Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-06-07 19:28:01    
Safari nchini China

cri

      Mimi ni Xavier Telly Wambwa wa Bungoma Kenya, napenda kuwafahamisha wasikilizaji wenzangu kuhusu safari yangu nchini China. Niliweza kupata fursa ya kuitembelea miji ya Beijing na Xian. Nilipoangalia maswala mbalimbali kuhusu Hekalu la Tanzheshi, Hekalu la Yonghegong, Ukuta mkuu, Jumba la mikutano ya umma la Beijing, Bustani la Temple of Heaven, Forbidden City, summer palace, sanamu za askari na farasi wa mfalme Qinshihuan, Jumba la maendeleo ya Xian pamoja na Chuo kikuu cha mawasiliano cha Xian, hayo yote ni mambo ya maajabu unapotazama kwa macho yako mwenyewe.

Mazingira kuhusu watu wa China, ukweli ni kuwa wao ni watu wa amani, upendo wa hali ya juu na bila kusahau umoja. Sababu ni kuwa katika sekta mbalimbali, kwa mfano uzalishaji wa mazao, usafirishaji, miundo mbinu tofauti ya majengo ya kisasa ni ya kupendeza mno. Nilipomuuliza rafiki yangu wa dhati Bwana Xie Yi, (kijana wa idhaa ya kiswahili ya Radio China kimataifa ambaye aliniambatana nami na kuwa mkalimani wangu katika matembezi yangu) kuhusu maendeleo, yeye alinishangaza sana akisema maendeleo ya kila sehemu hapa nchini bila shaka yanalingana kwani ukitembelea miji tofauti ya mikoa, utadhani ni mji wa Beijing.

Lugha rasmi hapa nchini China ni kichina. Lakini wachina niliokutana nao niligundua kwamba wanaweza kuzungumza lugha za kimataifa kwa usanifu bila kusitasita au kutatanika. Wengi wasiojuwa lugha ya kiswahili na wanayo ile hamu ya kujua lugha hiyo, waliweza kuniuliza ruhusa ya kuwapa anuani yangu bila shaka kwa kutaka ushirikiano wa pamoja wa kujifunza lugha hizi mbili (kiswahili na kichina) na bila kusita nipata marafiki wengi wakiwemo wazee, vijana na watoto.

Nchini China hakuna waafrika wengi, basi niliweza kuulizwa, vipi nikafika China? Kulingana na swali hili, nilifurahi sana kuweza kupata fursa kubwa ya kuwaeleza kuhusu idhaa ya kiswahili ya CRI pamoja na vipindi kemkem kila siku hadi siku ya kupanda ndege bila tatizo lolote. Na kama vile CRI ni radio inayoongoza duniani nzima kuliko radio nyingine hivi sasa, sina budi kusema hongera Radio China kimataifa. Katika kila hali nimeweza kujisikia niko nyumbani licha ya kuwa mimi ni mgeni nchini China.

Mimi nilishuhudia kwa macho yangu mwenyewe. Natumai kwa wazo langu moyoni. Nilikuwa na wakati mgumu kuwajulisha wachina wengi kuhusu sehemu nitokako duniani. Nilipata fursa ya kutembelea jengo zuri la CRI lililojengwa kwa ustadi, ukweli ni kuwa nilibubujika moyoni mwangu kwa furaha na hata pia kukutana na watangazaji, wahariri na vijana ambao wamejitolea sana kuhakikisha kuwa CRI inatimiza lengo lake kwa wasikilizaji wake duniani. Bwana Fadhili Mpunji alifurahi sana aliponiona kwa mara ya kwanza macho kwa macho. Mimi nilidhani yeye ni mtangazaji mwafrika lakini kwa ajili ya CRI pamoja na hali ya hewa mjini Beijing, yeye amebadilika kidogo, hata vitendo vyake fulani vinafanana na mchina halisi.

Niliweza kukutana na mama Chen mkarimu ambaye aliweza kunihoji kupitia kwa studio ya Radio China kimataifa na nilihisi kuwa mtangazaji kwa dakika chache tu. Natumai siku moja nitakuwa mtangazaji wa CRI, Mola akinijalia.

Nchi ya China ni ya kupendeza mno. Ingawa ni mara yangu ya kwanza kusafiri nje ya nchi yangu Kenya, sijui hasa kama nchi za Ulaya zinalingana na China. Lakini maendeleo ya China ni ya kasi mno. Nakumbuka vyema nilipokuwa mgonjwa, katika hospitali mjini Beijing, nilishangazwa sana baada ya kupokea matokeo ya damu yangu iliiyochukuliwa kupimwa kwa dakika 5 tu kwa ukaguzi wa kila aina ya magonjwa mwilini mwangu na kupewa dawa za kichina ambazo ni za nguvu zilizoweza kuniponesha hadi kiwango cha kawaida wangu. Ukweli teknolojia ya matibabu ya China ni wa hali ya juu. Jambo lingine nilishangaa sana kuwaona polisi wa kichina kila mara wakisimama wima kila sehemu yoyote na wanatembea kigwaride au kulingana sana na masomo waliyohitimu. Hapo nawapa hongera kwa juhudi zao za kulinda usalama wa China.

Nilikuwa sijawahi kuona gari la moshi la ghorofa mbili pamoja hata pia gari la umeme chini ya ardhi (subway). Hali hii pekee ilithibitisha kuwa China ni nchi iliyositawi. Basi za kutumia umeme pia ziko nchini humo.

Katika safari yangu ya Xian nikitumia gari la moshi la mwendo wa kilomita 160 kwa saa moja kutoka Beijing, tulimaliza muda wa saa 12 njiani na nilishangazwa sana kwa tukio hilo. Hivyo ni kusema kila sehemu iko na hali halisi yake kwa sababu nikiwa ndani ya gari moshi linalotumia umeme, niliwaona wachina wakishughulika na shughuli za shamba la uzalishaji wa ngano pamoja na miti za matunda, maisha ya wachina ni ya kiujamaa wala siyo kiubinafsi. Hata pia idadi ya wanafuzni katika chuo kikuu nilichokitembelea mawasiliano cha Xian , kilikuwa na wanafunzi zaidi ya 3000, maana yake ni kuwa China inazingatia elimu pia. Ingawa kulikuwa na wakenya 7 tu katika chuo hicho.

Wasikilizaji wapendwa, natumai mtafuraia maelezo yangu kuhusu nilivyoiona nchini China. Ni mimi wenu msikilizaji hodari, Bw. Xavier L.Telly Wambwa.

Idhaa ya Kiswahili 2005-06-07