Mashindano ya ubingwa wa soka ya vijana ya kimataifa ya FIFA mwaka 2005 yalifunguliwa tarehe 10 nchini Uholanzi. Kwenye mchezo wa raundi ya kwanza wa kundi B, timu ya China iliiangusha timu ya Uturuki ambayo ilichukua nafasi ya pili kwenye mashindano ya vijana ya Ulaya kwa magoli mawili kwa moja na kuweka mwujiza wa kwanza tangu mashindano hayo yalipofunguliwa. Matokeo ya michezo mingine ni hivi: Marekani iliishinda Argentina, Nigeria ilitoka sare na Brazil, Korea Kusini ilifungwa na Uswisi, Syria ilitoka sare na Canada na Italia ilichapwa na Colombia. Hadi hapo, michezo ya raundi ya kwanza kwenye makundi ilimalizika. Uholanzi, China, Ukraine, Hispania, Chile, Marekani Ujerumani, Uswisi na Colombia zilipata ushindi na huenda zitajitokeza kwenye makundi yao.
Mchezo wa kituo cha Ujerumani wa mashindano ya kulenga shabaha kwa bunduki ya kombe la dunia mwaka 2005 ulimalizika tarehe 12. Mchezaji wa China Tan Zongliang alipata medali ya dhahabu kwenye mchuano wa kulenga shabaha kwa bastola kwa mita 10 kwa wanaume.
Mashindano ya 21 ya timu kamambe za mpira wa wavu za wanawake yalifungwa tarehe 12 nchini Uswisi. Kwenye fainali ya mashindano hayo, timu ya China ilishindwa kwa timu ya Brazil kwa seti tatu kwa mbili na kushika nafasi ya pili kwenye mashindano hayo. Timu ya Brazil ilichukua ubingwa.
Mashindano ya mwaliko ya mpira wa wavu ya wanaume ya kimataifa yalimalizika tarehe 12 mjini San Diego, Marekani. Timu ya China iliishinda timu ya Australia kwenye mchezo wa kugombea nafasi ya tatu na kupata nafasi ya tatu kwenye mashindano hayo. Kwenye fainali ya mashindano hayo, timu ya Uholanzi iliishinda timu ya Marekani na kupata ubingwa wa mashindano hayo.
Mashindano ya tuzo kubwa ya riadha ya Reebok yalifanyika tarehe 11 mjini New York. Mchezaji wa China Liu Xiang ambaye ni bingwa wa michezo ya Olimpiki ya Athens hakucheza vizuri na kushika nafasi ya tatu tu kwa muda wa sekunde 13.11. Mchezaji maarufu wa Marekani Allen Johnson alipata ubingwa kwa muda wa sekunde 13.03 na kuvumbua mafanikio mazuri kabisa mwaka huu. Mchezaji mwingine wa Marekani Dominique Arnold alishika nafasi ya pili.
Mchezo wa kumuaga mchezaji nyota wa soka wa Liberia George Weah ulifanyika mjini Marseilles, Ufaransa. Katika mchezo huo, George Weah alifunga magoli matatu na kumaliza vyema maisha yake ya soka. George Weah alikuwa kinara wa soka wa Afrika, Ulaya na dunia mwaka 1995.
Idhaa ya kiswahili 2005-06-14
|