Wajumbe 150 wa vyama vya madhehebu ya Sunni vya Iraq tarehe 8 huko Baghdad walifanya mkutano, wakitaka kuongezewa idadi ya wajumbe wa madhehebu ya Sunni kwenye kamati ya utungaji katiba ya nchi hiyo. Wajumbe hao waliona kuwa, kama idadi ya wajumbe wa madhehebu ya Sunni haitaongezwa hadi kufika 25, watasusia mchakato wa utungaji wa katiba na kuitisha watu wa fani mbalimbali kuunda chombo cha usuluhishi ili kujipatia uungaji mkono.
Siku hiyo, kiongozi wa mfuko wa dini wa madhehebu ya Sunni Bwana Adnan al-Dulaimi pia alitaka kuongezewa wajumbe 25 wa madhehebu ya Sunni, na kudai kuwa, wajumbe wa madhehebu ya Sunni wapewe haki ya kupiga kura sawa na wajumbe wengine. Aliongeza kuwa, katiba mpya inapaswa kulinda umoja wa Iraq na umaalum wa waarabu, na isiruhusiwe kuweka mambo yatakayokwenda kinyume na imani ya kiislamu.
Hivi sasa kati ya wajumbe 55 wa kamati ya utungaji katiba kuna wajumbe 2 tu wa madhehebu ya Sunni. Japokuwa idadi hiyo iliongezwa kufikia 17, lakini wajumbe hao hawana haki rasmi ya kupiga kura. Habari zinasema kuwa, wajumbe wa vyama vya madhehebu ya Sunni wameorodhesha majina ya watu 25 na kuamua kuikabidhi kwa bunge la mpito la Iraq.
Kutokana na kuwa, waislamu wa madhehebu ya Sunni walisusia uchaguzi wa bunge uliofanyika mwezi Januari mwaka huu, hivyo kati ya viti 275 vya bunge la mpito, kuna wabunge 13 tu wa madhehebu ya Sunni. Madhehebu ya Sunni yaliwekwa kando katika mchakato wa ukarabati wa kisiasa. Lakini waislamu wa madhehebu ya Sunni wanachukua asilimia 20 ya idadi ya watu wa Iraq. Kamati ya utungaji katiba itakabidhi mswada wa katiba katikati ya mwezi Agosti, na kufanya upigaji kura za maoni ya raia mwezi Oktoba. Kutokana na katiba ya serikali ya mpito, kati ya mikoa 18, ikiwa theluthi mbili ya wapiga kura katika mikoa mitatu wakipiga kura za hapana, katiba mpya haiwezi kupitishwa, na bunge la mpito pia linapaswa kuvunjwa na kufanya uchaguzi upya. Na ratiba ya uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika mwishoni mwa mwaka huu na jeshi la Marekani kuondoka Iraq pia itaathirika.
Waislamu wa madhehebu ya Sunni pia wataathiri mchakato wa ukarabati wa usalama wa Iraq. Kama maslahi yao ya kisiasa hayawezi kutoshelezwa, vyama vya madhehebu ya Sunni havitaweza kuwashawishi watu wake waache kuunga mkono vikundi vya wanamgambo dhidi ya jeshi la Marekani na serikali ya wa-Shia.
Zaidi ya hayo, mgogoro wa kugombea madaraka kati ya madhehebu ya Sunni na madhehebu ya Shiya na wakurd, na msimamo wa madhehebu ya Sunni wa kutoshirikiana katika mchakato wa ukarabati wa siasa na usalama huenda utazidisha uwezekano wa kuzusha vurugu nchini Iraq. Chama cha wazee wa madhehebu ya Sunni hivi karibuni kiliilaani serikali ya madhehebu ya wa-Shia kuanzisha "Operation Lightning" dhidi ya raia wa madhehebu ya Sunni, lakini kundi la Badr Brigade la kamati kuu ya mapinduzi ya waislamu ya Iraq (SCIRI) liliwaua kwa siri watu wa dini wa madhehebu ya Sunni. Lakini kiongozi wa SCIRI Bwana Abdel Aziz al-Hakim na rais Talabani ambao ni wa-wakurd wa Iraq tarehe 8 walieleza kuunga mkono kundi la Badr Brigade.
Kwa hivyo kuwapatia au la watu wa madhehebu ya Sunni haki kubwa zaidi katika utungaji katiba ni suala lenye utatanishi, kama suala hilo haliwezi kutatuliwa vizuri, hali isiyo tulivu ya Iraq itaongezeka kuwa ya wasiwasi zaidi, na mchakato wa ukarabati wa siasa wa nchi hiyo pia utaathirika.
|