Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-06-03 16:16:46    
Mkutano wa wakuu wa COMESA wataka kuimarisha umoja wa kanda hiyo

cri

Mkutano wa 10 wa wakuu wa COMESA ulifunguliwa jana huko Kigali, mji mkuu wa Rwanda. Wakuu waliohudhuria mkutano huo kwa kauli moja walizitaka nchi mbalimbali za COMESA ziharakishe mchakato wa umoja wa kanda hiyo, ili kupambana na changamoto zilizosababishwa na utandawazi

Kwenye sherehe ya ufunguzi wa mkutano, rais Paul Kagame wa Rwanda aliteuliwa kuwa mwenyekiti wa zamu wa COMESA. Alipohutubia sherehe hiyo aliwataka viongozi wa nchi mbalimbali wanachama waoneshe nia thabiti ya kisiasa katika mchakato huo. Rais Kagame alieleza kuwa mafanikio ya COMESA yanatokana na uwezo wa kufanya mkakati kwa pamoja kwa nchi mbalimbali wanachama. Alisema kuwa kwa kuwa nguvu za uchumi za nchi mbalimbali zote ni ndogo, kama soko hilo halitapanuliwa, nchi hizo hazitapata faida zinazotokana na utandawazi.

Mwenyekiti wa awamu iliyopita ya COMESA, rais Yoweri Museveni wa Uganda alifurahia mafanikio iliyoyapata COMESA katika kutatua migogoro ya kikanda na kuzitaka nchi mbalimbali zichukue hatua halisi za kutimiza umoja mapema iwezekanavyo. Alisema kuwa kasi ya ongezeko la uchumi wa nchi mbalimbali wanachama imeongezeka, lakini bado kuna safari ndefu kabla kutimiza lengo la maendeleo ya milenia.

Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika aliyehudhuria mkutano huo akiwa mgeni rasmi rais Olusegun Obasanjo wa Nigeria alisifu kazi zilizofanywa na COMESA katika kuziunganisha nchi za Afrika. Anaona kuwa ni kwa kuungana tu, ndipo Afrika itakapoweza kuendelea.

Kwenye sherehe ya ufunguzi, Libya iliyoko katika Afrika kaskazini imepokewa kuwa nchi ya 20 mwanachama wa COMESA.

Mkutano huo umefunguliwa wakati muungano wa ushuru wa forodha wa COMESA ambao uko mbioni kuanzishwa ulipokutana na vikwazo. Viongozi wanaohudhuria mkutano huo watatunga ratiba na mpango mpya wa muungano huo. COMESA lilitaka kuanzisha muungano wa ushuru wa forodha mwezi Desemba mwaka jana, kwa kuwa baadhi ya nchi wanachama zilikuwa na wasiwasi kuhusu mapato ya ushuru wa forodha, muungano huo umekwama.

COMESA ilianzishwa mwezi Desemba mwaka 1994 mpaka sasa imeitisha mikutano 9 ya wakuu. COMESA ni moja kati ya jumuiya kubwa kabisa za umoja wa uchumi barani Afrika. Nchi wanachama za COMESA zina watu karibu milioni mia 4 na kiasi cha pato la nchi hizo kimefikia dola za kimarekani bilioni 200. COMESA inafutailiwa sana kutokana na mafanikio yaliyopatikana katika umoja wa uchumi wa miaka ya karibuni.

Idhaa ya kiswahili 2005-06-03