Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-06-08 20:31:31    
Vifaa vya kisasa vya kupambana na ugaidi

cri
Katika miaka ya karibuni, tatizo la ugaidi limekuwa likiikabili dunia nzima. Ili kuongeza uwezo wa kupambana na ugaidi, nchi nyingi duniani zinazingatia kutafiti na kutengeneza vifaa vya kiufundi vya kupambana na ugaidi. Ikiwa nchi itakayoandaa Michezo ya Olympiki, China imefanya juhudi kubwa katika kutafiti na kutengeneza vifaa vya kupambana na ugaidi. Hivi karibuni, maonesho ya kwanza ya vifaa vya kiufundi vya kupambna na ugaidi yalifanyika hapa Beijing, ambapo vifaa vingi vya kisasa vilivyotengenezwa na China vilioneshwa, na maonesho hayo yaliwavutia watu wengi.

Miongoni mwa vifaa hivyo, kuna kifaa kimoja kinachoitwa "Jicho lenye Waya". Kifaa hicho kinaweza kufanya kazi kubwa katika mapambano dhidi ya utekaji nyara wa ndege. Kama magaidi wakiwateka nyara abiria na kujificha kwenye ndege, na kutoa tishio la kuwaua abiria, polisi wa kikosi maalum watatoboa sakafu ya ndege na kuingiza waya mmoja mweusi wenye kamera kwenye kichwa chake, mpaka waya huo utokeze kwa sentimita 2 kutoka sakafuni, polisi watajua hali ndani ya ndege, na watachukua hatua mwafaka.

Kwenye maonesho hayo, kifaa hicho kilifuatiliwa na watu wengi. Kifaa hicho kimetengenezwa na kampuni ya Yingruida ya Beijing, fundi wa kampuni hiyo Bw. Sun Yichao alisema:


"Kifaa hicho ni tofauti na kifaa cha kawaida cha aina hiyo, kwa kuwa kifaa cha kawaida cha aina hiyo kinavaliwa na mtu mmoja tu kama miwani, lakini picha zinazochukuliwa na kifaa hicho kipya zinaoneshwa wazi, sio mtu mmoja tu bali watu wengi wanaweza kuziona. Na kifaa hicho kina waya laini, ambao unaweza kuelekeza kichwa chake kwenye upande wowote, aidha, kifaa hicho chenye uwezo wa kukinga maji ni chepesi, uzito wake haufikii kilogram 5."

Wataalamu wamefahamisha kuwa "jicho" hilo linaweza kuelekea kwenye upande wowote, na linaweza kuonesha picha dhahiri, hivyo kifaa hicho sio tu kifaa hicho kinaweza kufanya kazi kubwa katika mapambano dhidi ya ugaidi, bali pia kinaweza kuchukua nafasi ya binadamu kuingia kwenye mazingira yenye joto kali, hewa yenye sumu au mionzi ya nyuklia ambapo binadamu hawawezi kukaribia.

Kifaa kingine kilichooneshwa kwenye maonesho hayo ni kifaa kinachoweza kupima upande inakotoka risasi kutokana na milio ya risasi. Kifaa hicho kinaweza kufanya kazi kubwa katika tukio la mauaji ya kisiri. Baada ya kutokea kwa mauaji ya kisiri, kutokana na mazingira yenye utatanishi, ni vigumu kumgundua mwuaji kutokana na mlio wa risasi, hivyo kwa kawaida, mwuaji hukwepa na msako wa polisi. Polisi wakiwa na kifaa hicho, wataweza kumgundua mwuaji mara baada ya yeye kufyatua risasi.

Kifaa hicho kina sehemu mbili, moja ni nyaya za kupokea milio ya risasi, sehemu nyingine ni chombo cha kuchunguza milio hiyo. Mtafiti wa kampuni ya teknolojia ya umeme Bi. Lu Yanfang, ambaye ni msanifu wa mfumo wa kifaa hicho, alisema:


"Tunaweza kujua upande inakotoka risasi kwa kupokea na kuchunguza milio yake. Kuna aina mbili za milio ya risasi, wa kwanza  ni mlio wa risasi inapotoka kwenye mtutu wa bunduki, wa pili ni mlio wa risasi inaposafiri. Kifaa hicho kinaweza kupokea aina hizo mbili za milio ya risasi na kuichunguza, halafu tutajua mwuaji alipo."

Bi. Lu alisema kuwa kifaa hicho kinaweza kubadilisha milio ya risasi kuwa ishara ya umeme, na kuchunguza ishara hizo, na kuthibitisha mwuaji alipo ndani ya sekunde 1. Baada ya kupata taarifa hiyo, polisi wanaweza kuchukua hatua kwa haraka za kumzuia mwuaji kufyatua risasi tena, na kumkamata.

Kwenye maonesho hayo, kifaa kingine kilivutia watu wengi. Kifaa hicho kinaweza kutambua kama watu wameficha vitu vya chuma kwenye viatu vyao au la, mwandishi wetu wa habari alifanya jaribio: aliposimama kwenye kifaa hicho bila kuweka kitu chochote kwenye viatu,  kifaa hicho kilionesha taa ya rangi ya kijani, lakini alisimama akiwa na msumari kwenye kiatu, kifaa hicho kilitoa onyo mara moja. Fundi wa kampuni ya usalama wa ndege za abiria ya Beijing Bw. Chen Guang alifahamisha akisema:


"Kwa kupitia kukagua uzito wa viatu, kifaa hicho kinajua kuna kisu au vitu vingine vya chuma humo ndani au la. Kama uzito wa viatu ukipita kiasi au uzito wa viatu vya kushoto na kulia ukiwa tofauti, kifaa hicho kitatoa onyo. Kifaa hicho kinatumia teknolojia ya kisasa duniani."

Kwenye maonesho hayo washabiki wa mambo ya kijeshi walivutiwa kabisa na bunduki yenye mtutu wenye mdomo wa milimita 12.7. Hivi sasa, magaidi wana silaha kali, baadhi yao wana bunduki aina ya submachine, vifaa vya kurushia makombora na hata maderaya, kutokana na hali hiyo, polisi wa kikosi maalum cha kupambana na ugaidi wanapaswa kuwa na silaha kali zaidi ili kukabiliana na magaidi wakatili.

Imefahamika kuwa bunduki ya aina hiyo ina darubini za aina mbalimbali, na inaweza kupiga shabaha lililoko umbali wa mita 1500, aidha, ina risasi za aina mbalimbali, ambazo kila aina ina umaaalum, na baadhi yake zinaweza kupenya deraya.

Msanifu wa bunduki ya aina hiyo wa kampuni ya silaha ya China Bw. He Weiping alisema kuwa bunduki hiyo imetengenezwa kwa kutumia teknolojia nyingi za kisasa.


"Tuliposanifu bunduki hiyo tulitumia vifaa vya aina mpya na ustadi mpya, ambao unatumika kwa mara ya kwanza nchini China.

Kwenye maonesho hayo, mashirika karibu 200 yalionesha vifaa vyao vya kupambana na ugaidi, silaha tulizofahamisha ni sehemu ndogo tu ya vifaa hivyo. Vifaa hivyo vitakuwa vitasaidia polisi wa Beijing wakati wa Michezo ya Olympiki ya 2008.
Idhaa ya Kiswahili 2005-06-08