Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-06-16 16:36:38    
EU yatakiwa kuwa na busara na ushujaa katika kuondoa vikwazo vya kuiuzia silaha China

cri

Mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya uliofanyika hivi karibuni uliamua kuahirisha mpango uliowekwa wa kuondoa vikwazo vya kuiuzia silaha China mwishoni mwa mwaka huu. Imedhihirika kuwa, Umoja wa Ulaya ulifanya uamuzi huo kutokana na shinikizo la Marekani. Lakini kuondoa marufuku ya kuiuzia China silaha ni ahadi ya kisiasa iliyotolewa na Umoja huo kwa China, Umoja wa Ulaya unatakiwa kutupia macho maslahi ya kipindi kirefu ya uhusiano kati yake na China, kupiga hatua mbele kwa kutumia busara na ushujaa.

Vikwazo vya Umoja wa Ulaya vya kuiuzia China silaha vilivyodumu kwa miaka 15 ni matokeo ya vita baridi, haviendani na hali mpya ya kukuza uhusiano wa ushirikiano wa kiwenzi kati ya China na Umoja wa Ulaya, Umoja huo unatakiwa kuondoa mapema vikwazo vinavyozuia ukuaji wa uhusiano huo. Mwaka 2003, rais Jaques Chiraq wa Ufaransa aliainisha kuwa, marufuku ya kuiuzia China silaha haiambatani na mkondo wa maendeleo, na inapaswa kuondolewa. Mwezi Desemba mwaka jana, mkutano wa wakuu wa Umoja wa Ulaya ulifanya uamuzi rasmi wa kuweka mada ya kuondoa vikwazo vya kijeshi dhidi ya China kwenye ajenda ya Umoja huo, na kufanya mwishoni mwa Juni Mwaka 2005 kama kikomo chake.

Lakini pendekezo hilo lilipingwa vikali na Marekani. Marekani ina wasiwasi kuhusu kuinuka kwa uwezo wa kiuchumi na hadhi ya kimataifa ya China, inataka kutumia jambo hilo kama njia moja ya kuzuia maendeleo kasi ya China. Zaidi ya hayo, maendeleo mazuri ya uhusiano kati ya China na Umoja wa Ulaya pia yanaitia wasiwasi Marekani, ili hadhi yake ya "nchi kubwa pekee" duniani isije ikatisika. Kwa hivyo, rais Bush wa Marekani alipotembelea Ulaya mwanzoni mwa mwaka huu aliwashinikiza viongozi wa Umoja wa Ulaya, na waziri wa mambo ya nje wa Marekani Bi. Condoleezza Rice hata aliwatishia kwa kuwawekea vikwazo au kuacha ushirikiano wa kijeshi kati yake na Ulaya. Imedhihirika kuwa, vikwazo vya kuiuzia China silaha vimekuwa hatua muhimu ya Marekani kuishinikiza China na kuchochea uhusiano kati ya China na Umoja wa Ulaya.

Wakati huo huo Uingereza ambayo ni mshirika mkubwa wa Marekani ilizishawishi nchi kadhaa za Ulaya Kaskazini kufuatana na msimamo huo wa Marekani. Hivyo Umoja wa Ulaya hatimaye ulichagua kuacha ahadi yake.

Chaguo hilo la Umoja wa Ulaya bila shaka ni hasara kubwa kwa uhusiano kati ya China na Umoja wa Ulaya. Pande hizo mbili ni washirika wakubwa ya kibiashara, zina maoni ya pamoja kuhusu masuala mengi ya kimataifa, na zina maslahi ya pamoja. Katika sekta ya kisayansi, China inashiriki kwenye mpango wa Galileo na mpango wa nishati ya nyuklia wa Umoja wa Ulaya. Lakini jambo la kusikitisha ni kwamba, Umoja wa Ulaya umesalimu amri kwa shinikizo la Marekani, na kuahirisha mpango wa kuondoa vikwazo vya kuiuzia China silaha. Jambo hilo si kama tu limeharibu maslahi ya China, bali pia limeharibu maslahi ya Umoja wa Ulaya wenyewe.

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya China alisema kuwa, China kuutaka Umoja wa Ulaya kuondoa vikwazo vya kuiuzia China silaha ni kwa ajili ya kutaka kuondoa ubaguzi wa kisiasa dhidi ya China, wala siyo kutaka kuingiza silaha kutoka nchi za Umoja huo. Kwa kweli, Umoja wa Ulaya unafahamu msimamo huo wa China, sasa jambo muhimu ni Umoja huo unatakiwa kuwa na busara na ushujaa, kupuuza shinikizo kutoka nje na kupiga hatua mbele ya kufuata ahadi yake.

Idhaa ya kiswahili 2005-06-16