Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-06-14 16:05:10    
Barua 0614

cri

Leo kwanza tunawaletea barua tulizopokea kutoka kwa wasikilizaji wetu, baadaye tutaendelea kuwaletea mazungumzo kati yetu na msikilizaji wetu Bwana Telly Wambbwa wa Bungoma Kenya ambaye alipata ushindi katika shindano la chemsha bongo kuhusu miaka 55.

Msikilizaji wetu Mary D. Ndunguru wa sanduku la posta 8145 Arusha Tanzania anasema katika barua yake anatusalimu wafanyakazi wa idhaa ya kiswahili ya Radio China salaam, na kutuambia kuwa yeye ni mzima. Mbali na salamu anatushukuru kwa barua tunazoandikiana mara kwa mara, lakini pia anatuomba tumsamehe kwa yeye kuchelewa kuwasiliana nasi, hii ni kutokana na matatizo yaliokuwa nje ya uwezo wake.

Anasema matangazo yetu anayapata vema kabisa, ila alikuwa anaomba kipindi cha salamu kiongezwe muda. Anaona kipindi hiki ni kifupi mno kwake yeye, pia matangazo yetu kwa ujumla ni mazuri ila muda, maana yeye anasikiliza kupitia idhaa ya kiswahili ya KBC, hivyo anaona muda wa nusu saa ni mfupi mno.

Anasema jambo jingine ni kuhusu lugha ya kichina, anauliza, je hatuna utaratibu wa kuchapisha vijitabu ili nao huko Kenya waweze kujifunza kichina? Maana anakumbuka tumewahi kumtumia makaratasi ambayo yanafundisha lugha hiyo ya kichina, na mpaka sasa anasemahayo makaratasi anayo, ila anasikitika kuwa hatujamtumia tena, yeye anawapenda sana Wachina, na pia anapenda kujifunza lugha yao. Na anatumaini tutazingatia ombi lake. Anasema atakuwa nasi bega kwa bega katika matangazo yetu na pia kuchangia mawazo. Anaomba tumtumie vijarida kama tutakuwa tunachapisha.

Tunamshukuru sana msikilizaji wetu huyo Mary Ndunguru kwa barua yake na ushauri wake, na mengi tulifahamisha mara kwa mara katika kipindi hiki cha sanduku la barua, kwani yanafuatiliwa na wasikilizaji wetu wengi, na tunaahidi kufanya juhudi bila kulegea, kama tukipata nafasi tutajitahidi kuyatatua masuala hayo kama vile muda mfupi wa vipindi hasa kipindi cha salamu zenu na kadhalika.

Msikilizaji wetu mwingine Stephen Magoye Kumalija wa shule ya msingi Kiliwi Mwamashimba Division sanduku la posta 1421 Mwanza Tanzania, anasema katika barua yake kuwa anapenda atoe maoni yake au makala kuhusu gonjwa lisitibika ambalo walimwengu wanapambana nalo, na angeomba maelezo haya yachapishwe kwenye jarida letu dogo la daraja la urafiki, litakalo chapiswha katika siku zijazo.

Anasema tangu ungonjwa wa ukimwi ugunguliwe duniani miaka 22 iliyopita. Kwa mara ya kwanza kuna dalili kuwa juhudi za kupambana nao angalau zimeanza kuleta matumanini, tumaini la kwamba tunaweza kupunguza kasi ya kuenea kwa ukimwi na virusi vyake na kudhibiti athari zake.

Dunia nzima inaendelea kupata tumaini kutokana na utafiti wa dawa ambazo zinaweza angalau kupunguza kasi ya kuzaliana kwa virusi vya ukimwi mwilini. Ingawa dawa hizi hazijaweza kutibu ukimwi hadi mtu akapona, na ghalama ni kubwa mno, lakini juhudi za utafiti wa dawa zimeanza kutoa tumaini kwa binadamu wote. Ujumbe wa siku ya ukimwi duniani unahimiza nchi zinazoendelea, serikali, mashirika na makampuni ya mada ya kutoigawa dunia. Kati ya wale ambao wanatumaini la kupata dawa na misaada na wale ambao hawawezi. Ili kuhakikisha kuwa dawa zinazogunduliwa na huduma za afya zinazostahili, zinawafikia wagonjwa wa ukimwi duniani kote.

