Rais Thabo Mbeki wa Afrika ya Kusini tarehe 14 alitangaza kumwondoa madarakani makamu wa rais Jacob Zuma kutokana na kujihusisha na ufisadi, na kumaliza makisio ya wiki kadhaa kuhusu mustakabali wa kisiasa wa Bw Zuma, na kupunguza mgogoro wa kisiasa wa nchi hiyo.
Bw. Mbeki alitangaza uamuzi huo kwenye mkutano wa pamoja wa mabaraza mawili ya bunge la Afrika ya Kusini uliofanyika mjini Cape Town. Alisema kuwa, kutokana na maslahi ya serikali na nchi, aliamua kumwondoa madarakani Bw. Zuma. Alitumai kuwa, uamuzi huo utazidisha uaminifu wa wananchi kwa serikali. Vyombo vya habari vimeona kuwa, uamuzi huo wa rais Mbeki unalenga kumaliza haraka mgogoro ambao ni mbaya kabisa wa kisiasa nchini humo tangu chama cha ANC kishike madaraka.
Mgogoro huo ulianzia kesi ya Bwana Schabir Shaik, ambaye ni mshauri wa zamani wa fedha wa Bwana Zuma, pia ni rafiki yake wa miaka mingi. Mahakama kuu ya Durban baada ya kufanya uchunguzi kwa miezi 7, mwanzoni mwa mwezi huu ilimhukumu Shaik kwa makosa mawili ya kutoa rushwa na hatia moja ya udanganyifu. Bw. Shaik alishtakiwa kwa kumpa Bw. Zuma rushwa ya dola za kimarekani elfu 196 kuanzia mwezi Oktoba mwaka 1995 hadi mwezi Septemba mwaka 2002, ili kumshawishi Bw. Zuma amsaidie kupanua biashara yake. Bw. Shaik pia alihukumiwa kumsihi Zuma apokee rushwa ya dola ya kimarekani elfu 75 hivi kutoka kampuni ya silaha ya Ufaransa, ili kuilinda kampuni hiyo isifanyiwe uchunguzi na serikali kwenye biashara yake kubwa ya silaha. Tarehe 8 mwezi huu mahakama hiyo ilimhukumu Bw. Shaik kutumikia kifungo cha miaka 15 cha jela. Jaji mkuu alisema kuwa, kuna uhusiano wa ufisadi kati ya Shaik na Zuma, idara ya mashitaka ya Afrika ya Kusini imeanza kufanya uchunguzi kuhusu mashitaka ya Zuma.
Hii ni moja ya kesi zilizohusiana na maofisa wa ngazi ya juu kabisa na zenye athari kubwa zaidi nchini Afrika ya Kusini tangu nchi hiyo itokomeze utaratibu wa kikaburu miaka 11 iliyopita, imevutia uangalifu mkubwa nchini humo na kuzusha "tetemeko kali" kwenye jukwaa la kisiasa la nchi hiyo. Ingawa Zuma alijitetea kutokuwa na hatia yoyote, lakini katika siku za karibuni, sauti kutoka fani mbalimbali za jamii na bunge za kumtaka ajiuzulu zinaongezeka siku hadi siku. Mvutano kati ya wanaomwunga mkono na wanaompinga ulipamba moto, na kukifanya chama cha ANC kikabiliwe na mgogoro mkubwa wa kisiasa.
Mgogoro huo ulimpa rais Mbeki shinikizo kubwa. Akiwa naibu mwenyekiti wa chama cha ANC, Bw. Zuma aliwahi kufanya mchango mkubwa katika kuchaguliwa kuwa rais kwa Mbeki, yeye pia ni mgombea mkubwa wa rais baada ya rais Mbeki amalize awamu yake ya pili mwaka 2009. Kukabiliwa na shinikizo kubwa kutoka vyama vya upinzani na hamaki za wananchi, rais Mbeki aliyewahi kusisitiza kwa mara nyingi nia ya kutokomeza ufisadi alipaswa kukata shauri na kufanya uamuzi wa kumwondoa madarakani Bw Zuma ili kupata uaminifu wa wananchi.
Uamuzi huo wa rais Mbeki ulipata uungaji mkono mkubwa kutoka fani mbalimbali za chama tawala na vyama vya upinzani. Rais wa zamani wa nchi hiyo Bwana Nelson Mandela alisema kuwa, "Bw. Zuma aliwahi kutoa mchango mkubwa kwenye mchakato wa ukombozi na demokrasia wa nchi hiyo, tumesikitishwa sana na jambo hilo. Tunaunga mkono uamuzi wa rais Mbeki." Mwenyekiti wa chama cha Democratic Alliance, ambacho ni chama kikubwa kabisa cha upinzani Bwana Tony Leon alisema kuwa, uamuzi wa rais Mbeki umeonesha nia ya Afrika ya Kusini ya kupambana na ufisadi. Vyombo vya habari vimeona kuwa, rais Mbeki alifanya uamuzi sahihi na kulinda sifa ya nchi yake.
Idhaa ya kiswahili 2006-06-15
|