Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-06-06 16:26:21    
Wakusanyaji vinyago vya Afrika, mume na mke Bw. Li Songshan na Bi. Han Rong

cri

Siku chache zilizopita, mume na mke Bw. Li Songshan na Bi. Han Rong walilizawadia Jumba la Sanaa la China vinyago vingi vya Afrika. Bw. Li Songshan na Bi. Han Rong wamekuwa wakijishughulisha na ukusanyaji wa vinyago kwa miaka mingi nchini Tanzania na walianzisha Shirikisho la Sanaa ya Makonde Tanzania.

Bw. Li Songshan ana umri wa miaka 64 na Bi. Han Rong miaka 60. Katika miaka ya 60 walijifunza lugha ya Kiswahili katika chuo ambayo ni lugha ya taifa ya Tanzania na Kenya na pia inatumika katika nchi nyingine za Afrika Mashariki. Baada ya kuhitimu, walifanya kazi ya kutafsiri vitabu. Mwishoni mwa miaka ya 70 na mwanzoni mwa miaka ya 80 watu hao wawili kwa mara kadhaa walitumwa na serikali ya China kwenda Tanzania kufanya kazi katika miradi iliyosaidiwa na China na kikundi cha matibabu cha China nchini humo. Katika miaka hiyo, hao wawili walipata nafasi ya kuwasiliana na vinyago vya Makonde. Bi. Han Rong alisema, "Kwa mara ya kwanza nilikuwa nchini Tanzania mwaka 1981 nikiwa mkalimani katika kikundi cha matibabu cha Wachina huko Makonde. Siku moja mkuu wa mkoa alifanya tafrija kutukaribisha na kutuzawadia kila mmoja kinyago kimoja cha mwili wa binadamu. Kinyago hicho kilikuwa kidogo na sikutia maanani sana, lakini baada ya kumaliza kipindi changu cha miaka miwili na kurudi nyumbani, kinyago kiliwashangaza baba na marafiki zangu kutokana na uzuri wake na mti wake wa mpingo. Tokea hapo nilianza kukusanya vinyago vya aina mbalimbali vya wanyama, maski na vitu vingine vya kuweka sakafuni, mezani na vya kutundikwa ukutani."

Makonde ni moja ya makabila ya Tanzania lililoko kusini mashariki mwa Tanzania, kwenye mpaka na Msumbiji. Wanaume wa kabila hilo wana mila ya kuchonga vinyago kwa mpingo ambavyo wageni huviita vinyago vya Makonde. Sanaa ya vinyago vya makonde inajulikana sana barani Afrika kutokana na historia yake ndefu ya kiasi cha miaka 200. Sanaa yake yenye mtindo asilia na dhahania inawapendeza sana wasanii duniani.

Mwaka 1984 Tanzania ilifanya maonesho ya vinyago vya Makonde katika Jumba la Sanaa la China mjini Beijing. Maonesho hayo yaliwashangaza wasanii wa China, hali ambayo ilimshitusha Bw. Li Songshan aliyekuwa mkalimani katika maonesho hayo. Wakati huo watu hao wawili walikuwa wamekwisha kusanya vinyago zaidi ya 100 lakini vyote vilikusanywa kutokana na mapenzi yao binafsi na hawakufahamu thamani ya vinyago hivyo.

Kutokana na maonesho ya vinyago vya Tanzania katika Jumba la Sanaa Bw. Li na Han walijibwaga katika ukusanyaji wa vinyago kwa kujinyima, na walianza kufanya utafiti wa sanaa na utamaduni husika. Bi. Han Rong aliwahi kusoma makala nyingi za Ulaya kuhusu sanaa ya vinyago vya Makonde, lakini yalikuwa ni melezo tu ya watu wa Ulaya, anaona afadhali awasiliane moja kwa moja na watu wa kabila la Wamakonde kwa lugha yao wenyewe ili aielewe kwa undani zaidi sanaa hiyo. Alisema, "Kwa sababu nawasiliana nao moja kwa moja kwa lugha yao naelewa kwa kina zaidi mila, desturi na utamaduni wao. Mtu akitaka kupata kitu katika utafiti wake wa sanaa, anapaswa aelewe

maisha yao na itikadi yao. "

Wanandoa hao walikuwa na ushabiki mkubwa na sanaa ya Makonde. Mwaka 1990 waliamua kuacha kazi na kuhamia Tanzania. Bw. Li alisema, "Utamaduni wa Afrika unatuvutia kwa nguvu kubwa, Afrika ni bara la chanzo cha binadamu, tusipofanya utafiti hatuelewi kuwa utamaduni, filosofia, sanaa na vitu vingi barani Afrika ni vyanzo vya utamaduni wa binadamu, tukiwa na mawazo hayo tuliamua kwenda Afrika."

Wanandoa hao walifika nchini Tanzania, walifanya biashara kila wawezavyo na huku wakijitahidi kukusanya vinyago na kufanya utafiti. Walienda kwa Wamakonde maskini kuwasaidia na kuweka urafiki nao na huku wakichunguza mawazo na hisia zao. Bi. Han Rong alisema, "Tunafahamiana sana nao na kila mahali penye watu hao tuliwahi kuwatembelea. Kutokana na kuongea nao kwa lugha moja, wanatutendea vema kama jamaa zao na wakiwa mawazo akilini mwao wanapenda kutueleza, wasanii wakiwa na shida wanatuambia bila wasiwasi. Tumekuwa kama kiini cha kuwaunganisha wasanii wa Makonde."

Katika miaka walipokuwa huko waliwahi kukumbwa na shida nyingi, na hata walihatarishwa maisha, japokuwa hivyo hawakurudi nyuma katika njia ya "kusaidia utamaduni kwa kufanya biashara". Kutokana na juhudi za miaka zaidi ya kumi wamekuwa wafanyabiashara wanaojulikana nchini Tanzania, na wamekuwa wakusanyaji wakubwa wa vinyago vya Afrika. Wamekusanya vinyago karibu elfu kumi vya Makonde ambavyo karibu vyote vinatokana na kazi ya wasanii wakubwa wa Makonde, na walijenga nyumba ya maonesho na kuanzisha Shirikisho la Sanaa ya Makonde".

Mwaka 2003 waliuzawadia mji wa Changchun, mji uliopo mashariki kaskazini mwa China, vinyago 500 na kuhifadhiwa katika jumba la sanaa la mji huo. Hivi karibuni walilizawadia Jumba la Sanaa la China mjini Beijing vinyago 157. Kadhalika, wanatayarisha maonesho ya "Afrika Imagine" katika sehemu ya makazi ya "Beijing Imagine" ili kuonesha vitu adimu vya sanaa ya Afrika. Bw. Li alisema, "Tuna vinyago vingi vilivyochongwa na wasanii wakubwa wa Makonde, vinyago hivyo ni mali kubwa, tunafikiria kulizawadia taifa letu la China kwani vitu hivyo siyo tena mali yetu bali ni ya binadamu wote."

Idhaa ya kiswahili 2005-06-06