Kutokana na mpango uliowekwa, waziri mkuu wa Uingereza Bw. Tony Blair angewasili leo huko Washington kuwa na mazungumzo na rais Bush wa Marekani, ili kutafuta uungaji mkono wa Marekani kuhusu mpango wake wa kusaidia Afrika na kupunguza utoaji wa hewa ya carbon dioxide. Lakini vyombo vya habari vya Uingereza vilipozungumzia safari hiyo viliona kuwa huenda Bw. Blair atarudi mikoni mitupu.
Ikiwa ni nchi mwenyekiti wa mwaka huu wa kundi la nchi nane, Uingereza imechukulia kusaidia Afrika kuondokana na umaskini na kupunguza utoaji wa hewa ya carbon dioxide kuwa mada kuu ya mkutano wa wakuu wa nchi wa kundi la nchi nane wa mwaka huu. Mkutano wa nchi hizo umepangwa kufanyika mwezi wa Julai huko Scotland, ingawa muda umebaki mwezi mmoja hivi kabla ya mkutano huo kufanyika, lakini nchi hizo nane bado hazijaafikiana kuhusu masuala hayo mawili. Ili kutafuta uungaji mkono, Bw. Blair alijitahidi kuwashawishi viongozi wa nchi nyingine 7. Wiki iliyopita Bw. Blair alifanya ziara nchini Italia kuhusu suala hilo. Baada ya hapo alinuia kuzitembelea Marekani, Russia, Ufaransa na Ujerumani na kuwa na mazungumzo kwa njia ya simu na waziri mkuu wa Canada na waziri mkuu wa Japan ili kuanzisha mazingira kwa utekelezaji wa mpango wake wa kuisaidia Afrika na kupunguza utoaji wa hewa ya carbon dioxide.
Ni dhahiri kuwa kupata uungaji mkono wa Marekani ni suala muhimu sana kwa utekelezaji wa mpango wa Bw. Blair. Lakini vyombo vya habari vinaona kuwa kutokana na msimamo wa kukosa juhudi kwa Marekani kuhusu kuisaidia Afrika na ukaidi wake kuhusu suala la kupunguza utoaji wa hewa ya carbon dioxide. Hivyo Bw. Blair ni vigumu kupata mafanikio katika ziara yake nchini Marekani.
Mpango wa serikali ya Blair wa kuisaidia Afrika una sehemu tatu, ya kwanza ikiwa ni kundi la nchi nane kuongeza mara dufu utoaji msaada kwa nchi za Afrika katika miaka 10 ijayo na kufikia dola za kimarekani bilioni 100; Pili, kupendekeza kuanzisha "asasi za urahisishaji wa mambo ya fedha duniani" ambayo itafanya usimamizi juu ya fedha za misaada kwa Afrika na kuhakiksha kuwa fedha hizo zitatumika kwa njia mwafaka katika miradi ya elimu na tiba; na tatu, kusamehe kabisa madeni ya nchi za Afrika.
Hadi leo hakuna dalili inayoonesha kuwa, Marekani itakubali kuongeza msaada kwa nchi za Afrika. Msemaji wa Ikulu ya Marekani Bwana Scott McClellan hivi karibuni alisisitiza kuwa, Marekani siku zote inapiga hatua mbele katika kuzisaidia nchi za Afrika. Kuanzia mwaka 2001, msaada wa Marekani kwa nchi za Afrika umeongezeka kwa mara tatu. Maneno yake yameonesha kuwa, serikali ya Bush inaona kuwa, imetoa msaada wa kutosha kwa nchi za Afrika.
Kuhusu suala la kupunguza utoaji wa hewa ya carbon dioxide, na kuzuia hali ya hewa duniani isiongeze joto kwa haraka, Marekani inashikilia msimamo wa ukaidi zaidi. Marekani ni nchi inayotoa hewa ya carbon dioxide kwa wingi kabisa duniani, iliwahi kusaini mkataba wa Kyoto mwaka 1998 unaohusu kupunguza utoaji wa hewa ya carbon dioxide. Lakini mwezi March mwaka 2001, serikali ya Bush ilitangaza kujitoa kwenye mkataba huo kwa kisingizio cha ati kupunguza utoaji wa hewa ya carbon dioxide kutaathiri maendeleo yake ya uchumi. Baadaye wizara ya mambo ya nje ya Marekani ilisisitiza mara kwa mara kuwa, Marekani haitabadili msimamo wake wa kupinga mkataba wa Kyoto.
Japo kuwa Bw. Blair muda si mrefu uliopita alisisitiza kuwa, ikiwa Marekani inakataa kufanya mazungumzo na nchi nyingine kuhusu suala hilo, basi suala la kudhibiti hali ya hewa duniani kuongezeka kuwa joto kwa haraka haliwezi kupata maendeleo. Imedhihirika kuwa, Bw. Blair hawezi kulainisha msimamo huo wa Marekani katika mkutano wa wakuu wa kundi la nchi nane.
Vyombo vya habari vimeona kuwa, matokeo ya safari hiyo ya Bw. Blair nchini Marekani yatakuwa jaribio kwenye uhusiano maalum kati ya Marekani na Uingereza. Ikiwa Marekani inaendelea kupuuza juhudi za Uingereza, na kupinga mpango uliotolewa na Uingereza kuhusu kuzisaidia nchi za Afrika na kupunguza utoaji wa hewa ya carbon dioxide, huenda itaufanya mkutano wa wakuu wa kundi la nchi nane ushindwe kufikia malengo yanayotarajiwa. Jambo hilo litakuwa dosari ya maisha ya kisiasa ya Bw. Blair, pia litaathiri maoni ya watu wa Uingereza kwa uhusiano maalum kati ya Marekani na Uingereza.
Idhaa ya Kiswahili 2005-06-06
|