Ukimwi ni tatizo la dunia nzima, hakuna mtu au nchi ambayo ni salama kabisa dhidi ya ukimwi na athari zake. Takwimu za mpango wa umoja wa mataifa wa kudhibiti Ukimwi (UNAIDS) zinaonesha kuwa zaidi ya watu milioni 40 wameambukizwa virusi vya ukimwi hadi sasa, wengi zaidi yao wako Afrika kusini mwa sahara.

Kwa hiyo usambazaji wa habari za elimu juu ya ukimwi lipewe kipaumbele. Njia mbalimbali za kuelimisha zinaendelee kutumika zikiwemo redio, magazeti, sinema, mikutano ,machapisho, televisheni na njia nyingine. Lengo kuu ni kumwezesha kila mtu kuelewa ugonjwa huu wa ukimwi na kutambua hatari inayomkabili kila mtu, na kuchukua hatua za kujikinga. Anasema kwa leo yake ni hayo tu, hana mengi zaidi bali anaomba maelezo yachapishwe kwenye toleo lijalo la jarida letu dogo la Daraja la Urafiki.

Tunamshukuru sana msikilizaji wetu Stephen Magoye Kumalija kwaa ufuatiliaji wake kwa vipindi vyetu na jarida letu dogo la Daraja la urafiki, tena ametoa maoni yake mazuri kuhusu ugonjwa wa ukimwi ambao ni changamoto inayotukabili binadamu wote, kuhusu hayo, hakika tutaweza kuchagua makala kama hizo na kuzichapisha kwenye jarida letu dogo la daraja la urafiki. Ni matumaini yetu kuwa, wasikilizaji wetu wataendelea kutuletea maoni na mapendekezo kuhusu sekta mbalimbali.

Msikilizaji wetu Mbarouk Msabah wa sanduku la posta 52483 Dubai-U.A.E ametuletea barua akituandika hadithi moja fupi kwa kuonesha uungaji mkono wake wa dhati kwa Jamhuri ya watu wa China juu ya swala la mkoa wake wa Taiwan urudi na kujiunga na China. Hadithi hiyo inaitwa: Mama aliyepotelewa na watoto wake watatu".

Hadithi hiyo inasema hivi, hapo zama za kale alikuwepo mama mmoja mwenye watoto wengi aliyekuwa akiitwa "China". Siku moja ghafla alipotelewa na watoto wake watatu aliokuwa akiwapenda sana, wawili kati yao hao walichukuliwa na wageni waliokuwa wakitokea barani Ulaya. Watoto hao ni "Hong Kong" ambaye aliyelelewa na waingereza na mwingine ni "Macau" aliyelelewa na wareno. Mtoto wa watu "Taiwan" aliamua mwenyewe kutoroka nyumbani na kwenda kuishi peke yake.

Mama China siku zote alikuwa ni mtu mwenye huzuni na majonzi makubwa kwa kupotelewa na watoto wake hao watatu aliokuwa akiwapenda mno. Siku zilizpopita watoto "Hong Kong" na "Macau" walikuwa na kupata akili, walianza kumtafuta mama yao mzazi "China". Hatimaye walipofanikiwa kumpata na wakarudi nyumbani walikozaliwa kwa furaha kubwa isiyo kifani. Naye mama China alishukuru Mungu kuwaona tena wanawe baada ya kupita miaka mingi na alilia kwa furaha huku akiwakumbatia watoto wake Hong Kong na Macau.

Lakini mtoto wa tatu aliyebakia "Taiwan" alionesha tabia ya ukaidi na kusikiliza maneno ya watu waovu ambao hawapendi kumwona mama China akiungana tena pamoja na mwanawe Taiwan. Hata hivyo mama China hakukata tamaa hata kidogo ya kumwona mtoto wake Taiwan akirudi nyumbani alikozaliwa na kuishi pamoja tena kwa furaha kama vile walivyofanya ndugu zake Hong Kong na Macau, kwani wahenga walisema: "Mwenda kozi na omo hurejea ngamani".

Haya wasikilizaji, huu ni utaalamu mwingine wa wasikilizaji wetu, kuweza kunielezea hali halisi ya China kwa kutumia hadithi zenye mahadhi ya Kiafrika. Bwana Msabah amejitahidi kueleza kwa ufupi na kwa ufasaha, hali ya mikoa ya China iliyopotea na kurudi.

Idhaa ya kiswahili 2005-06-14