Mwenyekiti wa mamlaka ya utawala wa Palestina Bw. Mahmoud Abbas tarehe 4 alisaini amri ya kutangaza kuahirishwa kwa uchaguzi wa tume ya utungaji sheria ya Palestina uliopangwa kufanyika mwezi Julai mwaka huu. Kitendo hicho cha Abbas kilipingwa vikali mara moja na kundi la Hamas la Palestina. Wachambuzi wameainisha kuwa mvutano kati ya Bw. Abbas na Hamas kuhusu tarehe ya kufanyika kwa uchaguzi huo umeonesha mgongano kati ya kundi la chama tawala Fatah na "kiongozi mpya wa kisiasa" Hamas na kugombea madaraka kati yao kuhusu utawala wa Palestina.
Bw. Abaas alifafanua chanzo cha kuahirisha uchaguzi wa tume ya utungaji sheria ya Palestina akisema kuwa, wajumbe wa tume hiyo bado wana maoni tofauti kuhusu mswada wa sheria ya uchaguzi na pande zote zinapaswa kufanya majadiliano na uratibu kwa muda mrefu zaidi, ili kufikia makubaliano. Lakini hakutaja tarehe ya kufanyika kwa uchaguzi huo. Ofisa mwandamizi wa Fatah alidokeza kuwa uchaguzi huo unaweza kufanyika kati ya mwezi Novemba mwaka huu na mwezi Januari mwakani.
Kundi la Hamas lilijibu mara moja uamuzi uliofanywa na Abaas. Msemaji wa Hamas Sami Abu Zuhri alieleza mjini Gaza kuwa kundi Hamas linapinga kuahirishwa kwa uchaguzi wa tume ya utungaji sheria. Alisema kuwa uamuzi huo wa Abbas umevunja mkataba uliofikiwa na utawala wa Palestina na makundi mbalimbali mwezi Machi mwaka huu mjini Cairo, na kuonesha kuwa utawala wa Palestina unafuatilia tu maslahi ya baadhi ya makundi, hasa Fatah kwenye ugawaji wa viti vya tume hiyo.
Hii ni mara ya kwanza kwa Hamas kushiriki kwenye uchaguzi huo tangu mwaka 1987 kundi hilo lilipoanzishwa. Katika muda mrefu uliopita, Hamas lilishikilia kufanya mapambano ya kisilaha. Lakini baada ya kushambuliwa na Israel, kundi hilo limeanza kutekeleza msimamo wa unyumbufu na kutaka kujiunga na mchakato wa kisiasa wa Palestina na utaratibu wa mkakati.
Vyombo vya habari vinaona kuwa Hamas limeweka changamoto kubwa kwa Fatah, kundi lenye hadhi ya chama tawala. Baada ya kufanya mapambano kwa muda mrefu, Kundi la Hamas sio tu limeweka msingi mkubwa ya maoni ya raia, bali pia limezingatia kuboresha sura yake. Kwenye uchaguzi wa mikoa wa kipindi cha pili wa Palestina uliofanyika hivi karibuni, kundi la Hamas lilipata tokeo la kushangaza kwa kupata theluthi moja ya mamlaka ya idara za minispaa za mikoa.
Ikilinganishwa na Hamas, kundi la Fatah ingawa ni chama kikubwa cha kwanza nchini Palestina, lakini ndani ya Fatah kuna makundi mengi, na ugombeaji wa madaraka kati yao ni mkubwa, hivyo nguvu yake imepungua.
Wachambuzi wanaona kuwa, uamuzi wa Bw. Abaas kuahirisha uchaguzi wa tume ya utungaji sheria, ni kutaka kujipatia muda mrefu zaidi wa kupunguza tofauti ndani ya Fatah na kujiimarisha, ili kukabiliana na changamoto kutoka kwa kundi la Hamas.
Idhaa ya kiswahili 2005-06-06
|