Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-06-10 16:19:28    
Mohmoud Abbas afikia makubaliano na makundi mbalimbali ya Palestina kuhusu kulinda hali ya usimamishaji vita kati ya Palestina na Israel

cri

Mwenyekiti wa mamlaka ya utawala wa Palestina Bw. Mohamoud Abbas tarehe 9 alifanya mazungumzo na viongozi wa makundi mbalimbali yenye silaha ya Palestina katika sehemu ya Gaza, na kufikia makubaliano kuhusu kulinda hali ya usimamishaji vita kati ya Palestina na Israel, na kuleta mazingira mwafaka kwa ajili ya kutuliza hali ya pande hizo mbili iliyokuwa hatari kwa muda mrefu.

Mohmoud Abbas alifanya mazungumzo na makundi mbalimbali ya Palestina mjini Gaza wakati ambapo hali ya usimamishaji vita imekuwa hatarini. Tarehe 7, askari wa jeshi la Israel walimwua kamanda mwenye cheo cha juu wa kundi la Islamic Jihad huko Jenin na kundi la Jihad lilijibu mashambulizi kwa kurusha mabomu kwenye makazi ya Wayahudi yaliyoko katika sehemu ya Gaza na kusababisha vifo vya watu watatu. Ili kuzuia hali isiendelee kuwa mbaya, Abbas tarehe 8 aliwasili mjini Gaza na kukutana na makundi mbalimbali ya Palestina.

Katika mazungumzo yaliyofanyika tarehe 9, Abbas alisisitiza kuwa kulinda hali ya usimamishaji vita kunaambatana na maslahi ya msingi ya Palestina. Aliyahimiza makundi mbalimbali hayo yafuate mkataba wa kusimamisha vita kati ya Palestina na Israel, kusimamisha vitendo vyote vya kuishambulia Israel na kutoipa Israel kisingizio cha kuishambulia Palestina. Abbas pia alikubali makundi ya Palestina yajiunge na kazi za matayarisho ya kuondoka mjini Gaza kwa Israel.

Baada ya mazungumzo hayo, msemaji wa Hamas alieleza kuwa kundi hilo litaendelea kufuata mkataba wa kusimamisha vita na kiongozi wa Jihad pia alieleza kuwa kundi hilo litafuata mkataba huo kwa muda, lakini aliyataka makundi mbalimbali ya Palestina yafikiri tena kuendelea na msimamo huo katika hali ya Israel kuvunja mkataba huo mara kwa mara.

Tangu mwezi Februari mwaka huu, Palestina na Israel zilipofikia makubaliano kuhusu kusimamisha vita, hali ya Palestina na Israel imekuwa ya utulivu kwa ujumla. Lakini Israel haikusimamisha msako kwa watu wenye silaha wa Palestina na watu wenye silaha wa Palestina pia walishambulia kwa mabomu shabaha za Israel. Lakini siku hizi pande hizi mbili zimejitahidi kulinda hali ya utulivu. Kwa hiyo, safari hii Abbas aliwasiliana na makundi mbalimbali ya Palestina kwa wakati na ni juhudi kubwa alizofanya Abbas kwa ajili ya kulinda amani kati ya pande hizo mbili.

Kadiri hali ya Palestina na Israel inavyoendelea, hakuna uhakika kama mgogoro kati ya makundi yenye silaha na jeshi la Israel utapanda ngazi. Sasa kuna wasiwasi ndani ya Palestina, yaani Israel inawezekana kufanya mashambulizi mazito dhidi ya watu wenye silaha wa Palestina kabla ya kuondoka katika sehemu ya Gaza, ili kuwazuia wasifanye mashambulizi mapya. Wakati Israel ilipoeleza kuchukua msimamo wa kujizuia, mshauri mkuu wa jeshi la Israel Bw. Dan Halutz tarehe 7 alionya kuwa uvumilivu wa Israel unapungua siku hadi siku. Kwa hiyo, watu bado wataendelea kutazama kuwa hali ya utulivu ya Palestina na Israel itakuwaje baada ya Abbas kufanya mazungumzo na makundi mbalimbali ya Palestina na kuendelea kufuata mkataba wa kusimamisha vita kati ya Palestina na Israel.

Idhaa ya kiswahili 2005-06-10