa umoja huo wameanza kuchukua hatua za dharura kukabiliana na tatizo la kutopitshwa kwa mkataba huo, na kujaribu kutafuta njia ya kutatua tatizo hilo kwenye mkutano wa wakuu wa Umoja wa Ulaya utakaofanyika katikati ya mwezi Juni.
Baada ya kufanya mkutano na Bw. Jean-Claude Juncker, Bw. Schroeder aliwaambia waandishi wa habari kuwa, ni muhimu sana kwa nchi wananchama wote wa Umoja wa Ulaya kumaliza taratibu zote za kupitisha mkataba huo, na Umoja wa Ulaya utaamua hatua baada ya taratibu kumalizika. Hivi sasa vitendo vyote vya kupita kiasi si sahihi.
Tarehe 29 mwezi Mei baada ya Ufaransa kupinga mkataba huo, Bw. Jean-Claude Juncker alifanya majadiliano kwa njia ya simu na viongozi wa nchi wananchama wote wa Umoja wa Ulaya. Habari zinasema kuwa, kabla ya mkutano wa wakuu wa Umoja wa Ulaya kufanyika, Bw. Juncker pia atafanya mkutano na viongozi hao na kujadiliana nao kuhusu hali ya umoja huo.
Aidha, kamati ya Umoja wa Ulaya, na bunge la Ulaya pia vitafanya mkutano maalum hivi karibuni ili kujadili suala hilo. Ingawa mkataba wa katiba ulikataliwa na Ufaransa na Uholanzi ambazo ni waanzilishi wa Umoja wa Ulaya, lakini viongozi wa Umoja wa Ulaya bado wanafanya juhudi kusukuma mbele nchi nyingine ambazo hazijafanya uamuzi zikamilisha taratibu za kupitisha mkataba huo. Lakini habari zinasema kuwa, Uingereza huenda itatangaza kusimamisha taratibu za kupitisha mkataba huo Jumatatu. Habari kutoka shirika la habari la AP zinasema kuwa, ofisa wa wizara ya mambo ya nje wa Uingereza alidokeza kuwa, mswada wa Uingereza kuhusu kupitisha mkataba wa katiba mwakani kwa upigaji kura wa wananchi wote umeahirishwa bila ya kikomo.
Ili kukabiliana na hali yoyote, inayoweza kutokea kwenye mkutano na waandishi wa habari uliofanyika baada ya Uholanzi kupinga mkataba wa katiba ya Umoja wa Ulaya, mwenyekiti wa kamati ya Umoja wa Ulaya Bw. Jose Manuel Barroso alitoa mwito akitaka nchi wananchama wa umoja huo zisichukue hatua yoyote ya kusimamisha taratibu za kupitisha mkataba kwa upande mmoja kabla ya mkutano wa wakuu wa Umoja wa Ulaya. Tarehe 2 baada ya kufanya mkutano na viongozi wa vyama mbalimbali vya bunge la Ulaya, Bw. Barroso alisema tena kuwa anatumai viongozi wa nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya, hasa wakuu wa nchi hawatafanya uamuzi wowote wa upande mmoja, na kuwa makini na kuwajibika katika kipindi hicho maalum.
Msemaji wa kamati ya Umoja wa Ulaya Bi. Francoise le Bail tarehe 2 alisema kuwa, mpaka sasa Umoja wa Ulaya haujapata taarifa ya nchi yoyote kuhusu kusimamisha taratibu za kupitisha mkataba huo. Mkutano wa wakuu wa Umoja wa Ulaya utajadili hali ya umoja huo, lakini haijulikani utatoa uamuzi gani.
Viongozi wa Umoja wa Ulaya hawakabiliani na habari za kusikitisha tu. Baada ya Ufaransa na Uholanzi kukataa mkataba wa katiba, bunge la Latvia ambayo ilijiunga na Umoja wa Ulaya mwaka jana lilipitisha mkataba huo kwa kura nyingi, na kuwa nchi ya 10 iliyopitisha mkataba huo. Jambo hilo ni habari nzuri kwa Umoja wa Ulaya unaotaka kupunguza athari mbaya ya Ufaransa na Uholanzi kukataa mkataba huo.
Nchi wanachama kadhaa wa Umoja wa Ulaya zimetoa mapendekezo mapya kuhusu kutatua tatizo la kupitisha mkataba huo. Kwa mfano, Jamhuri ya Czech ilipendekeza kuahirisha muda wa mwisho wa kupitisha makataba wa katiba baada ya mwaka 2006, na waziri mkuu wa Austria Bw. Wolfgang Schuessel alipendekeza kufanya upigaji kura wa raia wote wa nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya. Mapendekezo hayo huenda yatajadiliwa kwenye mkutano wa wakuu wa Umoja wa Ulaya.
Idhaa ya Kiswahili 2005-06-03
|